Azam wachemka

Friday May 19 2017

 

By GIFT MACHA

MSIMU unaomalizika ulikuwa ni darasa tosha kwa Azam FC ambayo tangu kupanda Ligi Kuu imekuwa ikila bata tu. Matajiri hao wa Ligi Kuu Bara wamejikuta wakiwa na msimu mbovu zaidi kwao, jambo ambalo limeonekana kama funzo kuwa mpira una milima na mabonde.

Tangu kuanzishwa kwake, Azam imekuwa ni timu inayopiga hatua kwenda mbele. Imekuwa ikiimarika msimu hadi msimu lakini mwaka huu imekutana na kigingi na darasa kwamba hata ukiwa na fedha, vikwazo haviepukiki.

Kwenye soka nyakati nzuri na mbaya zipo, na zina umuhimu wake. Matokeo ya mechi za mwisho za Ligi Kuu ndiyo yatakayoamua nafasi ya Azam kwa msimu huu.

Timu hiyo ipo nafasi ya tatu na pointi 52 na inafuatiwa na Kagera Sugar yenye pointi 50 katika nafasi ya nne. Timu hizo mbili zinakutana kesho Jumamosi na mshindi atamaliza juu ya mwenzake.

Wakati msimu ukimalizika, ni vyema tukatazama milima na mabonde ya Azam katika msimu mpya. Timu hiyo inayomilikiwa na Familia ya Bakhresa ilikumbwa na nini.

Kocha mpya

Azam iliamua kuanza msimu ikiwa na kocha mpya, Zeben Hernandez ambaye alirithi mikoba ya Muingereza, Stewart Hall. Hernandez alikabidhiwa timu mapema na kufanya mapendekezo ya usajili na alifanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chake.

Kwanza, aliwaruhusu washambuliaji, Didier Kavumbagu, Allan Wanga na Ame Ali kuondoka. Baada ya hapo akafanya usajili wa wachezaji Bruce Kangwa, Gonazo Bi Ya Thomas na Fransesco Zekumbawira.

Kocha huyo mzaliwa wa Hispania alianza msimu kwa maandalizi ya nguvu yaliyomwezesha kuanza mechi za mwanzo kwa kasi. Baada ya mechi nne za mwanzo, Azam ilikuwa inalingana pointi 10 na Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Kuondoka kwa Tchetche

Bahati mbaya zaidi kwa Azam ni kwamba msimu ulianza kwa mshambuliaji wao Kipre Tchetche kulazimisha uhamisho wa kuondoka klabuni hapo. Kwa mujibu wa taarifa za Azam ni kwamba mshambuliaji huyo alitaka changamoto mpya.

Kuondoka kwa Tchetche kuliacha pengo kubwa katika safu ya ushambuliaji ya Azam. Tchetche alicheza Azam kwa misimu mitano na kufunga mabao zaidi ya 60 katika mashindano yote jambo ambalo lilimfanya kuwa mtu muhimu zaidi katika kikosi.

Mara nyingi hata kasi ya kufunga ya John Bocco ilitokana na kazi kubwa ya Tchetche ambaye alikuwa na uwezo wa kupunguza walinzi wawili hadi watatu na kwenda kufunga.

Mhispanyola akwama

Simba ilianza kutibua hesabu za Hernandez baada ya kuifunga Azam bao 1-0 katikati ya mwezi Septemba mwaka jana. Kipigo hicho ni kama kiliitia Azam gundu kwani baada ya hapo mambo yalianza kuwaendea kombo.

Azam ilikwenda Mtwara ikafungwa tena na Ndanda. Ikarejea Chamazi ikapata sare ya mabao 2-2 na Ruvu Shooting. Ikasafiri kwenda Kanda ya Ziwa ikafungwa na Standa United na Mbao FC. Vipigo hivi vilitosha kuwavuruga na kuwaondoa katika mbio za ubingwa, tena mapema tu.

Pigo kubwa zaidi kwa Azam lilikuwa kushindwa kurejea kikosini kwa beki wao tegemeo, Sergie Wawa aliyekuwa majeruhi huku beki mwingine, Shomary Kapombe akishindwa kuupata ubora wake mapema kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuumwa.

Washambuliaji, Ya Thomas na Zekumbawira walionekana kuchemka ambapo katika duru lote la kwanza walifunga mabao manne tu. Azam ililazimika kuachana nao katika usajili wa dirisha dogo.

Katika usajili wa dirisha dogo, Azam ilifanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake nao iliachana na viungo, Kipre Bolou na Jean Mugiraneza huku Ya Thomas na Zekumbawira wakiunganishwa pia katika safari hiyo.

Baada ya hapo, Azam iliwasajili nyota wanne kutoka Ghana na mmoja kutoka Cameroon ili kujaza nafasi hizo pamoja na ile ya Wawa aliyeondoka mwenyewe. Nyota hao ni Yahya Mohammed, Samuel Afful, Yakub Mohammed, Enock Agyei na Stephane Kingue.