Hapana! Kiganja aiangalie upya kalenda

Muktasari:

Waliocheza soka katika karne ya 19 na 20 bila ya shaka wanajitofautisha mno na wanaocheza katika zama hizi za karne ya 21, kuanzia mbinu, ufundi na hata malipo wanayolipwa. Leo Cristiano Ronaldo na Messi wanalipwa fedha kiasi cha kutisha sana.

DUNIA iliingia karne ya 21 kama miaka 15 iliyopita, ikiwa imejaa mabadiliko makubwa kuanzia ya kimaendeleo, kijamii, kiuchumi na hata kwenye michezo.

Waliocheza soka katika karne ya 19 na 20 bila ya shaka wanajitofautisha mno na wanaocheza katika zama hizi za karne ya 21, kuanzia mbinu, ufundi na hata malipo wanayolipwa. Leo Cristiano Ronaldo na Messi wanalipwa fedha kiasi cha kutisha sana.

Paul Pogba amenunuliwa kwa rekodi ya dunia ya Pauni 100 milioni, je ni mchezaji gani wa karne zilizopita aliyeweza kununuliwa kwa kiasi hicho na kulipwa mshahara mnono kama Mfaransa huyo na wengine waliopo sasa?

Hata hivyo, wakati mataifa mengine yakienda na kasi ya mabadiliko ya dunia, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) bado linataka kuuaminisha umma kuwa Tanzania bado inaishi karne ya 15.

 

KI VIPI?

Klabu za Simba na Yanga zote za Dar es Salaam zina miaka 80 tangu kuasisiwa kwake na kuendeshwa na wanachama, lakini hazijapata mafanikio ya maana katika michuano ya kimataifa.

Kwa miaka yote hiyo zimekuwa zikishiriki miachuano mbalimbali ya kimataifa, na kuwa kama wasindikizaji kwa wenzao Afrika. Mbali na kutamba Afrika Mashariki na Kati kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame mara kadhaa haijawahi kutwaa taji lolote Afrika.

Rekodi za kujivunia ni kufikia hatua fulani katika michuano ya klabu Afrika, lakini hata mara moja hazijaleta taji katika ardhi ya Tanzania, kadhalika ni klabu zilizodumaa kimaendeleo tofauti na umri mkubwa ilizonazo.

Mwaka 1993 Simba ilileta Kombe la CAF, Dar es Salaam ilipotinga fainali za michuano hiyo, lakini Watanzania waliishia kulitazama kwa macho tu uwanjani kwani, lilibebwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast baada ya kufungwa 2-0.

Rekodi nyingine ni za kutambiana wenyewe kwa wenyewe, lakini hazina tija yoyote kwa soka la Tanzania, kwani kila zinapotoka kuiwakilisha nchi zimekuwa kama kichwa cha mwendawazimu, zikinyolewa na kurudi nyumbani.

Ukitoa takwimu hizo hakuna kitu cha maana ambacho Simba na Yanga chini ya wanachama wanajivunia, huku zikiendeshwa kwa misaada ya wanachama na wahisani badala ya kujiendesha zenyewe na kumiliki uchumi.

Wanachama wa klabu hizo baada ya kuwa gizani kwa muda mrefu wamepata mwanga na wamegundua katika maisha ya sasa ni lazima wafanye mabadiliko ili kuleta maendeleo ya klabu zao.

 

SERIKALI YAZIGOMEA

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohammed Kiganja kwa mara nyingine amedai timu hizi haziwezi kuondolewa mikononi mwa wanachama kwa madai kunaweza kuhatarisha amani bila kufafanuza zaidi.

Madai haya ni wazi ni msimamo wa serikali na yamekuja baada ya wanachama wa Simba na Yanga kutaka mabadiliko katika uendeshaji wa klabu zao. Wanachama wa Yanga kupitia mikutano yao halali wameamua kumkodisha klabu yao, Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kwa miaka 10 na Simba iko kwenye mchakato wa kutaka kumuuzia hisa asilimia 51 mwanachama wao, Mohammed Dewji ‘MO’ kwa Sh20 bilioni.

Hata hivyo, Kiganja katika hali ya kushangaza anadai, suala hilo haliwezekani kwa kuwa ni mali ya wanachama na zina wafuasi wengi hata kama wanachama wenyewe ndio wataamua mabadiliko hayo.

Msimamo wa Kiganja kama ni wake binafsi utakuwa hauna madhara kwani, mabadiliko wanayotaka Simba na Yanga watayafanya bila matatizo lakini kama ni msimamo wa serikali ni jambo ambalo halifai na linazidumaza klabu hizo.

 

WATANI ZAIDI YA VYAMA VYA SIASA?

Moja ya madai ya Kiganja ni kwamba, Simba na Yanga haziwezi kutoka mikononi mwa wanachama kwa vile zilisaidia mapambano ya kudai Uhuru wa Tanganyika.

