Jangwani hamsomeki mjue

Muktasari:

ASIKUAMBIE mtu, soka bwana ni mchezo mtamu sana kuuangalia na hata kuucheza, achilia mbali kuuongoza.

ASIKUAMBIE mtu, soka bwana ni mchezo mtamu sana kuuangalia na hata kuucheza, achilia mbali kuuongoza.

Hata hivyo mchezo huu una changamoto zake, kwani wakati viongozi wakijitapa kwa hili na lile kuwa timu imefanya maandalizi kabambe kwa mechi husika, lakini kumbe wachezaji wala hawana habari na kusababisha mambo kwenda kombo.

Kuna wakati wachezaji wanaweza kuoneka na kuwa imara, lakini tatizo likawa kwa viongozi na wakati viongozi wakiwa makini, wachezaji wanavuruga na wakati mwingine benchi la ufundi nalo likawa na matatizo mkubwa kadhalika.

Ndivyo mnapoweza kuona makocha wakitimuliwa ovyo na viongozi na kuiacha mishahara minono ya kila mwezi.

Hebu itazame Yanga kwa sasa, ni timu iliyokamilika kila idara, ikiwa na viongozi makini chini ya Mwenyekiti Yusuf Manji, ambaye hana choyo kabisa pale linapokuja swala la mafanikio ya timu.

Yanga hii ina benchi la ufundi imara kabisa chini ya Kocha Hans Pluijm, mkongwe na mzoefu wa soka la Afrika akisaidiwa na Juma Mwambusi, huyu ni miongoni mwa makocha bora kabisa hapa nchini akiwa na leseni A ya CAF. Benchi hilo pia lina Juma Pondamali, kocha mzoefu wa makipa hapa nchini.

Upande mwingine Yanga ina kikosi bora kabisa msimu huu kikiundwa na wachezaji mahiri katika idara zote zikiwa zimekamilika, hapo ndipo wengi wanakubali kuwa huu ni mwaka wa Yanga labda wenyewe tu wajichanganye.

 

MOTO WA YANGA

Yanga ijichanganye yenyewe tu kwa hali ilivyo na labda kama haitaandaliwa vema kisaikolojia kufikia ndoto za mashabiki wake, timu hiyo ya kutisha nchini na Afrika kwa ujumla.

Hata hivyo kama hujui ni kwamba Yanga ina kauli mbiu yake isemayo ‘Yanga Imara Daima Mbele Nyuma Mwiko’.

Kauli mbiu hii imekuwa ikitumiwa na Yanga tangu klabu hiyo ilipoanzishwa mnamo mwaka wa 1935, je viongozi, wanachama, wachezaji na mashabiki wa timu hii wamekwisha kuitafsiri kauli hii?

Yanga kwa uelewa wa wachache ilianzishwa chini ya wito huu ikimaanisha kujenga klabu imara itakayoongozwa na viongozi imara walio na mipango imara na makini ili kujenga timu imara yenye wachezaji imara ili iwe mbele daima na nyuma mwiko.

Klabu hii kama lilivyo jina lake la Dar Young Africans haikulenga kutawala jiji la Dar au Tanganyika na baadae Tanzania peke yake shabaha na malengo ya msingi ni kutawala soka la Afrika.

Hapa ndipo wazee na wakongwe wa timu hii na hata wachambuzi makini wa soka hapa nchini wamekuwa wakijiuliza hivi kweli wito huu wa Yanga imara daima mbele nyuma mwiko unaeleweka vizuri kwa wadau wa klabu hiyo wakiwamo viongozi, wanachama, mashabiki, wachezaji na wachezaji wa timu hii?

Yapo mashaka kuwa wengi wamekosa uwezo wa kuutafsiri wito huo. Ukifuatilia soka la Uingereza unazipata baadhi ya timu zilizoundwa chini ya wito au kauli mbiu mbalimbali mfano mzuri ni Liverpool wao wanasema hivi; ‘You Will Never Walk Alone’ kwa kifupi kauli hii ni kuwa wapo pamoja muda wote na wachezaji kamwe hawatatembea pekee yao kwa vile wapo wengine nyuma yao.

Zinaweza kutolewa tafrisi nyingi katika hili na siku zote haya yameonekana pale Anfield na hata nje ya uwanja huo timu ya Liverpool inapocheza na ni namna gani mashabiki wake wanavyoshikamana kuihamasisha timu yao hata kama itakuwa imefungwa mechi hiyo.

