Figisu na Siku 90 za Stand United

Muktasari:

  • Stand ilikuwa kwenye wakati mgumu kiuchumi wakati inapanda Ligi Kuu kabla ya kupata udhamini ambapo wakati huo ikija kucheza mechi za jijini Dar es Salaam ilikuwa ikipiga kambi yake Tandika na kufanya mazoezi viwanja vya huko huko Tandika ambako wakitimuliwa vumbi basi mafua yalikuwa yakihusika.

MGOGORO wa kimasilahi uliopo ndani ya Stand United ndio gumzo la sasa kwenye Ligi Kuu ya Soka Tanzania hususan kwa mashabiki wa Kanda ya Ziwa. Ni mgogoro wa kiutawala wa kugombania umiliki wa timu ambao unatishia kuipeleka pabaya timu hiyo ya Shinyanga.

Stand ilikuwa kwenye wakati mgumu kiuchumi wakati inapanda Ligi Kuu kabla ya kupata udhamini ambapo wakati huo ikija kucheza mechi za jijini Dar es Salaam ilikuwa ikipiga kambi yake Tandika na kufanya mazoezi viwanja vya huko huko Tandika ambako wakitimuliwa vumbi basi mafua yalikuwa yakihusika.

Tandika ni wapi?

Ni eneo dogo la Wilaya ya Temeke ambalo lina makazi yenye msongamano,limebeba sehemu kubwa ya wafanyabiashara ndogondogo na makazi mengi bei zake zimepoa tofauti na sehemu zilizopo karibu na katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwenye nyumba za kulala wageni kuna vyumba mpaka vya Sh 5000. Idadi ya watu kwenye eneo hilo inakadiriwa kuzidi 10 0,000.

Msimu uliopita, Stand ilipata udhamini mnono wa Sh 2.4 bilioni kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Acacia, maisha ya timu hiyo yalibadilika ghafla, wachezaji walilipwa mishahara yao kwa wakati, wanaishi sehemu nzuri, wanakula vizuri ikiwa ni pamoja na kusafiri kwa raha pale wanapokwenda kucheza mechi za ligi nje ya mji wa Shinyanga.

Hivi sasa ndani ya Stand United maisha yalianza kubadilika mara baada ya udhamini huo kuanza kufanyakazi, mgogoro ulianza kujitokeza kwa viongozi wa klabu hiyo kikubwa ikiwa ni kudai kwamba baadhi ya viongozi wanajinufaisha wenyewe.

Hivi karibuni, Acacia ilitoa angalizo kwa Stand United la miezi mitatu kwamba wakishindwa kumaliza migogoro yao basi ni wazi watavunja mkataba wao ambao umebaki mwaka mmoja sasa. Nini kinaweza kusaidia mgogoro huo unaoitafuna Stand huku baadhi wakidai kunyang’anywa timu yao, basi kunusuru hali hiyo kutotokea basi yanaweza kufanya haya ambayo ni baadhi tu.

Jonas Tiboroha

Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Jonas Tiboroha ndiye aliyechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Stand United wakati ikiwa kwenye mchakato wa kubadilishwa kutoka klabu kwenda kampuni. Mabadiliko hayo yalifanywa na baadhi ya wanachama ambao inaelezwa kuwa ni waanzilishi wa Stand United.

Yawezekana kabisa wazo la kumteua Tiboroha lilikuwa ni jema lakini inawezekana pia lilikuja kipindi ambacho hakikuwa kizuri kwao kutokana na mgogoro uliokuwa tayari umeanza. Kwa vile Tiboroha si mwanzilishi wa timu hiyo anapaswa sasa kukaa na kuwashauri wenzake ili waungane wawe kitu kimoja kuiokoa Stand United ili hata kama wataamua kubadilisha mfumo iwe ni maridhiano ya pamoja ambayo hata yeye pengine hawezi kuchafua sifa yake ya usomi.

Mbasha Matutu

Mbasha ni mratibu na mjumbe wa Kamati ya Usajili na pia ni mjumbe kwenye Chama cha soka Mkoa wa Shinyanga inadaiwa kuwa naye si mwanzilishi wa Stand United na kwamba pia ni mmoja wa wadau wanaochangia kuwepo kwa mgogoro ndani ya klabu hiyo ingawa habari pia zinadai kuwa ni miongoni mwa wale waliochangia kusajili Katiba ya Stand United.

