Kikosi cha Wenger cha miaka 20 Arsenal

LONDON, ENGLAND

ARSENE Wenger ametimiza miaka 20 tangu alipoanza kuinoa Arsenal. Jana Alhamisi alitimiza miongo yake hiyo miwili katika kikosi hicho cha Washika Bunduki wa London. Katika kipindi hicho cha huduma yake klabuni hapo amebeba mataji matatu ya Ligi Kuu England, sita ya Kombe la FA huku ikishuhudiwa mastaa kibao kutoka kila pembe ya duniani waliowahi kupita chini yake.

Tangu Wenger alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwaka 1996 na tangu hapo Arsenal imeshuhudia mafanikio makubwwa na kucheza soka tamu zaidi kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England.

Wenger amekuwa na nyakati tamu kwenye kikosi cha Arsenal ikiwamo kuwa na timu ile iliyochukua mataji mawili kwa msimu mmoja katika awamu mbili tofauti na kikosi chake kilichocheza msimu wote bila ya kupoteza mechi hata moja, Invincible. Je, ni kikosi gani bora zaidi kinachostaahili kuwa cha kwanza cha muda wote wa Wenger aliokuwa na Arsenal.

Kipa: David Seaman

Wakati alipowasili London, Wenger alilirithi kikosi cha Arsenal kikiwa na safu imara ya ulinzi ikiongozwa na kipa David Seaman. Hapo awali safu hiyo ya ulinzi ilionekana kuwa tatizo, lakini Mfaransa huyo aliibadilika na kuifanya kucheza kibingwa. Seaman alicheza kwa ubora mkubwa sana na kufanikiwa pia kuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England akiwa chaguo la kwanza golini.

Beki wa kulia: Lauren

Kwenye orodha ya mabeki wa kulia, Wenger amepata kuwa na wakali wawili bora kabisa katika wakati wake, Mcamerooni Lauren Etame Mayer na Lee Dixon. Lakini, Lauren alikuwa mtamu zaidi katika mabeki wa kati waliokuwa chini ya Wenger kwa kipindi hicho cha miongo miwili. Mcamerooni huyo alibadilishwa na Wenger kutoka kucheza kiungo wa kati hadi kuwa beki wa kulia na alicheza kwa mafanikio makubwa sana katika kikosi hicho cha Wenger. Kwenye nafasi hiyo amempiku pia Bacary Sagna.

Beki wa kati: Tony Adams

Huyu alifahamika kama Bwana Arsenal. Tony Adams alikuwa tayari alishabeba mataji kabla ya kuja kwa Mfaransa huyo, ambaye alimfanya kuwa nguzo yake imara kwenye safu ya ulinzi. Beki huyo Mwingereza licha ya kwamba alicheza chini ya Wenger katika zama za mwisho za maisha yake ya soka bado alikuwa mtu muhimu katika kikosi hicho wakati kilipobeba mataji mawili kwa msimu mmoja katika awamu mbili tofauti. Adams alikuwa nahodha wa vikosi hivyo vilivyobebeba mataji mawili kwa msimu mmoja kwa awamu pili tofauti.

Beki wa kati: Sol Campbell

Sol Campbell anatajwa kuwa ni usajili wa utata uliowahi kufanywa na Wenger kwa sababu beki huyo wa kati alijiunga kwenye timu hiyo akitokea kwa mahasimu wao Tottenham Hotspur. Campbell alisaidia kutwaa mataji mawili katika msimu wake wa kwanza klabu hapo na alikuwa sehemu muhimu ya safu ya ulinzi wa Arsenal ile iliyocheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mechi na alifunga pia bao kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Campbell alikuwa mchezaji wa kiwango cha dunia alipokuwa kwenye ubora wake na hapa anaingia kikosini akiwazidi Kolo Toure na Laurent Koscielny.

Beki wa kushoto: Ashley Cole

Licha ya kwamba Ashley Cole amekuwa adui kwa mashabiki wa Arsenal, lakini beki huyo wa kushoto haimzuii kuingia kwenye orodha ya nyota bora kabisa wanaopaswa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal ya miaka 20 chini ya kocha Wenger. Cole alikuwa beki wa pembeni anayeshambulia zaidi kuwahi kutokea kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Emirates kwa sasa. Ashley aliwatibua mashabiki wa Arsenal baada ya uamuzi wake wa kwenda kujiunga na Chelsea na kwenye nafasi hiyo anawazidi Nigel Winterburn, Gael Clichy na Nacho Monreal.

