Hii ni ishara mbaya kwa kompany

Muktasari:

Bahati mbaya beki huyo wa kati alidumu kwa muda wa dakika 37 tu katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Crystal Palace na kutolewa nje ya uwanja kutokana na kupata majeraha mapya ya maungio ya nyonga baada ya kugongana na kipa wake Claudio Bravo.

WIKI iliyopita katika mechi ya ligi dhidi ya Swansea City, klabu ya Manchester City ilishuhudia kwa mara ya kwanza chini ya Kocha Pep Gurdiola nahodha wake Vincent Kompany akirejea kutoka majeruhi.

Bahati mbaya beki huyo wa kati alidumu kwa muda wa dakika 37 tu katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Crystal Palace na kutolewa nje ya uwanja kutokana na kupata majeraha mapya ya maungio ya nyonga baada ya kugongana na kipa wake Claudio Bravo.

Itakumbukwa Kompany mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa katika mchezo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona uliochezwa mwezi Mei, mwaka huu.

Manchester City itaendelea kukosa huduma ya beki huyu kutokana na kubainika kuwa ana tatizo katika makutano ya nyonga hivyo, atalazimika kukosekana kwa wiki 3-4.

Jeraha alilopata wiki iliyopita dhidi ya Crystal Palace linakuwa ni jeraha la 34 katika miaka minane anayochezea Manchester City huku majeraha 30 pekee ni ya tangu mwaka 2012 mpaka sasa 2016.

Amekuwa akipata majeraha ya misuli ya paja na kigimbi mara kwa mara ambayo ndiyo yalikuwa yanamweka nje muda mrefu katika msimu uliopita.

Kwa beki huyu wa kati mwenye umri wa miaka 30 kupata majeraha haya si ishara nzuri kwani, majeraha ya mara kwa mara yanaweza kuchangia nafasi ya kustaafu soka kabla ya wakati.

Pia kwa timu kama Manchester city inayotumia mamilioni ya fedha kusaka mafanikio, mchezaji huyu anaweza kuwekwa benchi au kuuzwa mapema kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

 

SABABU ZA MAJERAHA

MARA KWA MARA

Nafasi anayochezea Kompany inaweza kuchangia kupata majeraha ya mara kwa mara kwani, ikumbukwe beki wa kati mara nyingi wanakuwa na mzigo mkubwa kukaba na kukimbiza hivyo ni dhahiri anatumia nguvu nyingi huku akigongana na washambuliaji.

Vile vile mchezaji huyu ana kawaida ya kupanda ghafla kushambulia na kuwachezesha wengine kama vile ni kiungo hivyo, kuchangia mara kwa mara kukumbana na faulo nyingi na hivyo kujeruhiwa.

Sababu ya pili ni kutumika sana kwa mchezaji na mwili kutopata mapumziko ya kutosha. Kompany ni mchezaji wa kutegemewa pale Man City na kwenye timu ya taifa ya Ubelgiji hivyo, hujikuta akitumiwa kupita kiasi.

Ikumbukwe pia mchezaji mjeruhiwa baada ya kutoka katika mazoezi tiba anahitajika kupumzika sana ili kutoa nafasi ya mwili kujijenga na kuwa na kinga imara. Upo uwezekano kuwa Kompany hapati muda wa kupumzika.

Kupata majeraha mara kwa mara au kutopona mapema hutegemea pia na aina ya jeraha na mahala lilipo, majeraha katika maeneo ya maungio ikiwamo goti na kifundo na kuchanika misuli ya paja ni majeraha ambayo huwa yanachukua muda kupona.

Majeraha anayopata Kompany mengi huwa ni katika maeneo ya goti kifundo, misuli ya nyuma ya paja na kigimbi hivyo kuwa ni moja ya sababu inayochangia kujirudia kujijeruhi kutokana na kutopana sawa sawa.

Majeraha anayopata mengi yanaangukia daraja la pili na tatu hivyo huwa ni majeraha makubwa ambayo yanalazimu kukaa nje muda mrefu ili kuweza kupona.

Upo uwezekano kuwa majeraha anayopata yanajeruhi pia tishu zingine mwilini ikiwamo mishipa ya fahamu, mifupa pamoja na damu kuvilia ndani ya jeraha hilo nayo pia huweza kuchangia kutopona vizuri majeraha yake na hivyo kujirudia.