Yawezekana Mbasha ni kiongozi bora ama sio kiongozi bora, ila kwa kipindi kama hiki pia alistahili kukaa pembeni ili kutojihusisha na tuhuma zinazoelekezwa kwake, angewaacha viongozi wa Stand kama Stand wafanye wanayoyahitaji yeye awepo tu kama kutoa ushauri kama kutakuwepo na hitaji hilo. Mambo yakitulia, basi wagawane vyeo kwa usawa.

Amani Vincent

Huyu alikuwa ni Mwenyekiti wa Stand United na ni kiongozi wa tatu tangu timu hiyo ianzishwe ambapo timu hiyo ilianza kupiga soka kwenye michuano ya Polisi Jamii iliyoanzishwa kwa lengo la kupunguza vibaka hasa wakilengwa wapiga debe wa Stand ya Shinyanga ambako kulikuwa na uhalifu mkubwa.

Kabla ya kuanzisha wazo la kufanya mabadiliko kutoka klabu kwenda kampuni, tayari Vincent alikuwa na mgogoro na baadhi ya viongozi huku pia kutokuwa na mawasiliano mazuri na Kocha Patrick Liewig.

Wazo la Vincent pengine lilikuwa zuri ila lilipokelewa tofauti kwasababu wengi hawakuelewa kwani hivi sasa klabu nyingi zinatoka kwenye mfumo wa wanachama na kujiendesha kikampuni, huenda pia Vincent alilitoa wazo hilo wakati tayari suala la kufanyika kwa uchaguzi mkuu likiwepo, hivyo anadaiwa alikuwa anakwepa uchaguzi huo .

Vincent ni mmoja wa watu ambao wanapaswa sasa kukaa chini na kulimaliza tatizo hilo na wenzake ili Kampuni ya Acacia isijiondoe, kwani kujiondoa kwa Acacia kutapelekea timu hiyo kuyumba kwani itakuwa haijajiandaa kupata mdhamini mpya.

Wananchi wa Shinyanga watapata pigo kubwa na kupata mdhamini, si jambo jepesi kama wengine wanavyofikiria. Amani ni mtu muhimu sana na anahusika katika kumaliza mgogoro huo.

TFF

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), wao wana nguvu ya kumaliza tatizo lililopo ndani ya Stand United pasipo kuwepo na upendeleo. Stand United imeshikiria maisha ya watu wengi, endapo Acacia itajiondoa kwa kushindwa kumaliza mgogoro uliopo ni wazi utawaathiri kwa kiasi kikubwa wachezaji ambao wengi wao wanaendesha maisha kupitia mpira.

Kuwepo kwa Acacia ndani ya Stand United si kwa kuwasaidia wachezaji na viongozi wa klabu hiyo, bali hata kuinua uchumi wa mji huo ambao wadhamini hao unawazunguka kutoka na migodi ya madini waliyowekeza huko. TFF inapaswa kuona kwa kina nini kimesababisha kuwepo kwa tatizo hilo na kulitatua ili kunusuru udhamini huo. TFF ndiyo yenye mamlaka ya soka hapa nchini ni wazi na ni kazi yao kuona na kutatua tatizo husika kwenye klabu yoyote.

TFF haipaswi kufumbia macho mambo ambayo yanaonekana na wananchi wanayaona, endapo TFF itashindwa kumaliza hili ingawa ilishatamka kuwa mwenye mamlaka na anayetambulika ni klabu na viongozi waliochaguliwa lakini mambo yanayoendelea Shinyanga si ya kisoka bali ni kuharibu mpira.

TFF ilibariki kuitambua klabu na sio kampuni iliyokuwa inaongozwa na Amani pamoja na Tiboroha kama Mkurugenzi, lakini bado wana kazi ya kufanya kuokoa udhamini huo usiondoke, ni wazi udhamini wa VPL hautoshekezi, basi waisaidie klabu kuulinda udhamini unaopatikana.

Hapa hata FA ya Shinyanga nayo inapaswa kuingilia kati mgogoro huo kwa kuumaliza kataika njia zilizo sahihi maana timu hiyo ipo chini yao, isionekane kana kwamba na wanaegemea upande mmoja. Kama inatakiwa kubadilishwa mfumo, basi utumike utaratibu ambao kila mmoja ataridhika nao ila kipindi hiki iachwe iliyopitishwa na TFF imalize muda wake.

