Barcelona inavyoingia chaka bovu

Muktasari:

  • Katika uhamisho wa majira ya joto, Barcelona iliipiku Real pale kocha, Luis Enrique alipomnasa Paco Alcacer kwa Pauni 30 milioni na kumtoa kwa mkopo Munir El Haddadi.

BARCELONA, HISPANIA. MAMBO kutokutulia ndani ya Bodi ya Wakurugezi, usajili wa bei mbaya usio na mipango katika eneo la kiungo na kudorora kwa uhusiano mzuri baina ya wachezaji na maofisa wa klabu, kunaelezewa kuitoa katika njia klabu hiyo na kuwa kama wapinzani wao, Real Madrid, ilivyopotea njia zamani.

Mambo yamegeuka. Si zamani sana, walikuwa ni Real Madrid waliofahamika kwa sera ya kuwasajili mastaa wa klabu nyingine, wakati Barcelona ilisifika kwa sera imara ya kukuza wachezaji wake yenyewe. Sasa inaonekana wazi mambo ni kinyume chake.

Katika uhamisho wa majira ya joto, Barcelona iliipiku Real pale kocha, Luis Enrique alipomnasa Paco Alcacer kwa Pauni 30 milioni na kumtoa kwa mkopo Munir El Haddadi. Pia klabu hiyo ilimsajili, Andre Gomes kwa Pauni 35 milioni wakati mashabiki wengi wakitaka kumwona Sergi Samper akipewa nafasi.

Munir na Samper tayari walishaumudu mfumo wa uchezaji wa Barcelona na kwa hakika wawili hao hawana ubovu wowote unaowazidi watu waliopewa nafasi zao kikosini humo. Lakini kama ilivyokuwa kwa Real miaka ya nyuma, huu ni mfumo wa kutegemea pochi badala ya kukuza vijana. Kinyume chake sasa, Madrid imemrudisha straika aliyekulia klabuni hapo, Alvaro Morata, huku kukiwa pia na vipaji vya Hispania; Lucas Vazquez, Nacho, Marco Asensio na wengene kama vile Mariano – katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu huu.

Kwa hali ilivyo, kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane, ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo aliyekuzwa hapo kutokea timu B, anataka kuachana na mpango wa kutegemea mastaa wa kutoka nje.

Lakini pale, Camp Nou, hata hivyo, ni Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar ndio wanaoiokoa Barcelona na hata gwiji wao ni kama anausaliti mfumo uliomkuza klabuni hapo. Kimfumo wa usajili, Madrid sasa ina mfumo mzuri kuliko mahasimu wao hao.

Juu ya yote, Bodi ya Wakurugenzi ya Barcelona imewakosesha raha wachezaji wengi pale Camp Nou, akiwamo Messi, huku kukiwapo na uchelewashaji mkubwa wa mazungumzo ya mkataba mpya wa Suarez na Dani Alves ameijia kuu bodi hiyo akisema haijui namna ya kushughulikia masuala ya wachezaji.

Zamani, ni Real Madrid ndio ilikuwa na matatizo hayo ambapo, Iker Casillas, alitemwa bila ya kuagwa vizuri licha ya kufanya kazi kubwa pale Santiago Bernabeu. Kwa sasa mambo ya wachezaji yanashughulikiwa vizuri pale Real.

Mashabiki wengi wa Barcelona hawapendi kuona hali iliyopo sasa ikiendelea klabuni kwao, klabu inaonekana kuanza kufanana na Madrid katika enzi za mifumo yake mibovu, kwa chochote kitakachotokea mbeleni msimu huu, Barcelona inahitaji kurejea katika mifumo yake ya asili.