Huo mzuka wa Bilionea wa Taifa Jang'ombe si mchezo

Mbunge wa Mpendae, Salim Turuk ‘Mr White’

Muktasari:

  • Napata shauku ya kufahamu sasa namna alivyoingia kuifadhili timu ya Taifa Jang’ombe, namuuliza kwa nini alichagua timu hiyo na siyo nyingine zilizopo visiwani humo.

HAPA visiwani Zanzibar mabilionea Yusuf Manji na Mohammed Dewji ‘MO’ sio habari hata kidogo. Watu wa hapa wanapenda vya kwao na mtu maarufu zaidi katika soka la hapa ni Mbunge wa Mpendae, Salim Turuk ‘Mr White’.

Mwanaspoti halina hiyana kwani limefunga safari hadi ofisini kwa tajiri huyo eneo la Kilimani karibu na Ikulu ya Zanzibar na kufanya mahojiano maalumu na bilionea huyo, ambaye ndiye mfadhili wa timu ya Taifa Jang’ombe.

Baada ya kufika ofisini kwake tu, napata shauku ya kufahamu kwa nini bilionea huyo ambaye, ofisi yake yote imejaa vitu vyeupe, aliamua kuingia katika soka.

“Miaka ya nyuma nilikuwa nacheza soka, nilicheza timu ya Spurs ambayo baadaye ilifahamika kama Shangani tangu ikishiriki Daraja la Tatu hadi Ligi Kuu, nilikuwa pia meneja wa timu kwa wakati huo,” anaanza kwa kueleza Turuk, ambaye ni mmiliki wa hoteli za kifahari za Golden Tulip.

“Niliendelea kuisapoti timu ya Shangani na mwaka 1994/95 ilifanikiwa kuwa Mabingwa wa Zanzibar, mwaka 1995 kulikuwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa visiwani hapa na nikaamua kuingia kwenye siasa,” anaeleza wakati huu akionekana kuwa makini na mahojiano yetu.

Aingia Jang’ombe

Napata shauku ya kufahamu sasa namna alivyoingia kuifadhili timu ya Taifa Jang’ombe, namuuliza kwa nini alichagua timu hiyo na siyo nyingine zilizopo visiwani humo.

“Baada ya kuwa Mbunge wa Mpendae niliendelea kuzipa sapoti timu ambazo ziko jimboni kwangu. Unajua Jimbo la Mpendae halikuwepo hapo awali na kulikuwa na Jimbo la Jang’ombe na ndiyo chimbuko la timu ya Taifa na Jang’ombe Boys.

“Baada ya jimbo kugawanyika, timu ya Taifa ikabaki katika jimbo langu na ndiyo maana nimekuwa nayo karibu sana. Jang’ombe Boys ilikuwa ni timu ya vijana ya Taifa na ikafanya vizuri na kufanikiwa kupanda Ligi Kuu mapema,” anaeleza kwa utulivu tajiri huyo, ambaye kampuni yake inazalisha pia maji ya Zan Acqua.

“Baadaye Taifa wakawa wanataka kupanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza kwenda Ligi Kuu na muda mwingi walikuja kwangu wakiomba niwape sapoti, hapo ndipo nilipoamua kuwa mfadhili wao. Waliomba pia udhamini kwa wakurugenzi wa kampuni zetu na wakapewa.

“Kwenye jimbo langu natoa sapoti kwa timu zote, timu zinazoshiriki Ligi Kuu huwa nazipatia Sh1 milioni pamoja na vifaa. Timu za Ligi Daraja la Kwanza huwa nazipatia Sh700,000 na vifaa na zile za Ligi Daraja la Pili huwa nazipatia Sh400,000 na vifaa,” anaeleza huku akijinasibu kuwa yeye ni mtu wa soka.

Atumia mil 100 Jang’ombe

Namtazama Turuk na kupata shauku ya kufahamu kiasi cha fedha ambacho anakitumia katika klabu ya Taifa Jang’ombe ambayo ina sapoti kubwa ya mashabiki visiwani hapa.

