Kichuya anakabika? Unaumwa wewe

Muktasari:

Hata hivyo, tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti imebaini kuwa winga huyo hakabiki na hata ukimpania vipi akiamua kukufunga atakufunga tu. Kichuya tayari amezifunga timu sita kati ya tisa alizocheza nazo msimu huu.

MABEKI wa baadhi ya timu za Ligi Kuu wametangaza kiama kwa Shiza Kichuya. Wamedai kuwa mabeki aliowasumbua mpaka sasa ni hao hao na hataweza kuwa hatari kwani watamkaba vilivyo katika mechi zijazo ili asilete madhara.

Hata hivyo, tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti imebaini kuwa winga huyo hakabiki na hata ukimpania vipi akiamua kukufunga atakufunga tu. Kichuya tayari amezifunga timu sita kati ya tisa alizocheza nazo msimu huu.

Alianza kwa kuifunga Ndanda ya Mtwara na kisha akazifunga Azam, Majimaji, Yanga, Mbeya City na Kagera Sugar. Baada ya kuzifunga timu hizo amekaa kileleni katika chati ya wafungaji bora akiwa na mabao saba.

Mwanaspoti linakuletea tathmini ya mabao matano ya Kichuya kuonyesha namna alivyotumia uwezo na akili nyingi kuwafunga wapinzani hao.

 

Dhidi ya Ndanda

Bao lake la kwanza msimu huu. Kichuya alifunga bao hilo akirejesha mpira uliokuwa umeokolewa na kipa wa Ndanda, Jackson Chove kutokana na kona ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Kichuya alikaa pembeni kidogo ya wachezaji wengine kama hana habari na kona hiyo lakini baada ya Chove kuupangua mpira, Kichuya aliulaza mguu wake wa kushoto na kuachia shuti kali ambalo lilikwenda moja kwa moja wavuni. Bao hili ni miongoni mwa mabao bora zaidi yaliyofungwa Ligi Kuu msimu huu.

 

Dhidi ya Azam

Baada ya kukaa mechi tatu bila kufunga, Kichuya alirejesha makali yake katika mchezo na Azam na alifunga moja ya mabao bora pia. Wakati Azam ikiwa imejiaminisha kuwa inaweza kuondoka na pointi walau moja dhidi ya Simba, Kichuya alipokea kwa ustadi mpira wa kichwa uliopigwa na Javier Bokungu na kuutuliza gambani kisha akaupeleka kwa ufundi katika ukingo wa goli na kufunga.

Kipa wa Azam, Aishi Manula ambaye ndiye kipa bora zaidi nchini kwa sasa alishindwa kuufikia mpira na kuishuhudia timu yake ikilala kwa bao 1-0.

 

Dhidi ya Majimaji

Achana na bao la penalti alilofunga katika mchezo huu. Bao lake la pili lilikuwa murua zaidi ambapo aliichangamkia pasi ndefu ya Jonas Mkude na kuwazidi kasi walinzi wa Majimaji kabla ya kukutana na kipa Amani Simba na kumfunga kirahisi. Mabeki wa Majimaji walikuwa wakijaribu kucheza ‘offside trick’ lakini Kichuya alikaa nyuma yao na kuchomoka kwa kasi ambayo iliwashinda mabeki hao.

 

Dhidi ya Yanga

Ally Mustapha ‘Barthez’ pengine mpaka sasa haelewi ni kitu gani kilitokea hadi akafungwa bao lile. Kichuya alipiga kona ambayo ilikwenda moja kwa moja wavuni huku Barthez akiruka bila mafanikio yoyote.

Wachezaji wa Yanga walidhani kuwa Kichuya anapiga kona ya kawaida lakini akauzungusha mpira ambao ulikwenda na kuingia katika nyavu ndogo na kuipatia timu yake bao la kusawazisha.

 

Dhidi ya Mbeya City

Pamoja na beki wa Mbeya City, John Kabanda kuambiwa kuwa kazi yake uwanjani ni kumlinda Kichuya tu na asijihusishe na ishu nyingine, alijikuta akizidiwa kasi baada ya Jonas Mkude kupiga pasi ndefu kwa winga huyo. Kichuya baada ya kumzidi kasi Kabanda aliumiliki mpira na kusogea eneo la hatari kabla ya kufunga kwa shuti kali ambayo lilimfanya kipa wa Mbeya City, Owen Chaima kukosa cha kufanya.

 

Mguu wa kushoto

Mabao yote saba ya Kichuya msimu huu amefunga kwa kutumia mguu wake wa kushoto jambo ambalo ni adimu kwa washambuliaji kuweza kufanya hivyo. Mabao yote matano ya kawaida aliyafunga kwa mguu huo pamoja na mawili ya penalti ambazo pia alipiga kwa mguu wa kushoto.