Changamoto 7 zilizoikumba Yanga

KABLA YA pambano la jana Simba walikuwa na uhakika mkubwa kwamba wanaifunga Yanga jeuri hiyo ilikuwa ikiongezeka kadri siku zinavyosogea kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza ndani ya kikosi cha Yanga.

Mashabiki wa Yanga walikuwa na wasiwasi kutokana na mambo hayo yaliyojitokeza lakini ujasiri pekee uliowasukuma kuja uwanjani ni ushindi uliokuwa umepitia timu yao katika mechi tatu za nyuma huku pia kasi ya safu yao ya ushambuliaji bila kusahau vigogo mbalimbali wakipambana kunusuru mambo. Hizi ni changamoto saba zilizotokea kabla ya mchezo huo.

 

MANJI ASHIKILIWA

Pigo kubwa na mshtuko kwa mashabiki wa Yanga ni kukaribia kwa mchezo huo huku mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji ambaye ndiyo kila kitu akiwa ameshikiliwa na vyombo vya dola kwa mambo mbalimbali hili lilichangia kuwaondoa katika akili yao ya kawaida kujiandaa na mchezo huo kutokana na kichwa cha familia kuwa katika msukosuko mkubwa.

Ilifikia wakati hata viongozi wa Yanga walikuwa wanasita kujadiliana mambo ya mpira na Manji kila walipopata nafasi ya kumuona kwa hofu ya kibinadamu kufuatia kiongozi wao kuwa katika matatizo mambo mengi ya uwezeshaji yalikosa usuluhishi wa haraka kutokana na tatizo hilo.

 

YANGA YABADILI KAMBI

Chaguo la kwanza kwa Yanga kwa maana ya kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba ilikuwa ni kutua Pemba ambako kwao ni sawa na machinjioni,Simba haijawahi kuifunga Yanga katika miaka ya karibuni wakati Yanga ikitokea Pemba lakini wakati fikra zikiwa hivyo kambi hiyo ilibadilishwa ghafla baada ya kuonekana ingelazimu bajeti kubwa, badala yake Yanga waliamua kukimbilia Kimbiji, Kigamboni.

 

WAKOSA UWANJA WA MAZOEZI

Yanga walipotua Kimbiji ilikuwa kila kitu kimalizike huko kwa maana ya timu kulala huko na hata kufanyia mazoezi lakini walipofika wakakuta sababu kibao kwamba uwanja mzuri waliopanga kufanyia mazoezi hautaweza kutumika baada ya wahusika kuzuia. Hawakuwa na namna ikabidi timu iwe inasafiri umbali mrefu kutoka Kimbiji mpaka Kurasini kwa safari ya kwenda na kurudi.

Safari hii iliwalazimu Yanga kutumia sio chini ya masaa mawili na nusu katika safari tu ya kwenda mazoezini na kurudi hili ni wazi liliwatibulia mpango halisi wa mazoezi endapo kuna mambo zaidi ambayo makocha wao walipanga kuyafanya.

 

NGOMA AGOMA KUCHEZA

Wakati Yanga ikijiandaa kuingia kambini gumzo kubwa baadaye lilikuwa ni kuingia kambini kwa mshambuliaji wao Donald Ngoma, awali alipata maumivu ya nyonga lakini inadaiwa kwamba alianza mazoezi ya gym hatua ambayo daktari wake alikubali kumpa ruhusa ya kucheza mchezo huo.

Kilichotokea ni kwamba wakati mabosi wa Yanga wakimpeleka Ngoma nyumbani kwake kwenda kuchukua vifaa ili aingie kambini raia huyo wa Zimbabwe alibadili akili yake na kuingia mitini huku akiwazimia simu viongozi wake hili liliwatibulia mipango Yanga kwa kupangua safu yao ya ushambuliaji.

 

BOSSOU NAYE ACHOMOA

Yanga ikianza kutuliza akili katika kutibu changamoto za safu yao ya ushambuliaji ghafla wakajikuta wanapokea pigo lingine kwa beki wao Vicent Bossou naye kugoma kuingia kambini kwa madai ambayo hayakujulikana.

Tofauti na Ngoma ni kwamba Bossou aliifanyia Yanga uso wa mbuzi kwa kuamua kufanya mazoezi na wenzake kisha anapomaliza mazoezi anarudi kwake hakutaka kulala kambini kitu ambacho kisingekuwa rahisi kwa benchi la ufundi kumuingiza katika orodha ya wachezaji waliotakiwa kuivaa Simba.