Miongoni mwa mambo ambayo siku zote yanayokumbukwa na wachezaji wa timu hiyo pindi wanapohama ni sapoti kubwa toka kwa mashabiki na viongozi wakati wakichezea timu hiyo, ndiyo tafsiri halisi ya you will never walk alone.

Hapa Tanzania sidhani kama mashabiki na viongozi hata wachezaji walikuwa kweli wanaitafsiri vilivyo kauli mbiu ya Yanga imara daima mbele nyuma mwiko.

 

MECHI YA MEDEAMA

Katika mechi ya nyumbani kati ya Yanga na Medeama ya Ghana mtu anaweza kujiuliza hivi ni kweli kauli mbiu ya Yanga ilikumbukwa?

Kama ni kweli waliizingatia katika hali ile ambayo timu ilikuwa inahitaji ushindi kwa hali yoyote inapotokea bao lile la Yanga limepatikana mapema na kutafsiri daima mbele hakukuwa na sababu yoyote inayoweza kukubalika iliyosababisha kukiukwa na kukamilisha neno hili nyuma mwiko.

Wengi waliamini wachezaji na benchi la ufundi wangekumbuka hilo ni wazi wangehamasishana vilivyo kuhakikisha bao lile halirudi na kudhihirisha kauli hiyo.

Yanga ya sasa ni timu bora iliyo na udhaifu sugu unaoonyesha kutopatiwa dawa siamini kama makocha hawalioni hili tatizo ambalo wachambuzi wa soka hapa nchini wamekuwa wakilirudia kila mara.

Kikosi cha Yanga kwa sasa inapendeza kweli kuiangalia ambayo katika michezo yake ya kimataifa inaweza kukupa kicheko kwa asilimia 99.9, kisha kukuliza machozi ya damu sekunde ya mwisho ukahisi kujinyonga kama adhabu kubwa.

 

MICHEZO ILIYOSALIA

Yanga wamebakiza mechi tatu, moja ikiwa ya nyumbani dhidi ya MO Bejaia na mbili ugenini dhidi ya Medeama na TP Mazembe. Hapa lazima niwakumbushe nyota wa Yanga kuwa klabu yao ni timu kubwa wasijisikie fahari kupandisha mabega na kujiona wamefika, huku wakicheza na majukwaa kisha kusahau kuwa wanao wajibu mkubwa wa kuandika historia mpya ya timu wanapaswa kujiongeza na kuipigania timu na wakashangilie baada ya ushindi.

Kwa mashabiki na wanachama acheni hizo! Mnawaharibu wachezaji wenu kwa kuwapa sifa zilizopitiliza semeni kweli nyie huyo Donald Ngoma amekuwa Pele, Rivelino au Ronaldo de Lima ambae hamjayaona makosa yake?

Mbona yapo mengi! Ni kweli Ngoma ni mchezaji mzuri lakini anayo makosa mengi kwa sasa hivyo tungetegemea ahamasishwe ili ajitume zaidi na kuisaidia timu.

Hivi sasa Yanga tayari imecheza mechi zaidi ya kumi za kimataifa hebu kiangalieni kiwango cha hawa kina Ngoma na Amissi Tambwe wamefunga mabao magapi ili mpate kufahamu kuwa wamelinda, wamepandisha au wameshuka kiwango.

Tayari katika dakika 270 Yanga imeambulia bao moja na pointi moja tu, ikiwa imepoteza pointi nane na kufungwa mabao matatu katika mechi zao tatu zilizopita za Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A.

 

USHABIKI KANDO

Soka halihitaji ushabiki usiokuwa na tija mchezaji wa kulipwa anatakiwa kufanya kazi yake kwa umakini siku zote na aonyeshe tofauti iliyowazi kati yake na wazawa. Kwa mchezaji wa kulipwa kutoka nje katika mechi kumi za kimataifa anapaswa awe na mabao angalau yasiopungua manne.

Hata Msimbazi napo, hata wao inaonesha bado wameshindwa kutafsiri kauli mbiu yao ya Nguvu Moja.

Hivyo Wanamsimbazi a.k.a. Mnyama ni kweli wengi wenu mnaelewa maana ya kauli mbiu hiyo? Na kama mnaelewa kweli kwa nini hamzingatii na kuendelea kukumbatia migogoro inayokizana na kauli mbiu yenu ya Nguvu Moja?

Wazee na waasisi wa klabu hiyo walikuwa na maana kubwa kwa kauli hiyo mnaweza kuwa mnawasononesha sana pale inapokiukwa kauli hiyo, kukosekana kwa nguvu moja matokeo yake huzalisha utengano ambao labda ndio umechangia kuifanya klabu yao kuusotea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne sasa.