REKODI: Kante akaribia kufuata nyayo za mastaa hawa

N’golo Kante

Kuzaliwa:    Machi 29,  1991  
Mahali:     Paris, Ufaransa
Urefu:     Futi 5, inchi 6  
Nafasi:     Kiungo
Klabu:     Chelsea
Jezi:     Namba  7
Taifa:     Ufaransa

Muktasari:

  • Endapo Chelsea itachukua ubingwa, Kante atakuwa amejiweka katika rekodi moja na mastaa hawa kuchukua mataji ya Ligi Kuu England na klabu mbili tofauti.

LONDON, ENGLAND. KIUNGO wa Chelsea, N’Golo Kante anaonekana kufukuzia kwa kasi ubingwa wa pili mfululizo akiwa na Chelsea baada ya msimu uliopita kutwaa ubingwa huo na Leicester City. Endapo Chelsea itachukua ubingwa, Kante atakuwa amejiweka katika rekodi moja na mastaa hawa kuchukua mataji ya Ligi Kuu England na klabu mbili tofauti.

Henning Berg

Mlinzi wa zamani wa kimataifa wa Norway ambaye aliweka heshima Manchester United. Berg alikuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivi baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na Blackburn Rovers msimu wa 1994/95 baadaye alipotua Manchester United alitwaa tena msimu wa 1998/99 na ule wa 1999/2000.

Nicolas Anelka

Kinda wa zamani wa Arsenal ambaye Arsene Wenger alimnunua klabuni hapo akitokea PSG ya Ufaransa. Anelka alitwaa taji lake la kwanza na Arsenal msimu wa 1997/98, lakini baada ya kuzurura huku na kule alijikuta akitwaa tena taji hilo miaka 12 baadaye akiwa na kikosi cha Chelsea  msimu wa 2009/10 chini ya Kocha Carlo Ancelotti. Taji lake la kwanza na Arsenal alitwaa akiwa na miaka 19 wakati lile Chelsea alilitwaa akiwa amepitisha miaka 30.

Ashley Cole

Staa mwingine aliyefuata nyayo za Anelka. Ashley alikuwa mlinzi wa kutegemewa wa kushoto wa Arsenal wakati ilipotwaa taji msimu wa 2001/02. Baadaye alitua Chelsea na miaka minane baadaye alitwaa tena taji hilo msimu wa 2009/10 akiwa katika kikosi cha Chelsea.

Kolo Toure

Staa mwingine aliyeondoka Arsenal kwenda kwingine kutafuta mataji na kweli akayapata.

Toure ni mwanachama wa kikosi cha Arsenal kilichocheza msimu mzima bila ya kupoteza mechi (Invincible) msimu wa 2003/04 na kutwaa taji hilo. Pia alikuwa katika kikosi cha Manchester City ambacho kilitwaa ubingwa wa msimu wa  2011/12 kwa bao la kushangaza la dakika za majeruhi la mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina Sergio Aguero.  Mwaka 2014, Kolo angeweza kuwa mchezaji wa kwanza katika Ligi Kuu England kutwaa mataji na timu tatu tofauti kama Liverpool ingemalizia mwendo wake vyema lakini ikachemsha katika dakika za majeruhi.

Gael Clichy

Nyota mwingine wa Arsenal ambaye safari ya kwenda Manchester City ilimsaidia aingie katika historia ya kutwaa mataji na klabu mbili tofauti.

Kama ilivyo kwa Toure na yeye alikuwepo katika kikosi cha Arsenal kilichocheza msimu mzima bila ya kupoteza mechi 2003/04 na kutwaa taji hilo. Baadaye alihamia Manchester City na kutwaa mataji mawili misimu ya 2011/12 na 2013/14. kwa kifupi Mfaransa huyu amefanikiwa kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ndani ya miaka 10 tu.

Carlos Tevez

Nyota wa kimataifa wa Argentina, ambaye mataji yake yote matatu aliyapata katika Jiji la Manchester ndani ya miaka mitano tu. Baada ya kuhama West Ham na kwenda Man Unite, Tevez alitwaa mataji mawili katika misimu ya 2007/08 na 2008/09.

Baadaye alihamia kwa majirani Manchester City na kwenda kutwaa lile taji la msimu wa 2011/12 sawa na ilivyo kwa Toure na Clichy.

Robert Huth

Mlinzi nguli wa Ujerumani ambaye alipelekwa England akiwa kinda na klabu ya Chelsea. Kama Kante akichukua ubingwa msimu huu na Chelsea basi atakuwa amefuata nyayo za rafiki yake wa msimu uliopita Huth ambaye alitwaa na klabu zote mbili Chelsea na Leicester City. Huth alitwaa taji lake la kwanza na Chelsea msimu wa 2004/05 kisha msimu uliofuata wa 2005/06. Miaka kumi baadaye msimu uliopita alitwaa taji hilo katika moyo wa safu ya ulinzi ya Leicester msimu wa 2015/16.

Mark Schwarzer

Kama ilivyo kwa Huth na Kante basi ndivyo ambavyo ilivyo kwa kipa huyu wa kimataifa wa Australia. Wote hawa wanakuwa wachezaji ambao wametwaa mataji mawili na klabu mbili tofauti ambazo ni Chelsea na Leicester City.  Schwarzer ni mchezaji wa kwanza katika orodha hii kutwaa mataji na klabu mbili tofauti kwa misimu miwili mfululizo. Kama Kante akifanya hivi msimu huu hatakuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo. Awali Schwarzer alitwaa ubingwa na Chelsea msimu wa 2014/15 na kisha msimu uliofuata ambao ni msimu uliopita akatwaa na Leicester 2015/16.