“Kwa sasa tumewapa udhamini wa mwaka mmoja kupitia bidhaa yetu ya V Gas na ndiyo maana umeona tumewapa fulana zenye nembo hiyo,” anaanza kwa kueleza.

“Nimekuwa nikiwapa fedha za usajili ambapo, kwa sasa wamesajili wachezaji wawili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mmoja kutoka Kenya, nadhani wameongeza ushindani katika timu. Natoa pia posho kwa wachezaji na hivi karibuni tutaanza kuwalipa wachezaji mishahara, lengo letu ni kutaka kutwaa ubingwa msimu huu. Kwa jumla hadi msimu unamalizika tutakuwa tumetumia fedha nyingi, tunaweza kutumia hadi Sh100 milioni,” anaeleza kwa msisitizo.

Ashusha kocha wa Fanja

Pamoja na kuwepo kwa makocha Sheha Khamis na Othman Bariki na wengine katika benchi la ufundi, Turuk amemleta visiwani hapa aliyewahi kuwa Kocha wa Fanya FC ya Oman.

“Kama nilivyosema awali tunataka kuweka rekodi ya kuwa timu ya pili kupanda daraja na kutwaa ubingwa, miaka ya zamani iliwahi kufanya hivyo timu ya Small Simba. Malengo yetu haya ndiyo yanatufanya tuboreshe timu zaidi.

“Kocha huyu tuliyemleta ana elimu kubwa ya ukocha na wasifu mkubwa. Amefundisha soka Oman kwa miaka 22, tumempa mkataba wa mwaka mmoja na atawaongezea nguvu makocha waliokuwepo ili tuweze kufanya vizuri zaidi. Siku akiondoka atakuwa amewasaidia zaidi makocha wetu,” anaeleza bosi huyo.

Azungumzia soka la Zanzibar

Mbunge huyo anaeleza kuwa soka la Zanzibar limekuwa na changamoto kubwa kutokana na kukumbwa na ukata hivyo, kushindwa kufurukuta mbele ya klabu zingine za Tanzania Bara ama za Ukanda wa Afrika Mashariki.

“Miaka ya nyuma soka letu lilipiga hatua kutokana na kuwepo kwa wafadhili wengi, miaka ya sasa mambo yamekuwa tofauti. Timu nyingi zimekuwa na uwezo mdogo wa kifedha,” anaeleza.

“Kutokana na ukata hata timu zinazopata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa zimekua zikipata wakati mgumu kufanya hivyo, zimekuwa zikikosa fedha za maandalizi hivyo kutolewa mapema.  Timu nyingi za majeshi KMKM, JKU ziliinuka kwa sababu wachezaji walipata chochote, timu za kiraia zilikuwa na wakati mgumu sana,” anasema. Kwa sasa kunaweza kuwa na mabadiliko kidogo kwa vile kuingia kwangu kumeweza kuwaamsha matajiri wengine, pengine msimu ujao tunaweza kuwa na hali tofauti. Kama mambo yakienda vizuri nataka kuipa sapoti Ligi ya Nane Bora,” anaeleza kigogo huyo ambaye amekuwa hakosekani katika mechi za Kombe la Mapinduzi.

Ukubwa wa Ligi

Ligi ya Zanzibar ina timu 18 kwa hapa Unguja na timu 18 kwa Pemba hivyo kufanya kuwa na timu 36 ambazo ni nyingi kuliko hata ligi kubwa duniani, namuuliza Turuk juu ya hili.

“Tumeshakubaliana kuzipunguza timu kwa msimu ujao, zitapungua timu sita kwa Unguja na timu sita kwa Pemba, angalau tutabaki na timu 24.

Hata wadhamini wakitaka kuingia itakuwa nafuu,” anamalizia kwa kueleza wakati huu tunazungumza mengine machache na kuagana. Siku yangu inakuwa imekwisha hivyo.