Juma Amir : Pele wa Mwanza aliyekatishwa soka kimaajabu

Muktasari:

Majina yake kamili ni Juma Amir Maftah, nyota wa zamani wa timu za Coop United, Pamba Mwanza, Simba na Taifa Stars.

HAKUPEWA jina la Pele wa Mwanza kuwa kubahatisha, hapana! Hii ilitokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza soka na hasa katika kupiga chenga, mbio na kufunga mabao yake kiufundi kama ilivyokuwa kwa gwiji wa Brazili, Pele.

Majina yake kamili ni Juma Amir Maftah, nyota wa zamani wa timu za Coop United, Pamba Mwanza, Simba na Taifa Stars.

Kwa mashabiki wa Yanga unapolitaja jina la Juma Amir, mioyo yao inashtuka na kusisimka kutokana na ukweli alikuwa mmoja ya mastraika waliokuwa wakiikosesha raha timu yao kwa umahiri wake dimbani.

Amir aliyejiunga na Simba mwaka 1994 na kudumu nao kwa misimu mitano mfululizo kabla ya kutundika daluga bila kupenda mwanzoni mwa miaka ya 2000 anathibitisha kuwa siku zote kupanga sio kuchagua.

Straika huyo wa kimataifa, alikuwa na ndoto zake nyingi katika soka na alipanga malengo kadhaa katika maisha yake ya soka akiota kufika mbali zaidi na kunyakua tuzo ili kujenga heshima, lakini mambo yalienda sivyo ndivyo.

Mwenyewe anakiri kwamba alikuwa na ndoto za kuendelea kucheza soka, ili kufurahia kipaji chake alichokihangaikia utotoni, huku akikumbana na vikwazo kutoka kwa baba yake aliyetaka ajikite kwenye mafundisho wa kidini zaidi.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalum yaliyozaa makala haya, Amir, aliyekuwa akisifika kwa umahiri wake wa kusakata kandanda na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu, amefunguka mambo mengi ya kusisimua.

Kubwa kati ya hayo ni jinsi anavyosikitika mpaka leo kwa kitendo cha kuvunjwa mguu na mchezaji ambaye mpaka leo hajamtambua katika pambano la kirafiki na kujikuta akikatishwa ndoto alizokuwa amejiwekea kwenye soka. Ilikuwaje?

Songa naye katika simulizi hili la kusisimua linalozungumzia maisha na safari yake ya soka tangu utotoni mpaka alipo kwa sasa akiendesha shughuli zake jijini hapa.

KIVIPI ALIKATISHWA NDOTO?

Mkali huyo aliyeanza soka tangu akiwa kinda jijini Mwanza, anasema hawezi kulisahau tukio lililokatisha ndoto zake za soka akiwa bado hajaamua kupumzika soka baada ya kukumbwa na kisanga cha ajabu uwanjani.

Amri anasema akiwa ndio kwanza ana msimu wa tano tangu ajiunge na Simba akitokea Pamba ya Mwanza mwaka 1994, alijikuta akivunjwa mguu wa kulia na kulazimika kuachana na soka bila kupenda.

Anasema anakumbuka ilikuwa ni katika mechi ya kirafiki kati ya Simba na Zaragoza FC (Moro United) ambapo wakati akipokea pasi ya mchezaji mwenzake bila kutegemea alijikuta amevamiwa na mchezaji wa timu pinzani.

“Bora angenivamia tu, lakini mchezaji huyo ambaye sikujua hata ametokea wapi alinichomekea miguu yake kwa ndani na kuniangusha,” anasema.

Amiri anasema mpaka refa alipopuliza kipyenga ili kwenda kumjulia hali pale alipokuwa ameanguka, tayari alikuwa akihisi mguu wa umekufa ganzi, baada ya awali kusikia maumivu ambayo hakuwahi kuyasikia maishani mwake.

“Mguu ilikufa ganzi na nilipokuja kutolewa uwanjani ili kwenda kupata matibabu ndio ikawa mwisho wangu wa kucheza soka, yaani kiutani utani tu nilipumzishwa soka bila kutarajia,” anasema.

