Cheki stori ya mchezaji aliyetoroka Senegal kwenda Ulaya

Coulibaly 

Muktasari:

KUTUA JUVE: Coulibaly ni shabiki mkubwa wa Manchester United, lakini anatarajiwa kuwa staa mkubwa Ulaya baada ya mabingwa wa Italia, Juventus kukaribia kunasa huduma yake baada ya kuvutiwa na kiwango chake.

DAKAR, SENEGAL. MAISHA hayataki mchezo mchezo. Kuwa na maisha bora kunahitaji kuwa na uthubutu. Mamadou Coulibaly anasubiri kuandika historia kubwa kabisa katika maisha yake kutoka kuwa mtoto mkimbizi hadi kujiunga na moja ya klabu maarufu duniani katika mchezo wa soka.

Coulibaly (18) kwa sasa ni kiungo matata kabisa katika kikosi cha Pescara kilichokuwa kikicheza Ligi Kuu Italia msimu huu, kabla ya kushuka daraja kutokana na kuwa mkiani. Lakini, kwa namna alivyotoka kwao Senegal hadi kuingia Ulaya, ndicho kitu kinachotoa tafsiri kwamba maisha yanahitaji kupambana.

Mambo magumu yote aliyokumbana nayo katika safari yake ya kutoka Senegal hadi Ulaya yanakaribia kuleta matunda baada ya kuwa katika hatua za mwisho kabisa kukamilisha usajili wa kujiunga na mabingwa wa Italia, Juventus.

Stori ya maisha ya Coulibaly yanatoa funzo kwamba, hupaswi kukata tamaa bila ya kujali vikwazo gani umekuwa ukikumbana navyo kwenye harakati za jambo lolote unalotaka kulifanya.

Coulibaly, ambaye siku si nyingi atakuwa staa mkubwa duniani, aliingia Ulaya mwaka 2015 baada ya safari ya misukosuko mingi kutoka Senegal, akapitia Morocco kabla ya kufika kwa Wazungu na kisha kipaji chake cha mpira kilionekana na Pescara.

Anasimulia jinsi alivyojivika ujasiri na kuondoka nyumbani kwao bila ya kuaga, akiwa amebeba kibegi chake tu mgongoni na kwenda Ulaya kwa njia za panya. “Niliondoka nyumbani na kibegi changu cha mgongoni.

“Nilimwambia Mamadou tu, huyu ni rafiki yangu na wazazi wangu walidhani nipo shule.

Nilizima simu na sikupiga simu yoyote kwa miezi mitano au minne hivyo, walidhani nimekufa.

“Nyumbani kwetu hakukuwa na shida, tulikuwa na chakula cha kutosha tu kwa sababu watoto tulikuwa mimi na dada zangu wawili. Baba yangu hakutaka kabisa nicheze soka. Kwake yeye shule ndiyo ilikuwa kitu cha muhimu, mimi natokea kwenye familia ya walimu.

“Baba aliniambia atanipeleka kwenye timu za Ulaya, lakini alifanya hivyo kunituliza tu. Nikaamua kuyaweka hatarini maisha yangu kwa ajili ya soka, lakini nimefanya hivyo kwa ajili yao, siku si nyingi nitaanza kuwasaidia,” anasema Coulibaly.

Kwa maneno hayo unaweza kuona kumbe Coulibaly alipata mambo kirahisi rahisi tu, lakini yalikuwa magumu sana. Coulibaly alikuwa akilala mitaani na angepoteza hata maisha baada ya boti aliyokuwa akisafiria kuingia Ulaya kupata matatizo na hakuwa akiweza kuogelea.

“Nililipia tiketi ya basi kutoka Dakar hadi Morocco, hilo halikuwa tatizo, tatizo lilikuja baadaye.

Pale Morocco nilikuwa nalala bandarini, sikuwa na pesa ya kupanda boti.

