Kariakoo mpango mzima

Muktasari:

  • Kwa kifupi timu ambazo zinapatikana Kariakoo ni Simba, Yanga, Cosmopolitan, Pan African na Nyota Nyekundu.

KAMA ulikuwa hufahamu ni kwamba ukifika jijini Dar es Salaam na ukaondoka bila kutembelea eneo la Kariakoo ni sawa tu na hujafika mjini. Kwa Dar es Salaam Kariakoo ndiyo kila kitu.

Kariakoo kunauzwa ubuyu, karanga, mchele, nguo, baiskeli, pikipiki hadi Magari. Kila bidhaa unayoifahamu nchini inapatikana Kariakoo. Kariakoo ndiyo eneo pekee ambalo lina vitu feki na orijino. Lina kila kitu ambacho kinayapendeza ama kuyachukiza macho ya mwanadamu. Pia Kariakoo ndio eneo ambalo unapaswa kuwa makini kuliko kwingine kwani ukizubaa tu, umeachwa.

Katika soka la Tanzania, Kariakoo ndiyo kila kitu. Timu nne kati ya tisa ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara zinapatikana Kariakoo ambayo kwa siku inakadiriwa kutembelewa na watu zaidi ya elfu 50 ili kupata mahitaji mbalimbali.

Kwa taarifa yako ni kwamba timu za Kariakoo peke yake zimetwaa mataji 46 ya Ligi Kuu Bara Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965.

Kwa kifupi timu ambazo zinapatikana Kariakoo ni Simba, Yanga, Cosmopolitan, Pan African na Nyota Nyekundu. Yanga ndiyo vinara wa timu za Kariakoo ikiwa imetwaa mataji 26 ya Ligi Kuu na kufuatiwa na Simba iliyotwaa mara 18 wakati Cosmo na Pan zimetwaa mara moja moja, wakati Nyota Nyekundu haina kitu.

Yanga

Hawa ndiyo wababe wa Kariakoo wakiwa wameshinda mataji mengi zaidi miongoni mwa timu za mitaa hiyo yenye pilika pilika nyingi za biashara.

Yanga makao makuu yake yako makutano ya mtaa wa Jangwani na Twiga (kama unavyoona katika ramani).

Timu hiyo ilianzia mitaa hiyo mwaka 1935 ambapo Kariakoo haikuwa mji mkubwa, ni kama ilivyo Kigamboni ama Bunju kwa sasa.

Kwa kufahamu ukubwa wa klabu hiyo, Yanga ilianzia Mtaa wa Mafia kabla ya kuhamia mitaa iliyopo sasa ambapo pia ilijenga uwanja mdogo wa Kaunda katika eneo hilo pamoja na ofisi za makao makuu ya timu. Kutokana na kukua kwa mji eneo ambalo Yanga ilijipambanua kama makao yake makuu sasa imekuwa katikati ya mji lakini uwanja wake wa Kaunda umekumbwa na mkondo maji na sasa upo katika eneo la mafuriko.

Simba

Timu hiyo ndiyo iko katika eneo zuri zaidi la kibiashara katika mtaa wa Msimbazi katikati kabisa ya Kariakoo.

Katika eneo hili Simba imejenga majengo mawili ya ghorofa na imepangisha kwa wafanyabiashara ambapo kwa mwaka timu hiyo inapata zaidi ya Sh250 milioni kama kodi ya pango tu. Pembeni kidogo ya makao makuu ya Simba kuna kituo cha Polisi cha Msimbazi halafu ukitembea kidogo unakutana na Ukumbi maarufu wa DDC.

Miongoni mwa timu za Kariakoo, Simba ni ya pili kwa mafanikio ikiwa imetwaa taji la Ligi Kuu mara 18 lakini pia ndiyo timu inayoongoza kwa kutwaa taji la Kagame, imetwaa mara sita. Hasara kwa Simba ni kwamba haikuweza kuwa na uwanja wa mazoezi katika eneo hili na inategemea eneo lao la Bunju lililopo nje kidogo ya Dar es Salaam.

“Hakukuwa na namna nyingine zaidi ya kuanzisha timu Kariakoo. Wakati Simba inaanzishwa Kariakoo ilikuwa ndio Dar es Salaam yenyewe, maeneo mengine yaliyokuwa yameendelea ni Magomeni na Ilala,” anaeleza Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.

“Uzuri ni kwamba Simba ilifanikiwa kuwepo katika mtaa wa Msimbazi ambao kibiashara ndiyo mtaa wenye thamani kubwa zaidi Kariakoo, hata hivyo hatukuweza kuwa na majengo mengi ambayo yangeweza kuwa faida kubwa zaidi kwetu.

“Kwa sasa tunatazama mbele, mabadiliko yanayofanyika sasa kwenye mfumo wa uendeshaji wa klabu yanaweza kutusaidia kujipambanua kibiashara. Majengo yetu mawili yaliyopo Kariakoo tunaweza kuyatumia kwa kuingia ubia na taasisi kama benki na tukapata fedha nyingi zaidi,” anaeleza Manara ambaye ni mzaliwa wa Kariakoo pia.