Wachezaji wenye umri chini ya miaka 25 wanapona haraka zaidi kuliko wenye umri mkubwa. Kompany ameanza kuandamwa na majeraha zaidi alipotimiza umri wa miaka 26.

Ukitizama katika umri huo kuanzia mwaka 2012-2016 amepata majeraha mara 30, na kwa sasa ana umri wa miaka 30 hivyo ni dhahiri yupo katika hatari ya kupata majeraha mara kwa mara.

Mara nyingine wanasoka hujikuta wakiamua kurudi uwanjani kwa kudanganya au kijikaza kuwa hawana maumivu hivyo kuchangia kujirudia kujijeruhi eneo hilo.

Kuwahi kurudi mchezoni kabla ya muda wa jeraha kupona kabisa nayo inachangia kupata majeraha ya mara kwa mara, majeraha kutopona mapema au kujijeruhi tena.

Kutokana na umuhimu wake Kompany katika timu na kuhitaji kulinda nafasi yake upo uwezekana wa kuwa na kawaida ya kurudi uwanjani kabla ya kuwa fiti asilimia 100.

Pia yapo makosa yanayofanywa na jopo la madaktari au na wataalamu wa mazoezi ikiwamo kukosa uzoefu wa kutibu majeraha ya wanamichezo au kutoa programu dhaifu ya mazoezi tiba.

Kukosa umakini katika upimaji na kushindwa kutathimini ukubwa wa jeraha pamoja na muda wake sahihi wa mchezaji kurudi uwanjani kuendana na aina ya jeraha alilopata.

Kupewa mazoezi tiba au ya viungo ambayo hayaendani na kiungo hicho kilichojeruhiwa.

Kwa kawaida mazoezi tiba ambayo hutolewa katika vituo maalumu ambao kuna wataalamu wa mazoezi ya viungo wenye sifa.

Wanasoka wanaopata majeraha hujikuta wakipewa mazoezi tiba na mtu asiye na uzoefu au ujuzi wa kutosha na mazoezi ya viungo ikiwamo yale ya kuimarisha na kurudishia utendaji wa awali wa viungo.

Asili ya maumbile ya mtu aliyozaliwa nayo ikiwamo utimilifu wa kimwili na uimara wa kinga ya mwili kukabiliana na majeraha yanaweza pia kuchangia mtu kupata majeraha yasiyopona.

Dosari za maumbile ya kimwili inaweza kuwa sababu, mfano mwanasoka anaweza kuwa na dosari ya ukuaji wa mifupa na misuli yake hivyo kutowiana wakati wa ukuaji. Hali hii inaweza kumsababishia kuvutika kwa misuli kupita kiwango chake.

Kutopata matibabu sahihi na kwa mtu sahihi, mjeruhiwa anaweza kutibiwa katika vituo visivyo na wataalamu wenye uzoefu na matibabu ya mejaraha ya michezo.

Huenda jopo la wataalam wa tiba za michezo wa Manchester City hawana uzoefu wa kutosha wa kukabiliana na aina ya majeraha yanayompata Kompany.

Hali hii inaweza pia kuchangia mchezaji mjeruhiwa hufungwa vifaa vya kutuliza mguu usitikisike visivyo na ubora na hivyo kiungo kilichojeruhiwa kutopata utulivu matokeo yake ni kuendelea kujijeruhi.

Kwa kiasi kikubwa hizi ni sababu zinazoweza kuchangia kwa namna moja au nyingine kusababisha mchezaji kupata majeraha ya mara kwa mara.

Kuna ulazima kwa klabu ya Manchester City kuwa makini zaidi kushughulikia majeraha anayopata Kompany kwani kwa sasa si ishara nzuri kupata majeraha ya mara kwa mara.

Kwa sasa Kompany anasubiri ripoti ya uchunguzi wa jeraha alilopata mara ya pili ambayo ilitarajiwa kuwa tayari wakati wowote.

Lengo la uchunguzi huo wa kiafya ni kutathimini majeraha aliyopata na makadirio sahihi ya muda wa kurudi uwanjani.