Kwa sababu hiyo Kiganja anataka mtu anayetaka kumiliki timu hizo ni bora tu, akaanzishe yake kama alivyofanya bilionea Said Salim Bakhressa aliyeanzisha ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Inawezekana maelezo ya Kiganja kuwa Yanga na Simba zilichangia kuleta Uhuru wa Tanganyika ni sawa, lakini swali la kujiuliza je klabu hizo zilikuwa na mchango mkubwa kiasi gani kuliko vyama vya siasa vilivyopigana uhuru huo?

Chama cha Tanganyika African National Union (TANU] kilileta Uhuru Tanganyika na Afro Shiraz Party (ASP) iliyoleta Uhuru wa Zanzibar wanachama wao waliamua kuviunganisha pamoja baada ya kuziunganisha nchi hizo mbili na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1964.

Pamoja na sifa hiyo kubwa ya kuleta uhuru wa nchi hizo, wanachama wa vyama hivyo waliamua kuviunganisha vyama vyao Februari 5, 1977 na kuwa chanzo cha kuzaliwa kwa (CCM).

Ni wazi wanachama wa TANU na ASP wangekuwa na mawazo mgando kama ya Kiganja ni dhahiri kwamba, CCM isingekuwepo kwani nao wangedai vyama hivyo ndivyo vilivyokomboa Tanzania kwa hiyo havistahili kufa kirahisi rahisi tu.

Katika mazingira haya Simba na Yanga wala hazifi bali zinatakiwa kuingia katika uendeshaji bora ili ziwe na mafanikio makubwa zaidi kuliko ilivyo sasa kama zilivyofanya Tanu na Asp ambazo baadhi ya kizazi cha sasa wala hawavijui.

 

WANACHAMA WAMECHOKA UMASKINI

Miaka kadhaa ya nyuma ungeliwa nyama kama ungetoa wazo kwa wanachama la kutaka kuzibinafsisha timu hizi au njia yoyote ile ya kuondoa umiliki wa moja kwa moja wa klabu hizi kwa wanachama.

Hata hivyo, mambo yamebadilika na sasa wanachama wa klabu hizo kupitia mikutano yao wanaamua kuleta mabadiliko ya uendeshaji, sasa inashangaza ni kwa vipi serikali inaweka ugumu katika jambo hilo.

Wanachama wamegundua katika mazingira ya sasa ya uendeshaji wa soka ni vigumu kuendesha klabu kwa mafanikio kupitia michango ya kupitisha kofia kuchangishana.

Miaka ya nyuma kuna tukio ambalo haliwezi kusahaulika wakati aliyekuwa mchezaji kipenzi wa Yanga, Fred Felix ‘Minziro’ alipong’olewa jino, wanachama wakiwa kwenye mkutano wakaamua kuchangia ili apewe msaada wa matibabu ila huwezi amini zilipatikana Sh 6,000 tu licha ya wanachama walioshiriki zoezi hilo kuwa zaidi ya 200.

Kwa hiyo wanachama wa klabu hizi wamegundua ni vigumu kuziendesha kwa mafanikio timu zao katika mtindo wa sasa ndio maana wanataka mabadiliko kwa kuwa, wana kiu ya mafanikio ya kuleta mataji ya Afrika kama walivyo wenzao.

BMT ITATOA RUZUKU

Inashangaza kwa serikali kung’ang’ania Yanga na Simba zibaki kwa wanachama kama vile zina mpango wa kutoa ruzuku katika uendeshwaji wa timu hizo.

Watanzania wa sasa wameamka, wanajua umuhimu wao ni kushabikia timu hizo bila kujali zitaendeshwa vipi iwapo mfumo huu utaziletea mataji klabu hizi.

 

WANACHAMA WAACHIWE WAAMUE

Kwa vile serikali haina uwezo wa kutoa ruzuku kwa Simba na Yanga kwa hiyo hakuna sababu ya kuwazuia wanachama wa klabu hizo kufanya mabadiliko wanayoyataka.

Wanachama wa Simba na Yanga waachwe wafuate taratibu hata kama ni kubadilisha Katiba zao na waruhusu uwekezaji katika klabu ili ziendeshwe bila matatizo ya fedha kama ilivyo sasa. Wakati umefika kwa klabu hizi kupewa ruhusa bila ya kikwazo chochote kile. Kiganja na wenzake watapata manufaa gani iwapo Yanga na Simba hazina mafanikio yoyote ya maana au wakishindwa kusajili wachezaji hodari au wakishindwa kulipa mishahara.

Hoja ya Kiganja kuwa klabu zipo nyingi kwa nini wang’ang’anie Simba na Yanga tu haina msingi kwani, tajiri yeyote yule atataka kuwekeza mahala penye faida na timu yenye mashabiki.

 

Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi ameyewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Bussiness Times (Mhariri Mwanzilishi wa Spoti Starehe) na Mwananchi. Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF). Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020.