Azam kumbe imejishtukia mapema

Muktasari:

Azam ilianza msimu ikiyumba ikigeuzwa jamvi la wageni kama iliposhiriki ligi kwa mara ya kwanza, lakini ikaja kuzinduka katika mechi za mwishoni na angalau imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kwenye nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Yanga.

ACHANA na msimu wao wa kwanza wa ushiriki wa Ligi Kuu Bara 2008, ambapo ushamba ulikuwa ukiwasumbua na kujikuta wakigeuzwa jamvi la wageni, Azam huenda wasiusahau msimu huu kwa jinsi walivyoianza ligi vibaya.

Azam ilianza msimu ikiyumba ikigeuzwa jamvi la wageni kama iliposhiriki ligi kwa mara ya kwanza, lakini ikaja kuzinduka katika mechi za mwishoni na angalau imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kwenye nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Yanga.

Matokeo mabaya ya mechi za awali ziliwafanya mashabiki wa Azam, mabosi na hata wadau wengine wa soka kushtuka na mwenendo huo.

Haikuwa kawaida ya Azam kuyumba vibaya katika misimu ya karibuni, ndio haikuwa ajabu kila mtu alipigwa na butwaa na kukumbwa na mshangao.

Katika duru hilo la kwanza la msimu huu, Azam imemaliza kinyonge kwani imeshinda mechi saba droo nne na kupoteza mechi nne.

 

WAJISHTUKIA

Mara baada ya kumalizika kwa duru la kwanza mabosi wa Azam wakishirikiana na kocha wao, Zeben Harnandez wameamua kufanya jambo moja la maana.

Waliamua kuuchangamkia usajili wa dirisha dogo kwa kushusha nyota saba kutoka nchi za Afrika Magharibi ili kuwajaribu na ni mmoja tu aliyepenya hapo.

Mshambuliaji Samuel Afful, ndiye aliyewavutia mabosi wa Azam na kusainishwa mkataba akitokea Klabu ya Sekondi Hasaacan ya Ghana kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi hicho katika safu ya ushambuliaji.

Pia, Azam imewasajili nyota wengine akiwamo Yahya Mohamed kutoka Adouana Stars ya Ghana na Enock Atta Agyei ambaye alikamilisha usajili wake wiki mbili zilizopita akitokea Medeama pia ya Ghana.

Kadhalika Azam imemalizana na Joseph Mahundi kutoka Mbeya City na inaendelea kufukuzia nyota wengine wazawa, akiwamo Idd Mobby kutoka Mwadui baada ya mipango ya kumnyakua Hassan Kabunda kukwama mapema.

 

KOCHA AFUNGUKA

Kocha Hernandez anayeinoa Azam na kufundisha soka Afrika kwa mara ya kwanza, amefunguka mambo kadhaa alipozungumza na Mwanaspoti.

Akiwa anatambua kuwa ana kibarua cha kuhakikisha Azam inafanya vizuri katika Ligi Kuu inayoshika kasi pamoja na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa mwakani, Mhispaniola huyo amejipanga.

Hernandez anasema mzunguko wa kwanza ulikuwa ngumu kwake kutokana na ugeni ndani ya soka la Tanzania na hata katika kikosi cha timu yake, pia kila timu shiriki ya Ligi Kuu ilikuwa imejipanga kutafuta ushindi.

“Raundi ilikuwa ngumu na mliona timu zilijipanga, kila timu ilicheza kwa tahadhari na umakini. Hii iliongeza presha kwa kila timu kusaka ushindi. Kulikuwa na ushindani hakika,” anasema.

 

MAJERUHI TATIZO

Katika michezo mingi ya raundi ya kwanza Azam ilikosa huduma za nyota wake muhimu wa safu ya ulinzi kama Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Pascal Wawa (aliyehamia El Merreikh) na Shomari Kapombe kutokana na kuwa majeruhi.

Kocha Hernandez anakiri uwepo wa majeruhi wengi kwa nafasi hiyo ndani ya kikosi chake kiliiathiri Azam na ndio maana iliyumba kabla ya kuzinduka mwishoni na kuvuna pointi za kutosha.

“Ni vigumu kuwa na majeruhi wengi tena walio muhimu katika timu, lazima timu itikisike. Nililazimika kuwachezesha waliokuwepo. Soka ndivyo lilivyo, wachezaji hawawezi kuwa fiti msimu mzima.”

 

ALIA NA WAAMUZI

Kama unadhani Stewart Hall aliongoza kwa kuwalaumu waamuzi alipokuwa Kocha wa Azam umeula wa chuya, hata Hernandez naye amebaini madudu ya waamuzi tangu alipofika nchini kwa mara ya kwanza.

