Edo Kumwembe anaswa kwa unga

Muktasari:

Wakati mwingine mwanadamu anajikuta ghafla yupo katika mazingira mepesi yaliyojaa raha nyingi. Ghafla anakumbana na janga kubwa ambalo hakulitegemea. Inatokea. Ni kweli ilinitokea Aprili 25, 2013 nikiwa mapumzikoni Ulaya.

ILIANZA kama mzaha. Ilianza kama masihara. Sikutegemea. Ilikuwa wakati kipindi cha baridi kikimalizika barani Ulaya kupisha ujio wa majiraa joto, Aprili 2013. Unaweza kudhani ilikuwa hadithi ya kutunga lakini ni kisa kilichonitokea. Kila nikikumbuka huwa natabasamu na kuishia kucheka.

Wakati mwingine mwanadamu anajikuta ghafla yupo katika mazingira mepesi yaliyojaa raha nyingi. Ghafla anakumbana na janga kubwa ambalo hakulitegemea. Inatokea. Ni kweli ilinitokea Aprili 25, 2013 nikiwa mapumzikoni Ulaya.

Nilikuwa katika nchi ya Uswisi ambako nilikwenda kumtembelea rafiki yangu mkubwa, staa wa zamani wa Simba na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Renatus Njohole ambaye anaishi katika Jiji la Yverdon tangu mwaka 1999.

Awali Renatus alikuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu ya Yverdon iliyokuwa Ligi Kuu Uswisi, lakini sasa anacheza daraja la tatu katika soka la ridhaa klabu ya FC Bavois huku akifanya kazi nyingine.

Ni kawaida kwangu kumtembelea Renatus kwa sababu ni rafiki yangu wa karibu tangu tukiwa shuleni Jitegemee pale Kurasini mwishoni mwa miaka ya 1990. Nilisoma naye kidato cha tano na sita. Nyakati hizo alikuwa mwanafunzi, pia akicheza soka kwa ustadi mkubwa.

Mara zote nilizokwenda Ulaya safari huwa inaanzia kwake kwanza. Safari hii haikuwa tofauti na safari nyinginezo, lakini nilikuwa nataka kufika mbali zaidi ya Uswisi. Nilikuwa nataka kwenda Italia kutimiza ndoto ya kufanya mahojiano na mwanasoka wa kimataifa wa Kenya, McDonald Mariga ambaye nyakati hizo alikuwa akikipiga katika klabu ya Parma kwa mkopo akitokea Inter Milan.

Mariga alikuwa ana miaka miwili tangu aweke rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Kenya na Afrika Mashariki kucheza Ligi ya Mabingwa na kutwaa michuano hiyo akiwa na Inter Milan. Kwa nini nisimhoji Mariga? Ningemfuata kokote alipo kwa ajili ya kuandika safari yake ya soka.

Hata hivyo, kabla ya kwenda kwa Mariga ilikuwa lazima safari ianzie kwanza Uswisi kwa kumtembelea Renatus na familia yake. Ingekuwa rahisi kwangu kusafiri kutoka Yverdon Uswisi mpaka Parma kumfuata Mariga kuliko kutoka Dar es Salaam moja kwa moja mpaka Parma. Uswisi na Italia ni nchi ambazo zinapakana katika upande wa Mashariki.

Niliwasili Uswisi, moja ya nchi zenye baridi kali barani Ulaya kwa kutumia shirika la Ndege la Swiss Air na kutumia siku nne kukaa pamoja na familia yake. Renatus ana mke wake wa kizungu, Nadja pamoja na watoto wake watatu wote wa kiume.

Baada ya siku chache za kukaa na Renatus na familia yake iliwadia siku ambayo nilipaswa kwenda Italia kwa ajili ya mahojiano na Mariga.

Kwa mpangilio wa usafiri ulivyokuwa, Renatus alinishauri kwamba ingekuwa rahisi kwangu kupanda treni ya moja kwa moja kutoka katika mji unaoitwa Lausanne nchini Uswisi mpaka mji mkuu wa Italia, Milan kisha nichukue treni nyingine niende Parma kwa ajili ya kukutana na Mariga.

Ilikuwa rahisi tu kwamba Renatus angenipeleka kwa gari kutoka Yverdon mpaka Lausanne kisha ningechukua treni. Asubuhi ya siku ambayo nilipaswa kusafiri nilichukua maamuzi ambayo sikujua kama yangenigharimu sana mbele ya safari na kuzua mkasa huu wa kusisimua.

Kwa kawaida nchini Uswisi vitu vingi vya kawaida vya manunuzi (shopping) huwa vinauzwa bei ghali. Saa ni bei ghali, suti ni bei ghali, viatu ni bei ghali. Karibu kila kitu ambacho ungependa kununua kwa ajili ya kutambia katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam kilikuwa bei ghali.

Tofauti ni kwamba, katika nchi jirani ambayo nilikuwa naelekea (Italia) kila kitu kilikuwa bei rahisi.

Si tu kwamba kila kitu ni bei rahisi, hapana, pia kila kitu ni kizuri na ni bei rahisi. Zaidi ya yote, wanamitindo wengi maarufu wanaotamba Ulaya wanatokea Italia. Gucci, Versace, Giorgio Amani na wengineo.

Kutokana na hali hiyo niliamua kuchukua maamuzi rahisi tu ambayo yalimfanya Renatus atabasamu usiku mmoja kabla sijaondoka, ingawa hakujua kuwa maamuzi hayo yangenigharimu mbele ya safari. Niliamua kuondoka Uswisi nikiwa na Laptop, Kamera, simu ya mkononi pamoja na koti zito ambalo Renatus alikuwa ameniazima kwa ajili ya kukabiliana na baridi njiani hadi Italia.

Kwa nini nibebe begi wakati nilikuwa na pesa za kutosha kununua nguo Milan pindi tu ningefika? Kwa nini nibebe nguo chache za Dar es Salaam mpaka Milan huku nikiwa nimejaza begi wakati nilipaswa kuwa na begi tupu kwa ajili ya kujaza manunuzi yangu ya Italia kuleta Dar es Salaam?

Baada ya Renatus kunifikisha katika kituo cha treni cha Lausanne niliagana naye vyema na kumpa ahadi ya kumpigia simu pindi nikifika salama Milan kisha Parma. Sikuwa na wasiwasi. Haikuwa mara yangu ya kwanza wala ya pili kuitembelea Ulaya. Treni ilikiacha kituo cha Lausanne taratibu.

Unajua ni tatizo gani kubwa lilimtokea njiani? Usikose Mwanaspoti JUMATATU kujua sehemu ya pili ya mkasa huu wa kusisimua katika kisa cha kweli kilichomtokea Mchambuzi wa Mwanaspoti Edo Kumwembe.