Guardiola wa Azam anakosea kidogo tu

Muktasari:

Kwanza kabisa wachezaji wa Azam wanaonekana wako fiti vilivyo, wanamudu kucheza dakika zote 90 kwa kasi ya ajabu. Wana uwezo wa kucheza dakika 120 pia bila kuchoka. Katika eneo hili kocha wa viungo amefanya kazi yake vizuri.

NIMEITAZAMA Azam ya Kocha Zeben Hernandez ‘Guardiola’ kwa makini, kisha nikaitazama tena na kuirudia ili kutaka kufahamu tatizo la msingi uwanjani ni lipi. Kwa bahati nzuri nimetazama mechi zao zote msimu huu. Nimetazama pia na marudio ya picha za video ili kujiridhisha vizuri.

Kwanza kabisa wachezaji wa Azam wanaonekana wako fiti vilivyo, wanamudu kucheza dakika zote 90 kwa kasi ya ajabu. Wana uwezo wa kucheza dakika 120 pia bila kuchoka. Katika eneo hili kocha wa viungo amefanya kazi yake vizuri.

Hata hivyo, mbali na kuwa fiti Azam haijapata matokeo ya ushindi katika mechi tano mfululizo sasa (kabla ya mchezo wa jana Jumatano). Ni matokeo mabaya zaidi kwa timu hiyo tangu msimu wa 2009/10. Matokeo hayo yameifanya Azam sasa kuwa nyuma kwa pointi 11 dhidi ya vinara Simba wenye pointi 23.

Azam ina pointi 12 tu baada ya mechi tisa. Ukiachana na changamoto nyingine za nje ya uwanja, ndani ya uwanja, Azam ina matatizo kadhaa ya kiufundi kama yanavyoainishwa hapa.

 

Himid si beki

Himid Mao kama anavyofahamika. Kila mtu anafahamu ubora wake anapocheza kama kiungo mzuiaji. Kila mtu anafahamu ubora wake wa kuwalinda mabeki na kuwapunguzia hatari.

Hata hivyo, Kocha Zeben amekuwa akimtumia zaidi kama beki wa kati. Amekuwa akimrudisha nyuma karibu katika kila mechi.

Katika uhalisia Himid ni kiungo na anafanya vizuri zaidi akicheza nafasi hiyo kuliko beki wa kati anayocheza kwa sasa.

Mabadiliko haya yameifanya timu hiyo kupoteza mpira na kushambuliwa kwa kasi maana hakuna mtu wa anayeweza kuzuia hatari hizo katika eneo la katikati kama anavyofanya Himid.

Nyota huyo anapaswa kuwalinda mabeki na sio kulindwa na mtu mwingine.

 

Ya Thomas pembeni

Straika Muivory Coast, Gonazo Bi Ya Thomas naye amekumbana na matatizo ya Kocha Zeben, ambaye amekuwa akimpanga kama mshambuliaji wa pembeni badala ya kumweka pale kati. Ya Thomas ni straika hatari na anafanya vizuri zaidi akicheza katikati. Kabla ya kutua Azam, alikuwa mfungaji bora wa klabu ya African Sports ya nchini kwao.

Ukimtazama uwezo wake ni dhahiri kuwa anashindwa kufunga kila wakati kutokana na kuchezeshwa mbali na lango. Katika mchezo dhidi ya Mbeya City ambao alifunga bao, alionekana kuwa hatari kutokana na kucheza katikati jirani kabisa na goli.

 

Kangwa si beki

Kocha Zeben amekuwa akilazimisha kumtumia winga Mzimbabwe, Bruce Kangwa kama beki wa kushoto badala ya mshambuliaji. Kangwa ni kiraka lakini ni tishio zaidi akicheza kama winga nafasi ambayo tangu ametua Azam amechezeshwa mara moja tu, dhidi ya Yanga.