Cosmopolitan

Timu hii ni miongoni mwa timu kongwe zaidi nchini na imekuwa na historia kubwa. Chimbuko la timu hii ni mtaa wa Mafia na Mkunguni (kama unavyoona katika ramani). Kutokana na wingi wa majengo pamoja watu katika eneo la Kariakoo, ukitoka yalipo makao makuu ya Simba ni vigumu kupata njia ya moja kwa moja kufika makao makuu ya Cosmo bila kuelekezwa na wenyeji.

Kama huifahamu Cosmo vizuri, timu hii ndiyo ya pili kutwaa taji la Ligi Kuu Bara, ilifanya hivyo mwaka 1967. Ikumbukwe kuwa Simba ilikuwa ya kwanza kutwaa taji hilo mwaka 1965 na kulitetea mwaka uliofuata.

Mmoja wa Wadhamini wa Cosmo, Hanin Seif anasema timu hiyo ilianzishwa baada ya wakereketwa kadhaa wa soka kukutana na kuamua kuunda timu ambayo iliibuka na kuwa miongoni mwa timu kubwa Tanzania.

“Naweza kusema Kariakoo ndiyo kitovu cha soka la Tanzania. Tofauti na timu nyingine zilizoanzia Kariakoo, Cosmo haikuwa ikifungamana na upande wowote. Ilianzishwa na juhudi za baadhi ya watu na imeendelea kuwa timu imara,” anasema Seif.

“Kilichoishusha Cosmo baadaye ni siasa za mpira tu, mpira una misingi yake hivyo yalipoanza kuingia mambo ya siasa ikawa ngumu kufanya vizuri. Hata hivyo, sasa kazi kubwa inafanyika kuirejesha kwenye ramani,” anafafanua Seif.

Pan African

Timu nyingine iliyoweka historia nchini ambayo inatoka Kariakoo ni Pan African ambayo makao yake makuu yapo mtaa wa Swahili. Timu hiyo ilitoka ubavuni mwa Yanga katika mgogoro mkubwa wa mwaka 1975 ambapo mastaa zaidi ya 13 waliamua kuachana na timu hiyo ya Jangwani na kujiunga na timu ya Nyota Afrika ya Morogoro.

Mpasuko huo wa Yanga ulipelekea kununuliwa kwa timu moja ya Veterani ambayo ilibadilishwa jina na kuitwa Pan hivyo kuingia moja kwa moja Ligi Daraja la Kwanza.

Saad Matteo ambaye ni mmoja wa viongozi wa Pan anasema kutokana na sheria za wakati huo kuiruhusu timu yenye wachezaji 10 wa timu ya Taifa kupanda moja kwa moja katika Ligi Kuu (wakati huo Ligi Daraja la Kwanza), wachezaji hao walihama kutoka Nyota Afrika na kuhamia Pan ambayo iliwenda moja kwa moja kushiriki Ligi.

“Sheria ya timu yenye wachezaji 10 wa timu ya taifa kwenda moja kwa moja Ligi Kuu ilitubeba na Pan ikapewa nafasi hiyo.

Hii ilikuwa mwaka 1975 ambapo Yanga iligawanyika vipande viwili na wachezaji hao kuhama,” anaeleza Matteo.

Pan ilikaa kwenye ligi kwa miaka saba na kufanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu mwaka 1982 hivyo kuwa miongoni mwa timu chache nje ya Simba na Yanga zilizofanikiwa kutwaa taji hilo lenye heshima zaidi katika soka la Tanzania.

“Timu baadaye ilipata changamoto kwanza kutoka kwa Yanga yenyewe ambayo haikutaka kuona tunafanikiwa.

Pili wachezaji waliohama walianza kuchoka na kizazi kilichofuata hakikuwa na moyo wa ushindani kama watangulizi wao, timu ikaanza kushuka na kuporomoka kabisa,” anafafanua kiongozi huyo.

Nyota Nyekundu

Timu yenye simulizi tamu miongoni mwa timu za Kariakoo ni Nyota Nyekundu (Red Stars). Kwanza kama ilivyo Pan Africans, timu hii ya Nyota Nyekundu nayo ilitoka ubavuni wa klabu kubwa nchini, Simba lakini haikuweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu hata mara moja.

Simba iliingia katika mgogoro mkubwa mwaka 1975 na mwaka uliofuata ikazaliwa klabu hiyo iliyopo mtaa wa Congo ambayo hata hivyo haipo tena.

Nyota Nyekundu ilifanikiwa kujipambanua na kununua jengo mtaa wa Kongo pale Kariakoo lakini haikuweza kushindana na kubaki katika ligi.

Kwa sasa waliokuwa viongozi wa timu hiyo wamekuwa wakigawana kodi ya pango ya jengo -hilo na kuendesha maisha yao mjini.