Kuna mtu alikuwa ananiona kwa siku kadhaa hapo na kuniuliza nataka nini hasa ukizingatia hata kulala nalala mitaani, nilimwambia nataka kwende Ulaya,” anasimulia Coulibaly.

“Baada ya siku chache alirudi, alikuwa akifanya kazi kwenye meli zinazokwenda Ufaransa na akaniambia naweza kwenda.

Nilipanda boti, si kama zile zinazoonekana kwenye televisheni zikibeba wakimbizi, ile ilikuwa kubwa ilikuwa ikisafirisha chakula. Kulikuwa na vijana wengine kama 20 hivi kwenye safari yetu. Nilikuwa nikiwaza mpira tu, wale vijana wengine sikuwa nawafahamu na wala sikuwa nafahamu ndoto zao.

Hivyo ndivyo nilivyofika Ulaya, sina cha kushukuru zaidi ya kufanikiwa kufika Italia kwa boti. Ilikuwa hatari sana, sikuwa naweza kuogelea, hivyo kama boti ingezama, ningeshakuwa nimekufa sasa.”

Baada ya kufika Italia, maisha ya Coulibaly hayakuwa mepesi pia. Alijikuta kwenye matatizo makubwa ya kubaguliwa kutokana na rangi yake na kitu kizuri ni kwamba, alikuwa akipata chakula.

“Kuna wakati watu wa Italia walikuwa wanaiita mimi mtu wa kwenye boti kunikashifu tu, sikuwa na namna. Nyakati ngumu zaidi zilikuwa kipindi kile nilichokuwa Livorno. Kuna mtu alipeleka huko kunitambulisha kwa baadhi ya timu, lakini asubuhi moja naamka hotelini, sikumwona tena. Sikuwa na pesa, sikuwa namfahamu yeyote na nilikuwa siwezi kuzungumza Kiitaliano pia. Mtu huyo aliniona tu nikicheza mpira ufukweni na kuniambia ananipeleka Livorno kufanya majaribio, kitu ambacho nilikitaka sana, lakini shida sikuwa na maelezo ya kutosha.

Nilikuwa nikilala mitaani na ilikuwa bahati sana kupata chakula,” anaweka wazi Coulibaly maisha yake yalivyokuwa baada ya kufika Italia.

Coulibaly aliamua kutoka huko na kwenda kwenye mji mkuu wa Italia na mambo yalizidi kuwa magumu zaidi. Alikumbana na nyakati ngumu zaidi katika kutimiza ndoto zake.

Anazidi kusimulia: “Nilikuwa Rome, hapo wakaniambia kuna Wasenegali wengi sana Pescara, hivyo nikaamua kupanda treni bila ya kuwa na tiketi. Nikashuka Roseto — ilikuwa sehemu nyingine kabisa na nililala uwanjani. Polisi walinikuta hapo na kunichukua na kunipeleka kwenye nyumba ya watu wa mitaani huko Montepagano.

Nikafanya majaribio Cesena, Sassuolo, AS Roma na Ascoli, lakini hakuna hata aliyeshawishika na mimi. Nilipokuwa Senegal nilicheza sana soka kwenye shule mbalimbali na nilijifunza pia kucheza soka la mitaani.”

Kwa muda wote huo, Coulibaly hakuwa akiwasiliana na wazazi wake, hivyo hawakuwa wakifahamu kama yupo hai au la.

“Baba yangu mnoko sana, miaka miwili iliyopita sikumwambia kama nipo Ufaransa, angenifuata nirudi nyumbani. Lakini, kwa sasa tunazungumza kwenye simu kila siku, ameniambia amefurahi na amenisamehe.

“Sijawaona bado na nimemmisi sana mama yangu. Alikuwa akilia tu, hakuwa akifahamu kama nipo hai. Najiona nina bahati sana.”

Coulibaly akisaini Juventus haitakuwa ajabu kama siku moja utamwona kwenye Ligi Kuu England akicheza katika moja ya timu kubwa kabisa baada ya yeye mwenyewe kudai amekuwa akiishabikia Manchester United.