Chukua hizo za Thiery Henry

LONDON, ENGLAND. THIERRY Henry unamjua? Sawa, unamjua, lakini kuna mambo yatakufanya umfahamu zaidi.

1. Shujaa wake wa soka

Gwiji huyo wa Arsenal, Henry amefichua kwamba kama kuna mchezaji ambaye alikuwa akimtazama sana na kumhamasisha kucheza soka basi ni Mdachi na gwiji wa AC Milan, Marco van Basten, ambaye anaaminika kuwa ni mmoja kati ya wachezaji bora kabisa katika kizazi chao.

2. Bao analipenda Arsenal

Henry alifunga mabao mengi na ya staili ya tofauti alipokuwa Arsenal. Mfaransa huyo amefunga mabao 228 na ataendelea sana kukumbukwa kama mmoja wa vinara wa mabao katika klabu hiyo yenye miaka zaidi ya 130. Henry amefunga mabao mengi, lakini moja analolipenda ni lile aliloifunga Leeds United katika mechi yake ya kwanza kabisa kuvaa jezi za Arsenal.

3. Mchezaji bora EPL

Hili litawafurahisha sana mashabiki wa Manchester United. Katika mahojiano yake, Henry alifichua kwamba mchezaji bora kabisa aliyewahi kukabiliana naye na kumshuhudia kwenye Ligi Kuu England, basi ni kiungo gwiji wa Old Trafford, Paul Scholes. Henry anasema Scholes hakupewa sifa zake anazostahili, lakini jamaa anajua sana.

4. Usajili wake Arsenal

Stori yake Henry ya kutua Arsenal inafurahisha sana. Uhamisho huo ulifanyika baada ya Henry kukutana na Arsene Wenger kwa bahati mbaya kwenye ndege. Henry anafichua kwamba alikutana na Wenger kwa bahati mbaya kwenye ndege akielekea Paris, Ufaransa na baada ya mazungumzo basi akavutiwa kwenda kujiunga na Arsenal. Agosti 1999 hilo likatimia.

5. Ushirikina

Inaelezwa kwamba kama una kawaida ya kufanya kitu fulani kwanza kabla ya kufanya kingine kwa kujirudia rudia na kufanya kuwa hiyo ni staili ya maisha yako, basi jambo hilo linatafsirika kuwa ni ushirikina. Imani ya kwamba huwezi kukifanya kitu kwa ufasaha zaidi kama ama hujavaa aina fulani ya nguo au viatu.

Henry kwa upande wake alihisi kuwa atakwenda kufanya vizuri ndani ya uwanja kila aliposikiliza muziki ama wa rap au wa zouk kabla ya mechi yoyote ile. Na wanamuzi aliokuwa akiwasikiliza ni Dr Dre, Snoop Dog, Xzibit, Wu-Tang Klan na Tupac.

6. Asili yake

Wengi wanadhani kwamba asili ya Henry ni Afrika kwa sababu tu aliichezea Ufaransa kwenye soka la kimataifa lililojaa wanasoka wengi wenye asili ya Afrika ambapo kuna nchi zilikuwa makoloni ya taifa hilo.

Lakini, hilo si kweli. Henry ana asili ya Visiwa vya Caribbean. Baba yake anatokea Guadeloupe na mama yake Martinique, mbali sana na Ufaransa.

7. Misosi

Henry anapenda sana misosi, hasa kuku, njegere, wali na vyakula vya asili ya kwao Carribean. Alipokuwa New York, Henry alisema kwamba alimisi sana msosi wa kupikiwa na mama yake huko kwao ambao mwenyewe anadhani ni bora zaidi. Misosi mingine anayopenda ni ya Kiitalio, Oriento na Spanishi.