Cannavaro mbona mapema hivyo?

Muktasari:

Binafsi naheshimu sana mawazo yake na uamuzi wake, pia nakubali sana uwezo wake mkubwa kiuchezaji na uongozi uwanjani, lakini naona ni mapema mno kwa kustaafu kwake timu ya Taifa.

AMEWASHTUA mashabiki wa soka, amewakosesha raha mashabiki wake, hii ni kwa sababu ya uamuzi wake wa ghafla wa kutangaza kustaafu soka kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars.

Uamuzi wa nahodha wa Yanga na aliyekuwa nahodha wa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ umeshangaza wengi na kustaajabisha. Hakuna aliyetarajia kuja ghafla namna hii, lakini ndiyo hivyo tena. Beki huyo wa kati ametangaza kuachana na soka la kimataifa katika timu ya taifa, ikiwa ni siku chache tu tangu Kocha Mkuu wa Stars, Boniface Mkwasa kumtangaza Mbwana Samatta kuwa nahodha mpya ya Stars.

Binafsi naheshimu sana mawazo yake na uamuzi wake, pia nakubali sana uwezo wake mkubwa kiuchezaji na uongozi uwanjani, lakini naona ni mapema mno kwa kustaafu kwake timu ya Taifa.

Cannavaro alikuwa nahodha wa kweli wa kiwango cha kina Sergio Ramos, Carlos Puyol, John Terry na kina Rio Ferdinand katika nafasi yake. Aliweza kuiongoza Stars katika michuano mingi na hivyo makocha wote walimkuta walimheshimu na kufanya naye kazi kwa juhudi kubwa.

Uamuzi wake wa kustaafu umenisikitisha binafsi kwani naamini alikuwa bado na uwezo wa kulitumikia taifa kwa zaidi ya miaka miwili mbele, huku akisubiri mrithi wake katika nafasi yake na unahodha.

Nakumbuka Uingereza ilivyopata tabu kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil baada ya John Terry kujiuzulu, akiwa bado ana uwezo wa kulitumikia taifa lake. Matokeo yake Uingereza ilishindwa kufika mbali na hivyo kutolewa mapema.

Kwenye timu yoyote huwa kuna vita ya namba, hii husababisha mchezaji kuamua kujitoa kwenye timu kama hana moyo wa subira na uvumilivu, pia kama ataona mchezaji mmoja anabebwa na yeye kubaniwa.

Pia kuna vita ya unahodha. Unahodha ni heshima kubwa anayoipata mchezaji katika timu hasa timu ya taifa. Ndiyo maana wapo wachezaji waliwahi kutofautiana kuhusu unahodha. Mfano mzuri ni katika unahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Michael Ballack na Philipp Lahm, kila mmoja alitaka kitambaa cha unahodha kwa wakati huo.

Chanzo nini?

Nguvu ya Samatta kwa sasa inawamwezesha kutamba. Ni wazi kila mmoja amependezwa na Samatta kuwa nahodha mpya wa Stars. Siyo kwamba Stars haikuwa na nahodha bora, hapana, bali ni heshima nyingine anapewa Mchezaji Bora huyo wa Afrika ambaye ataweza kuwahamasisha wenzake na wao wakafikia mafanikio yake. Lakini kwa Canavaro haitakiwi nguvu hiyo ikauzidi moyo wa kizalendo aliokuwa akiuonyesha kwa taifa lake.

Lazima Cannavaro akumbuke, David Beckham alivyopewa unahodha bado Scholes alikuwa anapiga kazi bila tatizo lolote. Ronaldo alipewa unahodha lakini Deco alizidi kupiga kazi akiwa kama injini ya Ureno. Argentina nako, Messi alipewa unahodha lakini Mascherano alizidi kupiga kazi akisimama kama mlinzi hodari. Hata Brazil, baada ya Neymar kupewa unahodha, kina Thiago Silva na David Luiz waliendelea kupiga kazi kuhakikisha taifa lao linasonga mbele.

Muda wa kuachana na timu ya taifa ni kama amefanya uamuzi mgumu lakini wa kukurupuka kwa hasira pengine kwa kitendo cha kupokwa unahodha kwa sababu ya Samatta. Dunia ya sasa inataka manahodha wa aina hiyo, naye anapaswa kukubali kwani hata yeye alichukua kitambaa kwa wengine.

Kama ningekuwa wakala au meneja wake ningemshauri mambo manne na maisha yake ya soka yangekuwa mepesi kabla ya kustaafu kwa heshima kama ilivyokuwa kwa kina Mecky Mexime, Shadrack Nsajigwa na Salum Sued ‘Kussi’.

Acheze na Samatta

Cannavaro ni mchezaji mzoefu na ndiyo maana ameweza kudumu na timu ya taifa. Ni mchezaji pekee ambaye ameweza kuwa nahodha wa timu tatu tofauti, Yanga, Taifa Stars na Zanzibar Heroes. Kwa kucheza na Samatta, angeweza kumpa uzoefu katika kuutumikia unahodha wa Stars. Pia atakuwa amelinda heshima yake kama mchezaji wa Stars pale atakapomkabidhi Samatta unahodha huku akiwa ndani ya Stars tofauti na alivyofanya. Angeweza kumfundisha mengi Samatta kuhusu unahodha.

Alinde heshima yake

Kwa kumwangalia tu Cannavaro ni wazi kwamba ana uwezo wa kuendelea kulitumikia taifa kwa miaka miwili ijayo. Sidhani kama ujio wa Samatta katika nafasi ya unahodha ndiyo sababu ya kustaafu, kuna sababu zake lakini kwa ushauri, Cannavaro angeendelea kulitumikia taifa kwa moyo na uzalendo ili akistaafu astaafu kwa heshima kubwa zaidi ya aliyonayo sasa.

Aangalie maisha yake

Wachezaji wengi wanategemea soka katika kuendesha maisha yao. Cannavaro bado ana nafasi ya kucheza kwa zaidi ya miaka miwili mbele, angeendelea kuitumikia Stars kwa ajili ya kupata mkate wake wa kila siku. Heshima aliyonayo Stars inamwezesha kuendelea kucheza na kupata riziki yake na kwa heshima ya kustaafu angeweza kupata zaidi ya kile alichokifikiria. Kwa mfano vituo mbalimbali vya utangazaji vingempa ulaji kwa kufanya kazi kama mchambuzi wa soka baada ya kuona amestaafu soka kama ilivyo kwa wenzake wa Ulaya. Pia ni yeye aliyetuaminisha kuwa ana miaka minne zaidi ya kucheza kabla ya kutundika daluga sasa imekuwaje tena?

Staili ya kustaafu

Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime alivyostaafu unahodha wa Stars alistaafu kwa kugawa kitambaa cha unahodha kwa Shedrak Nsajigwa.

Vivyo hivyo Cannavaro ili aweze kulinda heshima yake na astaafu kwa heshima, angefanya kama Mexime kwa kuanza kipindi cha kwanza kama nahodha kisha kipindi cha pili akamwachia Samatta kwa kumvalisha na kuaga wenzake. Nadhani hiyo ingempa heshima kama ilivyokuwa kwa Mexime.  Uamuzi wake wa sasa unaweza kumjengea taswira mbaya mbele ya wadau wa soka wakiwamo wadhamini na wafadhili wa timu ya Stars na hata Yanga.