Serikali

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wanafahamu juu ya mgogoro uliokuwepo kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye mara kadhaa alikuwa akitoa mwongozo kuhusu mgogoro huo lakini mpaka sasa ana nafasi ya kumaliza kabisa ili Acacia iendelee kuwepo ndani ya klabu hiyo.

Nnauye ana nguvu endapo atashirikiana vyema na TFF, viongozi wa klabu pamoja na wale wa kampuni kukaa meza moja na kuyamaliza ili maisha yaendelee kwani hakuna jambo ambalo halina mwisho na hakuna kiongozi ambaye anaongoza sehemu maisha yake yote, uongozi ni kupokezana vijiti, hivyo si jambo jema kuendeleza migogoro inayorudisha nyuma maendeleo ya soka kwa kugombea madaraka.

Nape tayari ametoa lake la moyoni na kuweka wazi juu ya mgogoro huo kwamba anaufahamu hadi kiini chake, hivyo ni rahisi kukaa na kulimaliza hilo. Kiongozi huyo ameagiza pande zote mbili zikae zimalize mgogoro huo ingawa kwa uhalisia inaonekana kushindikana kutokana na kauli zao.

Mahakamani

Hivi sasa suala la kupelekana mahakamani kati ya viongozi wa klabu na wale wa kampuni ni jambo la kawaida. Mara kadhaa viongozi wa Stand Kampuni ndio huwashitaki baadhi ya viongozi wa klabu. Hivi karibuni Mwanaspoti lilikuwa mjini Shinyanga na kushuhudia jinsi viongozi wa pande hizo mbili wakipishana kwenye milango ya mahakama ambapo viongozi wa Stand Kampuni ndio waliowashitaki wenzao.

Viongozi hao wa Stand Kampuni walifungua kesi nyingine mahakamani ya kutotambua uchaguzi uliofanywa ambao ulipitishwa na kuthibittishwa na TFF ingawa viongozi hao ndio wanaotambulika na shirikisho hilo.

Bado mgogoro huo pia unawakwaza wadhamini hao na kuonekana kama ni kuchafuliwa kwa kampuni yao.

Wanachama

Wanachama wa Stand United wana nguvu ya kumaliza mgogoro huo kwani ndio wenye mamlaka ya kuchagua viongozi ama kubadilisha klabu kuwa kampuni, hivyo wana nguvu pia ya kurejesha imani kwa wadhamini wao ili waendelee kuing’arisha Stand yao. Nguvu ya wanachama ni kubwa kuliko nguvu ya kampuni au klabu.

Umoja urudishwe ndani ya Stand United, Acacia pia afikirie jinsi gani wachezaji watakavyoharibikiwa kimaisha ukiachana na viongozi ambao tayari wao wana maisha yao.

Siku zote penye mgogoro wa kiuongozi wanaoumia ni wachezaji.

Hayo tu ni mabadiliko ya kutoka mfumo wa wapiga debe na kuwa mfumo mwingine wa maendeleo kwani wapiga debe pekee hawawezi kuendesha timu hasa kwa hatua iliyofikiwa kwa Stand United ambayo ni hatua ya ushindani zaidi, hivyo hata mfumo wa uongozi pia unaweza kubadilika kulingana na katiba yao inayowataka viongozi kukaa madarakani kwa miaka minne.

Leo hii Stand United inaongozwa na Mwenyekiti, Dr Elson Maeja lakini baada ya miaka minne itakuwa chini ya kiongozi mwingine, maisha yapo hivyo, hakuna sababu ya viongozi hao kulumbana na kuacha Stand iwe katika mfumo wa kizamani na kuna viongozi wa kutumbuliwa, basi majipu hayo yatumbuliwe tu iwe wa klabu ama kampuni.

Dr Maeja naye alikuwa mchangiaji tu kifedha wakati huo hakuna udhamini lakini ni mwanachama wa Stand United.

Acacia imewekwa msimamo wake kwani haitaki ionekana ndio yenye longolongo, iliingia kwa mema kwenye soka kama itachoka, basi iwe kipindi ambacho kazi yake iliyoikusudia iwe imemalizika na isiishie njiani kwasababu ya watu wachache tu.