Hapigi vitu laini bwana, ni mzee wa dona kwa mbele

Muktasari:

Anaishi jijini Dar es Salaam, ni katika kitongoji cha Sinza Darajani. Nyumba anayoishi ipo katika Mtaa wa Kondoa, hapo amepangishiwa na klabu yake inayomlipia kila kitu.

KAMA ilivyo kawaida ya ukurasa huu wa Mpaka Home kukuletea maisha ya wachezaji, safari hii ni zamu ya beki wa kulia wa Simba, Kelvin Faru.

Anaishi jijini Dar es Salaam, ni katika kitongoji cha Sinza Darajani. Nyumba anayoishi ipo katika Mtaa wa Kondoa, hapo amepangishiwa na klabu yake inayomlipia kila kitu.

Mwanaspoti ilitinga nyumbani kwake hapo na kukuta mambo si haba. Simba imemwekea samani chache lakini zile za muhimu; makochi, friji na vinginevyo.

Kinachofurahisha ni namna mchezaji huyo anavyoishi, unajua ikoje? Kijana huyo hukaa jikoni kujiandalia chakula mwenyewe, tena anapika kwa kutumia jiko la mkaa.

 

NYUMBANI

Mwanaspoti: Hodi!

Kelvin: Karibu dada, Ohoo! Mwanaspoti hiyo, karibu sana, pita tu ndani. (Baada ya kukaa) Hapa ndiyo nyumbani, kama unavyoniona naishi msela tu, sina mke wala mtoto.

Mwanaspoti: Ilikuwaje ukaamua kuishi hapa?

Kelvin: Ni mipango tu, klabu yangu ndiyo iliyonitafutia nyumba hii. Hapa nipo na mchezaji mwenzangu, Vincent Costa, yeye ni beki wa kati.

Mwanaspoti: Changamoto gani unazokuta nazo hapa?

Kelvin: Hakuna changamoto kubwa, labda maji kwani kuna nyakati huwa hayatoki, na umeme nao wakati mwingine hukatika. Lakini mambo mengine yote yapo vizuri. Mitaa hii hakuna wizi au fujo, katika usafiri pia pako vizuri, naweza kwenda popote kwa wakati.

Mwanaspoti: Nani anayekufanyia usafi na mpango wa chakula upoje?

Kelvin: Chakula naandaa mwenyewe na usafi nafanya mwenyewe pia. Ninayo ratiba ya siku inayoniongoza kufanya mambo hayo.

Asubuhi nakwenda mazoezini, ninaporudi natengeneza chai ambayo naweza kuinywa kwa maandazi, chapati au mkate, mchana napika ugali na lazima uwe wa dona, mimi bila dona mambo hayaendi.

Ugali huwa naula kwa samaki au nyama ya kuchoma ninayoiandaa mwenyewe pia, mbali ya hivyo huwa napika mboga za majani za asili kama mlenda na mchicha, ratiba ya mlo wa usiku huwa ni wali na mboga mbaga, maharagwe na nyama.

 

MAHABA

Mwanaspoti: Umeniambia hujaoa, vipi kuhusu mchumba, unaye?

Kelvin: Mchumba ninaye. Ninampenda sana na malengo yetu ni kufunga ndoa.

Mwanaspoti: Tutajie jina la mchumba wako, pia mna muda gani katika uhusiano wenu huo? Pia, ni kitu gani kilichokuvutia kwake hadi ukampenda?

Kelvin: Mh! (anaguna) Kutaja jina lake hapana, nahofia kumtaja kwa sababu haijawa rasmi, si unajua mambo ya wazazi! Lakini kwa kifupi anaishi kwao na anafanya kazi ya kuuza duka Tandika.

Nipo naye kwa takribani nusu mwaka sasa. Kilichonivutia kwake ni nidhamu. Ni binti mwenye maadili. Ananielewa ninapokuwa na shida au naumwa, ananijali siyo mtu anayenipenda kwa sababu ya kitu namfurahia kwa kweli.

Pia, macho yake (anatabasamu), ninapoyatazama huwa yananivutia sana, yaani huwa sichoki kumtazama. Natamani niwe namtazama siku nzima.

Mwanaspoti: Sasa lini mtafunga ndoa?

Kelvin: Mpango upo, lakini kulingana na hali ya maisha kwa sasa bado kwanza, nataka nifanye maamuzi hayo wakati nikiwa tayari nina maisha mazuri katika kazi yangu, pia niwe na nyumba nzuri ya kuishi.

 

MAISHA YA SOKA

Kelvin alisajiliwa na Simba kwa ajili ya kikosi cha vijana chini ya miaka 20, ametokea Prisons ambayo ilimnyanyua kutoka Wenda ya jijini Mbeya.

Kutokana na kufanya kwake vizuri, Simba imekuwa ikimjumuisha timu ya wakubwa katika baadhi ya mechi na anasema malengo yake ni kuwa mchezaji mahiri Tanzania na duniani kwa jumla.

“Safari hii ya mpira naamini itakuwa salama, nitapambana kwa nguvu zote kuhakikisha nacheza kikosi cha kwanza, hatua niliyoanza nayo namshukuru Mungu na sasa kazi yangu ni kumshawishi kocha ili anipe nafasi,” alisema.