Jamaa mapema wamesomeka

Yahya Mohammed

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuletea wachezaji waliosajiliwa katika dirisha hilo na jinsi walivyoanza kusomeka na kama watavutiwa pumzi zaidi, huenda wakatisha kwelikweli na kuzinufaisha klabu zao.

DIRISHA dogo la usajili lilifungwa wiki tatu zilizopita na ilishuhudiwa klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara zikinyakua nyota kadhaa vikosini  mwao.

Azam, Simba na Yanga ziliongoza kwenye dirisha hilo sambamba na Mbeya City, Majimaji na Mbao katika kuimarisha vikosi vyao.

Baadhi ya nyota waliosajili ndani ya klabu hizo kupitia dirisha dogo wameanza makeke yao, wapo walioanza kwa kasi kwenye Ligi Kuu Bara na wengine waliopo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar hawakamatiki kabisa.

Mwanaspoti linakuletea wachezaji waliosajiliwa katika dirisha hilo na jinsi walivyoanza kusomeka na kama watavutiwa pumzi zaidi, huenda wakatisha kwelikweli na kuzinufaisha klabu zao.

Pastory Athanas- Simba

Straika huyu alitua Msimbazi akitokea Chama la Wana, Stand United ya mjini Shinyanga. Tangu amefika katika kikosi hicho ameonekana kufiti katika mifumo ya Kocha Joseph Omog kwani, amekuwa akimuanzisha kuanzia mechi za Ligi Kuu Bara mpaka Kombe la  Mapinduzi. Ameonyesha kuwa na kasi na nguvu za kupenya safu ya ulinzi ya timu pinzani.

Hajafunga bao mpaka jana jioni, lakini Pastory ameonyesha anavyoisaidia Simba kutokana na aina yake ya uchezaji na iwapo ataendelea kuaminiwa atakuwa msaada mkubwa kwa Wekundu wa Msimbazi kwa vile soka analijua.

Emmanuel Martin- Yanga

Winga huyu amekuja na kujichukulia namba yake moja kwa moja akimzidi ujanja Deus Kaseke.

Alisajiliwa saa chache kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo akitokea JKU ya Zanzibar, hasa baada ya kuitungua Yanga mabao mawili safi kwenye mchezo wa kirafiki na uliokuwa wa kwanza kwa Kocha wa Yanga, Mzambia George Lwandamina.

Ni ngumu kuja kwenye klabu kubwa kama Yanga na kupata namba mara moja, lakini uwezo wake kisoka na hasa chenga zake, kasi na umakini wake uwanjani umembeba kiulaini Jangwani.

Bado mashabiki wanapaswa kuendelea kumvutia pumzi kutokana na kasi yake aliyoanza nayo na anayoiendeleza akiwa kwenye michuano ya Mapinduzi.

Zahoro Pazi- Mbeya City

Winga mwingine aliyeanza na mguu mzuri katika klabu yake. Pazi alikuwa ana miaka miwili na ushei hajaicheza Ligi Kuu Bara kutokana na tatizo la ITC yake kushikiliwa na klabu ya FC Lupopo ya DR Congo. Lakini baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuingilia katia ameanza makali yake akipiga mpira mwingi katika mechi yake ya kwanza na City.

Siyo kupiga mpira mwingi tu, bali aliifungia bao katikan ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbao na kama ataendelea na kasi hiyo atatisha zaidi pale Mbeya City.

Juma Liuzio- Simba

Wakati taarifa za kurudi kwake nchini, wengi walianza kumbeza na kuamini kuwa, ameshafulia. Liuzio au maarufu kama Ndanda alikuwa akicheza soka la kulipwa Zesco ya Zambia na ametua Msimbazi kwa mkopo bila kutarajiwa.

Katika ligi amefanikiwa kucheza mechi moja tu, lakini katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ameonyesha utofauti katika safu hiyo ya ushambuliaji.

Amejipambanua tofauti yake na Laudit Mavugo na hata Frederick Blagnon, kwani amekuwa msumbufu kwa mabeki pinzani akipiga mashuti na hata spidi yake na tayari ameshafunga bao moja Kombe la Mapinduzi.

Bado kuna muda wa kuvutiwa pumzi katika Ligi Kuu kwa sababu, ligi inaingia mkono wa lala salama ambapo ushindi huwa ni mkubwa zaidi na kama akiwa makini ndipo, ataudhibitishia umma kuwa Simba haikukosea kumsajili toka Zesco.

Yahya Mohammed- Azam

Wazee wa kutunga majina wanamuita Awilo Longomba, hii ni kutokana na mwonekano wake hasa rasta alizonazo kichwani. Lakini pamoja na bezo hizo jamaa huyo ni mkali uwanjani.

Yanga huenda wanamwota kwani ni kati ya wauaji wanne walioizamisha juzi Uwanja wa Amaan katika Kombe la Mapinduzi.

Katika Ligi Kuu keshafunga bao moja pia dhidi ya Majimaji, kwa jinsi alivyo machachari uwanjani ni wazi Azam imevuta kifaa na inasubiri kuanza kufaidika naye kwani, soka analijua na anajua kilichomleta nchini toka kwao Ghana.

Joseph Mahundi- Azam

Mwanzo wake haukuwa mzuri ndani ya Azam, alionekana hafiti katika mifumo ya timu hiyo, lakini aliyekuwa Kocha wa timu hiyo, Zeben Hernandez hakuchoka kumpanga na sasa moto wake umeanza kuonekana na kuchoma wapinzani.

Umewachoma Yanga katika Mapinduzi kwa kufunga bao la tatu kwa shuti la Dar Mpaka Moro, lililomfanya kipa Deo Munishi ‘Dida’ kuonekana si lolote.

Kama ataendelea kuaminiwa na yeye kujiamini uwanjani, Mahundi aliyekuwa Mbeya City akitokea Coastal Union atatisha zaidi kwani, kipaji kipo na soka pia analo mguuni.

Enock Agyei-Atta- Azam

Ni kijana mdogo, ndio kwanza ametimiza miaka 18 wiki iliyopita, lakini tayari ameanza makali yake kwa kishindo.

Agyei ameshafungua akaunti yake ya mabao kwa kuitungua Yanga bao la nne katika Kombe la Mapinduzi, tena akitokea benchi.

Makali ya Agyei, Yanga wanayajua sio kwenye michuano ya Mapinduzi ila hata kwenye Kombe la Shirikisho la Afrika alipokuwa akiichezea Medeama ya Ghana ambayo iliichachafya Vijana wa Jangwani nyumbani na ugenini.

Kwa umri alionao ni wazi Agyei atasumbua sana akiwa na kikosi cha Azam iwe kwa mechi za Ligi Kuu Bara ama Kombe la Shirikisho Afrika. Tusubiri.

Tito Okello- Mbeya City

Mganda huyu alisajiliwa na Wagonga Nyundo wa Jiji la Mbeya akitokea African Lyon alikotibuana na mabosi wake.

Alitua City na waganda wenzake, Hood Mayanja na William Otong, lakini ni yeye aliyeanza makeke mapema.

Achana na usumbufu wake kwa mabeki, lakini Okello pia ni mfungaji mabao na atayari ana bao moja na timu yake hiyo na City na kumfanya efikishe bao la nne katika Ligi Kuu msimu huu.

 Akipewa muda zaidi atatisha kama njaa.