Kili Queens wabishi kinoma

Muktasari:

  • Achana na timu ya Taifa ya Wanawake ya Twiga Stars ambayo hushirikisha wanasoka kutoka Tanzania Bara na wale wa Visiwani Zanzibar ila kuna Kilimanjaro Queens ambayo wachezaji wake hutokea Bara pekee na hii timu hushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki ‘Kombe la Chalenji’ upande wa wanawake ambayo imefufuliwa upya.

ASIKWAMBIE mtu soka ni mchezo wa kwanza unaopendwa na mashabiki wengi, japo zipo baadhi ya nchi mchezo huo unachukua nafasi ya pili ama ya tatu baada ya michezo mingine.

Ila sio kwa Tanzania. Soka linapendwa bwana, lakini wengi wanaoshabikia soka ni wale wanaopenda soka linalopigwa na wanaume huku soka la wanawake likiwa hawalipo katika kipaumbele sana.

Katika nchi yetu hii unaweza kusahau kabisa kama kuna soka la wanawake mara nyingi husikaka tu pale kunapokuwa na mashindano ama timu ikishiriki michuano fulani na hiyo tu ni kwa timu ya taifa kwani hakuna ligi ya wanawake ingawa Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF) lipo kwenye michakato ya kuianzisha.

Achana na timu ya Taifa ya Wanawake ya Twiga Stars ambayo hushirikisha wanasoka kutoka Tanzania Bara na wale wa Visiwani Zanzibar ila kuna Kilimanjaro Queens ambayo wachezaji wake hutokea Bara pekee na hii timu hushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki ‘Kombe la Chalenji’ upande wa wanawake ambayo imefufuliwa upya.

Michuano hii ni kama ile ambayo timu ya taifa chini ya miaka 23 ‘Ngorongoro Heroes’ hushiriki na kwa upande wa Zanzibar nao wanakuwa na timu yao, hapo kunakuwa hakuna undugu hata wakikutana kwenye mechi ya kuwania taji hilo.

Wiki hii michuano hiyo iliyoshirikisha nchi sita ilifanyika jijini Jinja, Uganda ambapo Kilimanjaro Queens imetwaa ubingwa huo uliachwa wazi na Zanzibar tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1986 na michuano hiyo kufa mwaka huo huo. Kili Queens ilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Kenya mabao 3-1.

Kili Queens ilipangwa kundi moja na timu ya Rwanda pamoja na Ethiopia wakati kundi lingine lilikuwa na timu za Kenya, Uganda na Zanzibar Quuens. Kundi la Kili Quuens lilikuwa gumu na ndiyo maana hakuna timu ambayo iliweza kupata mabao mengi yaani hakuna iliyowahi kushinda hata mabao matano katika mechi moja kutokana na kila timu kuwa imara tofauti na kundi ambalo Kenya ililopitia kufika fainali ambapo Zanzibar ilifungasha virago kwa jumla ya mabao 30. Zanzibar Queens iliweza hata kupigwa mabao zaidi ya kumi katika mechi moja.

Kilimanjaro Queens iliiondosha Uganda hatua ya nusu fainali kwa mabao 4-1 wakati Kenya waliifunga Ethiopia mabao 3-2 na kuzikutanisha timu hizo hatua ya fainali wakati Uganda ilicheza na Ethiopia kumpata mshindi wa tatu.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Edna Lema ‘Mourinho’ ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Twiga Stars  alifanya mahojiano na Mwanaspoti ambapo alielezea baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa na kuyafanyia kazi kabla ya michuano mingine kuanza itakayoshirikisha timu za wanawake.

MAANDALIZI

“Maandalizi yetu yalikuwa ya muda mfupi sana, kwani tulipata taarifa za sisi kushiriki michuano hiyo muda mfupi, hivyo hatukujiandaa vizuri ingawa tulijiamini tu kuwa tutafanya vizuri kwa kutumia uzoefu tulionao ikiwa ni pamoja na kuwajenga wachezaji kisaikolojia.