Kiungo wa kulia: Robert Pires

Wakati safu ya ulinzi ya kikosi hicho ikionekana kama kujieleza yenyewe tu, kwenye eneo la ushambuliaji mpambano ni mkali. Lakini, hakuna atakayeweza kuhoji uwepo wa staa wa Kifaransa, Robert Pires kwenye kikosi hiki. Pires alikuwa moto sana katika msimu wa 2001-02, akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu aliyechaguliwa na waandishi wa habari licha ya kwamba, kwa miezi kadhaa alikuwa nje ya uwanja kutokana na kuwa majeruhi. Alikuwamo pia kwenye kikosi kile kilichocheza bila ya kupoteza mechi na Pires ameondoka Arsenal akiwa gwiji. Kwenye kiungo hiyo ya kulia, amegombea nafasi na Ray Parlour na kumbwaga.

Kiungo wa kati: Patrick Vieira

Nahodha wa ukweli kabisa aliyewahi kutokea kwenye kikosi cha Arsenal chini ya Wenger. Patrick Vieira alikuwa fundi wa mpira, alicheza soka la staili zote akili na nguvu. Kwenye sehemu hiyo ya kiungo wa kati katika zama zake atashindana na Emmanuel Petit na Gilberto Silva, lakini huwezi kuona ni wapi utamweka benchi Vieira kwenye kikosi bora cha Arsenal cha miaka 20 iliyopita chini ya Mfaransa Wenger.

Kiungo wa kati: Mesut Ozil

Vita ya kumpata kiungo mwingine wa kati wa kucheza sambamba na Vieira ilikuwa kali, lakini Mjerumani Mesut Ozil anastahili kuwa kwenye safu hii. Viungo wa kukaba, Gilberto na Petit kwa bahati mbaya wameshindwa kupata  nafasi sambamba na fundi wa mpira Mhispaniola Cesc  Fabregas. Ozil tangu  alipotua Arsenal akiwa mmoja wa wachezaji ghali kabisa kusajiliwa na Wenger, Mjerumani huyo ameongeza kitu tofauti kwenye timu na hicho kimewafanya kushika namba nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Kiungo wa kushoto: Marc Overmars

Chaguo jingine gumu kwenye kikosi hiki. Unawezaje kumweka benchi Freddie Ljungberg katika kikosi cha kwanza cha Arsenal ya miaka 20 iliyopita?. Lakini, kama ulipata kumwona Marc Overmars katika miaka yake ya kwanza kwanza kabisa Wenger alipotua Arsenal utatambua kwanini Mdachi huyo anastahili kuwamo kwenye kikosi hiki. Kasi, akili na umaliziaji mzuri ilikuwa silaha kubwa ya Overmars kuwatesa mabeki wa Ligi Kuu England hadi hapo alipokwenda kujiunga na Barcelona. Staa mwingine aliyefanikiwa kumweke benchi kwenye eneo hilo ni Alexis Sanchez.

Mshambuliaji: Dennis Bergkamp

Mdachi mwoga wa kupanda ndege, lakini hajawahi kuwa mwoga wa kufanya yake ndani ya uwanja. Fowadi huyo aliyekuwa fundi wa mpira alitamba sana katika nusu ya kwanza ya miaka 20 ya kocha Wenger kwenye klabu hiyo ya Arsenal. Bergkamp alikuwa fundi wa kufunga mabao, kupiga chenga na pasi za mwisho zilikuwa hatari zaidi kwa wapinzani. Ushawahi kuona ile chenga yake aliyowapiga mabeki wa Newcastle, hadi sasa imebaki kuwa video ya kumbukumbu katika soka la England.

Mshambuliaji: Thierry Henry

Kinara wa mabao wa nyakati zote katika kikosi hicho cha Arsenal. Fowadi huyo Mfaransa ni nahodha mwingine wa mfano aliyewahi kutoka katika kikosi hicho chini ya kocha Wenger. Henry ana rekodi nyingine tamu akiwa miongoni mwa wapiga asisti nyingi kwenye Ligi Kuu England. Kocha Wenger ameshawahi kuwa na orodha ndefu ya washambuliaji wa kati kuanzia Ian Wright, Nicolas Anelka, Nwankwo Kanu, Sylvain Wiltord, Robin van Persie na Olivier Giroud, lakini Henry alikuwa wa aina yake. Amewafunika wote hao.

Watakaokaa kwenye benchi

Kila timu yenye kikosi cha kwanza lazima kuna mastaa wengine watakaa benchi. Mastaa wanaokaa kwenye benchi katika kikosi hicho cha Arsenal ya Wenger ya miaka 20 ni kipa Jens Lehmann, mabeki Martin Keown, Laurent Koscielny, viungo Gilberto Silva, Cesc Fabregas, Freddie Ljungberg na washambuliaji Nicolas Anelka na Robon van Persie.