MIAKA MIWILI YA MATESO

Amir anasema kabla ya maamuzi ya kuachana na soka, aliteseka kwa miaka miwili nje ya uwanja akijiuguza mguu huo. Anasema mpaka sasa analiona tukio lililomtokea ni kama miujiza kwake, kwani hakutarajia hakumbane hali hiyo.

“Huwezi amini kwa miaka miwili sikucheza kwa sababu ya kuuguza mguu huo ambao ulivunjika kiajabu kabisa, hivyo malengo na ndoto zake za kuichezea Simba na Taifa Stars kwa mafanikio makubwa zaidi yakaishia hapo.”

“Yaani siku hiyo sitaisahau kabisa, ilikuwa mechi ya kirafiki kati ya Simba na

Zoragoza ambayo baadaye ilikuja kufahamika kama Moro United, kitendo cha kuchomekewa mguu na kuanguka sikuweza tena kuinuka na kucheza soka.”

Anaongeza kuwa licha ya kuacha soka bila kupenda, lakini mpaka leo hamjui aliyemharibia na lau angemjua hata leo angetaka maelezo kutoka kwake kwanini alimtatishia ndoto zake wakati hakuwa amefika alipopataka.

“Miaka mitano niliyocheza Simba haikuwa mingi na kwa ukweli kabisa nilikuwa mmoja ya wachezaji wenye vipaji ambaye niliamini nilikuwa na nafasi ya kunyakua mataji na tuzo nyingi kama ambavyo Diamond Platinumz anavyotamba leo na kunyakua tuzo kwenye muziki wa kizazi kipya,” anasema.

ALIKOTOKEA

Straika huyo ambaye ana uhusiano wa kindugu na nyota mwingine wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah, anasema alianza kucheza soka tangu akiwa na miaka sita wakati huo akisoma madrasa ya Jamhuria iliyopo jijini hapa.

“Baba yangu hakutaka kabisa mimi nicheze soka kwa sababu alipenda nikijite zaidi kwenye mafundisho ya kidini, lakini nilikuwa najiiba na watoto wenzangu na kucheza kwa siri, kwa vile nilipenda soka sio utani,” anasema.

Anasema anakumbuka kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka sita tu na alikuwa akiichezea timu hiyo ya madrasa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Sahara na alikuwa akitupia sana kambani dhidi ya timu pinzani walizokutana nazo.

Anazikumbuka timu walizokuwa wakichuana nazo na kuonyesha umahiri wake wa kufunga kuwa ni Igogo, Uhuru na Rufiji.

Amir anasema mzuka wa soka ulitokana zaidi na mafanikio makubwa ya nyota kadhaa walioibuka jijini humo na kutamba nchini kama kila Athuman Juma Chama ‘Jogoo’, Majid Tall, Mashaka Magongo na Hussein Masha na wengine.

HAIKUWA KAZI RAHISI

Nyota huyo wa zamani anakiri kuwa, haikuwa rahisi kucheza mpira kutokana na baba yake kutotaka kabisa acheze, kwani licha ya kupenda ajikite kwenye dini, lakini alikuwa akihofia asiumizwe kwa kucheza na wachezaji waliomzidi umri.

“Baba alikuwa akihofia nitaumizwa kwa kucheza na wakubwa, pia alikuwa anapenda sana nifuate nyayo zake katika masuala ya kidini, kwani alikuwa Imamu wa Msikiti wa Raudhwa uliopo Mtaa wa Lumumba,” anasema.

“Hivyo alikuwa anapinga kitendo cha mimi cha kuchanganya dini na michezo na kunisisitizia zaidi kukomaa na mafundisho ya dini, lakini soka lilinielemea.”

Anasema hata hivyo, msimamo wake wa kupenda soka ulimfanya baba yake kuja kusalimu amri na kumuacha acheze, hasa baada ya kukingiwa kifua na mwamuzi wa zamani wa kimataifa, Kassim Chona aliyekuwa swahiba mkubwa wa baba yake.

Unadhani mwamuzi huyo alimkingia kifua vipi na kumlainisha Sheikh Maftah, aliyewahi kuwa Sheikh wa Wilaya ya Mwanza mpaka kukubali kumruhusu Amir kujikita kwenye soka na kuja kuwa mkali akitamba na klabu mbalimbali na timu ya taifa? Ungana naye Jumanne ijayo ili upate majibu kamili.