“Tuliondoka tukiwa tumeweka mikakati yetu, tulifika Bukoba ambapo tulicheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kuendelea na safari yetu, ni vigumu kuamini kwa mazingira ambayo tuliondoka nayo kuwa tungefanikiwa kubeba ubingwa huu mkubwa Afrika Mashariki,” anasema

ILIYOVYOKUWA JINJA

“Kundi letu lilikuwa gumu mno, tunamshukuru Mungu kutwaa ubingwa kwenye ardhi ya watu, ni mara chache mgeni kufanya vizuri sehemu ambayo si yake, ratiba ilibana sana, hivyo tulijiwekea malengo kuwa tucheze kwa kujituma lakini pia walitudharau pengine waliona hatutaweza, hivyo ni vitu ambavyo vilitutia hasira sana.

“Timu ilidharaulika kwasababu tu watu hawatupendi nadhani ni kutokana na jinsi tunavyofanya vibaya kwenye michuano mingine, hivyo tulipambana ili kufuta dhana hiyo kuwa Tanzania tunaweza. Uganda ilipotolewa walianza kutushangilia sisi kwani ilionyesha kuwa walikuwa na upinzani na Wakenya, tuliwalazimisha kutupenda kutokana na kiwango tulichokionyesha,”

YASAFIRI KWA BASI

Kuhusu changamoto ya safari yao, Edna alisema kuwa haoni kama ni tatizo kubwa sana kwani kwa nchi za Afrika ni jambo la kawaida ingawa inategemea na maandalizi ya nchi husika. Kili Queens ilikwenda Jinja kwa kutumia usafiri wa basi na jana Alhamis ilirejea kwa ndege ya Fastjet ikitokea Bukoba ambako timu hiyo iliondokea kwenda kwenye michuano hiyo.

“Hakuna tatizo lolote kusafiri kwa basi, safari yetu hii haijaharibu kitu na tumeifurahia hasa tuliporejea na ubingwa. Kenya walikuja na ndege lakini hawajatwaa ubingwa, hivyo nadhani matatizo ya usafiri ni changamoto kwa nchi zetu hizi za Afrika Mashariki, kikubwa tumepata kile tulichokihitaji.

“Safari yetu ilianzia Bukoba ambako tulikabidhiwa Bendera ya Taifa na mkuu wa Mkoa  huo, hivyo tulilazimika kupitia Bukoba kwa ajili ya kumkabidhi ushiriki wetu wenye mafanikio kama tulivyomahidi wakati tunakwenda huko,” anaeleza

VIONGOZI/ MASHABIKI

Ni wazi kwamba viongozi wengi wa soka nchini pamoja na mashabiki au wadau wa michezo huwekeza nguvu zao nyingi kwenye soka la wanaume kwa maana ya timu za taifa za wanaume hasa Taifa Stars ambayo ina mashindano mengi, hivyo husahau kuwekeza kwenye timu nyingine ambazo pia zinaiwakilisha nchi, Edna anasema:

“Tunahitaji sapoti kutoka sehemu mbalimbali kuanzia viongozi hadi mashabiki, wafanye kama vile wanavyoichukulia Taifa Stars japokuwa wengi wanaipenda timu hiyo kutokana na uwepo wa wachezaji wao wanaochezea timu za klabu zao.

“Hii ni timu ya taifa, inahitaji kupendwa na kutiwa moyo, si jambo rahisi kupata ubingwa ugenini, tulikosa ushirikiano wa mashabiki waliotutia moyo, Watanzania wanaoishi Uganda  walianza kuhamasika baada ya kuingia hatua ya nusu fainali tofauti na wenzetu ambao walipewa sapoti kubwa tangu mapema, hiyo yote ni kutokana na watu kutoipenda timu yao.

“Leo hii tumetwaa ubingwa imekuwa ni furaha ya nchi nzima ila tunawazawadia wanawake wote kombe hili, ila tunaomba viongozi wetu watuangalie kwa jicho la mbali, watoe kozi nyingi za ukocha kwa upande wa wanawake, tuwe na makocha wengi kama nchi za wenzetu ili tuweze kujiongoza wenyewe hata kama tutakuwa na makocha wa kiume lakini uwepo wetu kwenye timu ni muhimu sana.

“Hii hatua ni kubwa kwani hata nilipokuwa mchezaji wa Twiga Stars sikuwahi kuifikia hatua kama hii ambayo Kili Queens imefikia leo hii, hivyo ni jambo la kujipongeza ni hatua kubwa kwenye soka letu,” anasema Edna.