Huyu mtu Logarusic achana naye kabisa

Zdravko Logarusic

Muktasari:

Alipokuwa Msimbazi wachezaji waliomba po! Kwani hakuwa akitaka utani hata kidogo na wakati mwingine wakimzingua alikuwa akiwapa maneno ya shombo.

UNAMKUMBUKA yule mtata wa Simba, Zdravko Logarusic aliyetua Msimbazi kwa mbwebwe Desemba, 2013? Jamaa kwa sasa yupo Ghana akiifundisha Asante Kotoko. Ni jamaa fulani kauzu hivi, asiyependa mzaha kazini. Alipokuwa Msimbazi wachezaji waliomba po! Kwani hakuwa akitaka utani hata kidogo na wakati mwingine wakimzingua alikuwa akiwapa maneno ya shombo. Mabosi wa Simba wanashindwa kumvumilia kwa sababu walimuona kama mtu fulani asiyeeleweka jamaa akasepa zake kurejea Kenya walikomtoa.

Logarusic aliyekuwa akifahamika zaidi kama Loga, amerejea Ghana alikoanzia kufundisha. Amejiunga na vigogo wa Ligi Kuu ya huko, Asante Kotoko kwa mkataba wa miaka miwili. Mkataba huo aliuingia mwezi uliopita, lakini ukweli ni kwamba kocha huyo amefanya kazi katika mataifa manne tangu mwaka 2009. Mataifa hayo ni Ghana, Kenya, Tanzania na Angola.

Mwanaspoti linakuletea safari nzima ya kocha huyo katika soka lake barani Afrika.

 

Ghana: King Faisal, AsHanti Gold; 2009 - 2011

Logarusic (55) alitua Afrika kwa mara ya kwanza Julai Mosi, 2009 ili kuinoa King Faisal ya Ligi Kuu ya Ghana. Baada ya kufanya vyema katika timu hiyo ndani ya mwaka mmoja, Loga aliteuliwa kocha wa Ashanti Gold Julai Mosi, 2010 hadi Desemba 15, 2011.

 

Kenya: Gor Mahia; 2012 – Juni 2013

Baada ya kuzoea mazingira ya soka ya Ghana, kocha huyo alibadilisha upepo na kuhamia Kenya.

Machi 30, 2012, Logarusic alitangazwa kuwa, kocha wa mabingwa mara 15 Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia. Ndani ya Kogalo, alisisimua matokeo ya timu hiyo msimu wa 2012 akiwatoa nafasi za kuvuta mkia hadi kumaliza wa pili. Ni mwaka huo Gor ilishinda mataji mawili, ya Nane Bora na la Ngao ya GOtv, Loga akitangazwa kocha bora wa mwaka 2012. Baada ya miezi 15 kazini Juni 2013 jamaa akatoweka kwa kile maafisa wa Kogalo walisema ni utovu wa nidhamu.

“Ulienda kwenu na kukosa kurejea tunachofahamu ni kwamba umeacha kazi kwa hivyo wewe si kocha wetu tena tunakutakia kila la heri,” alisema Katibu mkuu wa Gor kwa wakati huo George Bwana akitangaza kumtema Loga.

 

Tanzania: Simba SC; 2013 – Agosti 2014

Desemba, 2013, Loga alitua Tanzania jijini Dar es Salaam na kusaini mkataba na Simba SC. Ni mwezi huo tu alitangaza kuwachachafya Yanga SC kwa kuwapa kipigo cha mabao 3–1 kwenye fainali ya Nani Mtani Jembe. Baadaye akashinda taji la Kombe la Mapinduzi lakini mambo hayakumwendea vyema kwenye Ligi Kuu Bara kwani Simba ilimaliza nafasi ya nne na kushindwa kukata tiketi ya michuano ya kimataifa. Ni wakati huo jamaa alifurushwa na kurudi zake Croatia. Simba iliachana na kocha huyo Agosti 11, 2014.

 

AFC Leopards: Februari – Oktoba 2015

Baada ya Ingwe kusitisha kandarasi ya Kocha Mholanzi, Hendrik Pietter De Jongh, ilimrejesha Logarusic Kenya ili kuinusuru timu hiyo iliyokua ikisuasua kwenye Ligi Kuu ya KPL. Loga aliiongoza Ingwe kwanzia Februari 2015 hadi Oktoba 2015 alipolia njaa na kurejea kwao Ulaya.

“Hamna mtu anayeshughulikia matakwa yangu, sijalipa kodi mwenye nyumba akidai kunifungia ndani, hivyo nimeamua kurudi Ulaya,” alikaririwa wakati huo kabla ya kupanda ndege kuelekea Croatia. Akiwa Ingwe, kitu muhimu alichokifanya ni kutopoteza dhidi ya wapinzani Gor Mahia tu kwenye debi la Mashemeji.

 

Angola: Novemba 2015 – Oktoba 2016

Safari ya Loga barani Afrika iliendelea baada ya kutua Interclube SC ya Angola Novemba 2015, kabla ya kutua huko, kocha huyo alihusishwa na uhamisho kuelekea Al Hilal ya Sudan. Baadaye alitua Angola kwenye timu hiyo ya maafande wa Jeshi na kuonyesha ubabe wake kuiongoza hadi nafasi ya saba kwa kushinda mechi 11, sare nane na kupoteza mechi 11 tu kati ya 30.

“Nilielewana na mwenyekiti wa klabu nirudi nyumbani kwani nilikumbana na changamoto kibao hapa hususan za matumizi ya lugha. Wao wanazungumza Kireno miye ni Kifaransa na Kiingereza tu,” alikaririwa kipindi hicho.

 

Asante Kotoko – Jan 9 2017

Kwa namna kocha huyo alivyo na wasifu nzuri katika soka la Afrika huwa, halali njaa kwani baada ya kuondoka Angola mapema Januari mwaka huu, jamaa alikula shavu fasta aliposaini mkataba wa kuinoa klabu ya Asante Kotoko ya Ghana.

Loga alitia wino mkataba wa miaka miwili akianza kazi kwa kishindo Jumapili iliyopita wakati vijana wake walipowacharaza Liberty Professionals mabao 2–1 ikiwa ni mechi ya kwanza Ligi Kuu msimu huu.

“Ligi ni ngumu huku, lakini vivyo hivyo tutapambana tu. Kotoko ni timu kubwa yenye zaidi ya mashabiki milioni nane ni lazima wajivunie kuwa nami kwa kuwapa mataji,” Loga aliliambia Mwanaspoti huku akimsifia mwenyekiti wa klabu hiyo, Opoku Nti aliyemkabidhi gari la kifahari pamoja na nyumba.

“Mwenyekiti Opoku amekuwa na mchango wa kupigia mfano tangu nije hapa. Si gari tu, nyumba yangu nitakayoishi inakarabatiwa na majuma mawili yajayo nitahamia kutoka hotelini ninayokaa hivi sasa.”

Mbali na Logarusic kwenye ligi hiyo ya Ghana pia yupo kocha wa zamani wa Gor Mahia, Frank Nuttall ambaye juzi aliteuliwa kuwanoa mahasimu wa Kotoko, Accra Hearts of Oak, ikielezwa kuwa ulikuwa mchongo wa Loga.

“Kweli, Mwenyekiti wa Hearts of Oak ni rafiki yangu na pindi tu niliposikia wanasaka kocha mwingine nilimpigia simu na kumpendekeeza rafiki yangu Nuttall ambaye tulichuana akiwa Gor nami Ingwe mwaka juzi.

“Niliweza kumtembelea Nuttall juzi na kumkaribisha jijini Accra sasa ni kazi tu.”