Ni Ajib Yanga, hakuna namna

Ibrahim Ajib

Muktasari:

  • Wala si Laudit Mavugo wala Muivory Coast Fredrick Blagnon. Dante amewaaminisha Yanga kwamba hao wanakabika kirahiiisi kinoma wala hana mzuka nao.

KOCHA wa Yanga, Hans Pluijm humwambii kitu kuhusu beki wake, Andrew Vicent ‘Dante’. Anamsifia Dante kwa jinsi anavyopiga vichwa licha ya ufupi wake. Lakini beki huyo amewaambia Yanga kwamba hata wakikutana na Simba leo mchezaji anayeweza kuwasumbua ni Ibrahim Ajib.

Wala si Laudit Mavugo wala Muivory Coast Fredrick Blagnon. Dante amewaaminisha Yanga kwamba hao wanakabika kirahiiisi kinoma wala hana mzuka nao.

Dante alisema mtu wa kuchungwa katika safu ya ushambuliaji ya Simba ni Ajib ambaye ndiye mtu anayeweza kusababisha madhara kama akikosa mtu wa kumchunga na kwamba hilo wameshaliona na wanajua jinsi ya kulifanyia kazi wala hawatishiki na kelele na mbwembwe za Simba.

“Nimeiona Simba lakini niseme wazi hakuna kilichonishtua siwezi kuwahofia Mavugo na huyo Blagnon ni wazuri lakini kwangu dawa yao ipo labda Ajib, ndio anahitaji akili kucheza naye,”alisema Dante aliyesajiliwa kutoka Mtibwa.

“Ajib anajua kusumbua kama akikosa ulinzi na Yanga dawa yake tunayo, sasa kama Ajib akitulizwa hao wengine tuachiwe sisi mabeki tutamalizana nao kirahisi tu wala haina presha.”

MAVUGO AJIPANGA

Mavugo amecheza dakika 180 katika Ligi Kuu Bara kisha akagundua jambo moja ambalo amelipangia mkakati kwamba akifanikiwa atatisha kwa mabao. Akizungumza na Mwanaspoti kabla ya kupanda ndege akielekea kujiunga na timu ya taifa lake la Burundi alisema mechi mbili hizo zimempa akili kwamba bila mapambano ya nguvu hataweza kufunga mabao anayotaka.

“Kule kwetu Burundi mabeki wengi wanatumia akili zaidi hapa ni nguvu sana,hawataki kukupa nafasi ya kufanya kitu sasa nataka kuongeza nguvu ili nikabiliane nao,”alisema Mavugo.

“Naweza kufunga na hilo ndiyo lililonileta hapa Simba lakini kwasasa tunajipanga ili viungo wanijulie mipira ya kunipa wakati huo na mimi nataka kujiandaa kupambana na mabeki wanaotumia nguvu.”