Anasema hakuwahi kufikiria suala hilo mapema, lakini katika raundi ya kwanza waamuzi hawakuitendea haki timu yake.

“Waamuzi hawakuchezesha vizuri. Kuna wakati unajiuliza kama wanachezesha kwa kufuata maagizo. Sikuridhishwa na kiwango cha uchezeshaji wa waamuzi,” anasema Hernandez ambaye ameadhibiwa na Shirikisho la Soka kwa kufanya sivyo ndivyo timu yake ilipokuwa ikipokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka Mbao FC, jijini Mwanza.

 

LENGO HALIJATIMIA

Kocha huyo anafichua kuwa, Azam ilijipanga kumaliza raundi ya kwanza ikiwa kileleni lakini mambo hayakuwa hivyo, hata hivyo, anasema yaliyopita si ndwele bali anaganga yajayo.

“Malengo yalikuwa ni kufanya vizuri, tumalize katika nafasi ya juu ila haikuwa, kwa sasa tunafikiria jinsi ya kufanya vizuri zaidi kwenye raundi ya pili kwani ushindani utakuwa maradufu na ilivyo sasa,” anasema.

 

VIGOGO WAMTIKISA

Kocha Hernandez anakiri Simba na Yanga ndizo zilizomsumbua katika raundi ya kwanza na sasa hana budi kujipanga kuhakikisha anavunja ufalme wao na kumaliza ligi, Azam ikiwa bingwa.

“Simba na Yanga ndio washindani wetu, tulijitahidi kupambana nao kwa kila hali, lakini hatukuwakamata vilivyo, kwa sasa wapo juu yetu, hatuna budi kujipanga japo najua ushindani ni mkali, ila tutapambana nao,” anasema.

 

USAJILI WAKE

Kuhusu usajili aliofanya mpaka sasa, Hernandez anasema anaamini wachezaji hao wataongeza nguvu katika kikosi chake kinachowania kutwaa taji msimu huu.

“Tuliita wachezaji wa kuwajaribu, tumempata Afful ambaye ninaamini atatusaidia. Pia tumemsajili Yahaya Mohammed na Agyei. Ni wachezaji wazuri ambao wataongeza nguvu kwenye kikosi wakishirikiana na waliopo,” anasema.

 

WALA HANA PRESHA

Akizungumzia ikiwa ana presha na kibarua chake ndani ya Azam, Hernandez anasema wala hana hofu kwa sababu anajua anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ila mambo tu hayakukaa vizuri kwao na anajipanga kurekebisha.

“Soka ni mchezo wa presha muda wote, nalazimika kupambana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri. Sifurahii tunapofanya vibaya, hata wachezaji wangu hawafurahii. Tuna kazi kubwa nayo ni kuhakikisha tunafanya vizuri. Hii itategemea na namna tunavyojipanga na kucheza na wapinzani wetu.”

Pia nafichua: ”Sina tatizo na uongozi wangu, ninafanya nao kazi vizuri na wananiunga mkono kwa asilimia zote. Ninajivunia kwa hilo, kilicho muhimu ni kuendeleza ushirikiano huu na kufanya kazi kwa karibu.”

 

USHINDANI AZAM

Akizungumzia kikosi chake kwa ujumla, Kocha Hernandez anasema Azam ina wachezaji wazuri na zaidi anafurahishwa na ushindani baina yao.

“Ninajivunia wachezaji nilionao ni wazuri na wenye ushindani wao kwa wao. Imani yangu tutafanya kazi na kuhakikisha tunapiga hatua. Azam ni klabu kubwa inayohitaji matokeo na wachezaji wanalijua hilo,” anasema.

 

MIKAKATI YAKE

“Kilicho muhimu kwetu kuelekea mzunguko ujao ni kuhakikisha tunapanda juu ya msimamo na kumaliza ligi tukitwaa ubingwa. Kazi ninayoifanya ni kufanya marekebisho katika maeneo yaliyokuwa na upungufu raundi iliyopita.”

Kocha Hernandez anasema ana imani ya kubeba ubingwa hata kama wapinzani wao katika ligi wanapiga hesabu kama hivyo, akitambia aina ya wachezaji alionao na jinsi wanavyoonekana kuanza kumwelewa vizuri.

Anasema kikosi chake kitaanza kambi ya maandalizi ya duru lijalo Novemba 30, na wachezaji wote wanajua ratiba hiyo na anaamini Simba, Yanga na wapinzani wengine, lazima waombe po katika duru hilo la pili.