Inashangaza kwa mchezaji kama Kangwa, ambaye wakati anaondoka kwao Zimbabwe alikuwa ametoka kuifungia timu ya Highlanders mabao saba, lakini sasa anachezeshwa kama beki. Ni kweli Kangwa anamudu pia nafasi ya beki ya kushoto, lakini si nafasi ambayo inampa uhuru uwanjani. Yawezekana Kocha Zeben hawafahamu vizuri wachezaji wake na nafasi wanazocheza.

 

Amoah pembeni

Mbali na Azam kutumia fedha nyingi kumsainisha beki wa kati wa Medeama ya Ghana, Daniel Amoah, Kocha Zeben amekuwa akimtumia kama beki wa pembeni.

Kwa waliobahatika kuzitazama mechi za Medeama katika Kombe la Shirikisho Afrika watakuwa wanakumbuka uwezo wa Amoah akicheza kama beki wa kati. Si Aggrey Morris wala David Mwantika anayeweza kumweka benchi.

Hata hivyo, Kocha Zeben amekuwa akimweka benchi na kuwachezesha Morris na Mwantika ama Himid na Mwantika na ikitokea Amoah amepangwa basi anapelekwa kucheza kama beki wa pembeni. Unatumiaje fedha nyingi kusajili beki wa kati halafu unakuja kumchezesha pembeni? Tena wakati huo ukimlazimisha kiungo Himid acheze kama beki?

 

Bocco ana nini?

Miguu imefunga breki. John Bocco kila mtu anafahamu kuwa jua limeanza kuzama. Miguu yake si hatari tena. Katika misimu mitatu iliyopita hakuna msimu aliovuka mabao 10. Sio Bocco wa miaka mitano nyuma. Kwa sasa amecheza mechi sita bila kufunga na wala haishangazi sana, uwezo wake umeanza kugota mahali.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza kocha huyo raia wa Hispania amekuwa akimng’ang’ania Bocco katika kikosi chake cha kwanza karibu kila mchezo. Hii ndiyo sababu amekuwa akimpanga Bi Ya Thomas pembeni ili kumpa Bocco makali eneo la kati, lakini ameshindwa.

Huu sio wakati wa Azam kuendelea kumtegemea Bocco peke yake pale mbele. Straika huyo mkongwe angekuwa tu anasubiri benchi na kupewa dakika chache dimbani. Bocco wa sasa ni kama tu Wayne Rooney wa Manchester United, hivyo hakuna sababu ya kocha kuendelea kumng’ang’ania wakati ana mtu kama Ya Thomas anayeweza kuwa mrithi sahihi wa Kipre Tchetche.

 

Viungo wengi

Kocha wa Azam amekuwa akitumia viungo watatu katika kila mchezo. Amekuwa akiwatumia Jean Mugiraneza, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya ama Kipre Bolou kwa pamoja wakati huo huo akimtumia Himid Mao kama beki.

Hii inamaanisha kuwa Azam inataka kuwa na umiliki mkubwa wa mpira katika kila mchezo. Hii ndiyo sababu amekuwa akimweka Mcha Khamis benchi. Inashangaza sana.

Azam inapocheza nyumbani dhidi ya African Lyon ama Ruvu Shooting ina ulazima gani wa kutumia viungo wengi? Hapana. Inatakiwa kuwa timu ya kushambulia zaidi. Inatakiwa kuwa timu yenye watu wenye uwezo mkubwa wa kushambulia kama Mcha na sio kujaza viungo wengi. Itazame Simba jinsi imekuwa ikicheza soka la kuvutia ikiwa na viungo wawili tu uwanjani. Jonas Mkude na Mzamiru Yassin wamekuwa wanatosha.

Katika baadhi ya mechi ngumu kocha amekuwa akimtumia Mwinyi Kazimoto kama kiungo wa tatu. Kwa Azam kila mechi wamekuwa wakijaza viungo. Hii imesababisha timu yao icheze mpira mwingi ila haishindi.