Aogelea kilomita moja kukutana na Messi katika boti lake

Muktasari:

WAKATI mwingine kukutana na staa kama Lionel Messi na kupiga naye stori akiwa katika boti lake la kifahari na familia yake inatokea mara moja katika maisha ya mwanadamu. Mhispaniola mmoja amepata nafasi hii na kutumia dakika 20.

WAKATI mwingine kukutana na staa kama Lionel Messi na kupiga naye stori akiwa katika boti lake la kifahari na familia yake inatokea mara moja katika maisha ya mwanadamu. Mhispaniola mmoja amepata nafasi hii na kutumia dakika 20.

Hata hivyo haikuja bure. Suli, mkazi wa mji wa Ceuta ambao unapakana na Pwani ya Morocco amelazimika kuogelea kwa kilomita moja katika fukwe za Ibiza kwa ajili ya kukutana na staa huyo akiwa katika boti yake.

Suli mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni shabiki wa Atletico Madrid alikuwa katika fukwe hizo akifurahia maisha ndipo alipoiona boti ya kifahari ya Messi ikiwa imeegeshwa katika fukwe za Salines kilomita moja kutoka alipo.

Hakufikiria mara mbili kuogelea kuifikia boti hiyo huku akiwaacha rafiki zake katika ufukwe. Aliogelea huku akiwa na mfuko wa plastiki ambao ulikuwa na simu yake ya mkononi. Aliwasili katika boti iliyokuwa imepakiwa katika eneo la Seven C.

Wakati huo, Messi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 29 alikuwa amejifungia ndani ya Boti lakini walinzi wake na wapambe wake walifanikiwa kumuona ‘mvamizi’ huyo na kumtaarifu Messi ambaye alitoka nje kwenda kusalimiana na shabiki huyo.

Kimbwanga kilitokea wakati Suli alipokuwa anataka kupiga picha na staa huyo wa kimataifa wa Argentina lakini akagundua kuwa simu yake ilikuwa imeloa katika mchakato huo wa kuogelea na kumfikia Messi alipo.

Hata hivyo, Messi aliokoa jahazi na kukata kiu ya shabiki huyo baada ya kumuomba mpambe wake mmoja ampige picha na shabiki huyo na kisha angemtumia kupitia moja kati ya simu zake. Kama vile haitoshi, Messi aliendelea kutenda wema kwa shabiki huyo kwa kumkaribisha Glasi ya Juisi huku akiendelea kupiga naye stori.

Messi alimuuza Suli kuhusu wachezaji ambao aliwahi kukutana nao siku za nyuma na alimjibu kuhusu wachezaji aliowahi kukutana nao huku mmoja wao akiwa kipa wa Chelsea na timu ya taifa ya Ubelgiji, Thibaut Courtois.

“Nilipoteza simu yangu lakini nilifanikiwa kupiga picha na Messi. Wakati anaongea na mimi hakuonekana kama staa mkubwa duniani. Alikuwa mpole, mwenye huruma, ilikuwa hivyo kwa yeye na familia. Watu wazuri sana.” alisema Suli.

Kuhakikisha kuwa alikuwa mtu mwema, Messi alihakikisha kuwa Suli anafika salama ufukweni kwa kumtuma mtu ampeleke na Boti ya Mwendokasi na kuhitimisha hadithi nzuri na ya kusisimua kwa Suli ambaye hatasahau kamwe katika maisha yake.

Hata hivyo, stori hiyo ya Suli haikuweza kurudiwa tena wakati alipokutana na hasimu wa Messi, Cristiano Ronaldo katika klabu ya usiku ya Balearic iitwayo Pacha. Mabaunsa walimlinda vema kiasi kwamba watu waliokuwepo, akiwemo yeye walishindwa kumsogelea.

“Sikuweza hata kumshika mkono. Alikuwa amezungukwa na walinzi na sikuweza hata kumkaribia,” alisema Suli.