Ana ana do ndani ya Stars

Muktasari:

Njia pekee ya Samatta na Ulimwengu kutocheza ni kuumia ama kutokupata ruhusa kutoka katika klabu zao vinginevyo hakuna namna nyingine.

KATIKA kikosi cha Taifa Stars ni wachezaji wawili tu, ambao wamejihakikisha nafasi ya kuanza. Ni Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu aliyekuwa akikipiga TP Mazembe.

Njia pekee ya Samatta na Ulimwengu kutocheza ni kuumia ama kutokupata ruhusa kutoka katika klabu zao vinginevyo hakuna namna nyingine.

Viwango vyao havina shaka, ndiyo maana wamekuwa wakiendelea kutamba nje ya nchi.

Kwa wachezaji wengine ambao wamekuwa wakijumuishwa katika kikosi hicho ni lazima wapigane kupata nafasi ya kuanza. Viwango vyao pamoja na mfumo wa Kocha Boniface Mkwasa ndivyo vinavyoweza kuwabeba.

Makala haya yanakuletea vita iliyopo baina ya wachezaji wa Stars, wewe unaweza kuona nani ana nafasi kubwa ya kucheza mbele ya mwingine.

 

MANULA/DIDA

Viwango vya makipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga na Aishi Manula wa Azam vinampa wakati mgumu Kocha Mkwasa kujua nani aanze na nani akae benchi. Dida ana uzoefu mkubwa zaidi, lakini amekuwa akikumbana na changamoto ya Manula, ambaye amejipambanua kuwa kipa bora zaidi nchini. Kwa sasa kabla ya mechi ya Stars ni vigumu kufahamu ni kipa yupi anaweza kuanza kwani, yeyote akianza baina yao ni sawa. Katika mechi ambazo wamecheza wote wameonyesha viwango vya juu.

 

ABDUL/KAPOMBE

Kipindi cha nyuma kila mmoja alikuwa anakubali kuwa Shomari Kapombe ndiye beki bora zaidi wa kulia nchini, lakini kwa sasa kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara ameporomoka kidogo na kuibua ushindani. Katika kikosi cha Stars kwa sasa Mkwasa anapata wakati mgumu kufahamu nani kati ya Kapombe na Juma Abdul anastahili kuanza.

Hata hivyo, Abdul naye amekuwa akisumbuliwa na majeraha hivyo kuiweka rehani nafasi yake ambapo, sasa beki Hassan Kessy huenda akajumuishwa katika kikosi cha Stars badala yao.

 

MWINYI/TSHABALALA

Mpaka sasa ni vigumu kusema yupi ni beki bora zaidi wa kushoto nchini kati ya Mwinyi Haji wa Yanga na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba. Mabeki wote hao wana uwezo mkubwa wa kukaba, kupanda kusaidia mashambulizi na kupiga krosi. Tofauti yao kubwa ni kwamba, Mwinyi ni mrefu na Tshabalala ni mfupi. Katika kikosi cha Stars ushindani wao ni mkubwa.

 

DANTE/MWANTIKA

Wakati mwingine unaacha kocha aamue ni nani anastahili kuanza kwani, viwango vya mabeki David Mwantika wa Azam na Andrew Vincent wa Yanga vipo juu kwa sasa. Dante amekuwa akianza katika kikosi cha Yanga wakati ambapo, Mwantika amekuwa mchezaji anayepewa nafasi zaidi katika kikosi cha Azam. Katika kikosi cha Stars beki yeyote kati yao anaweza kuanza na ikawa poa tu.

 

YONDANI/MORRIS

Mabeki katili wa kati, Kelvin Yondani wa Yanga na Aggrey Morris wa Azam nao wameibua ushindani mkali juu ya nani aanze na nani akae benchi katika kikosi cha Stars. Morris amekuwa hajumuishwi katika kikosi cha Stars mara kwa mara, lakini kwa sasa ameonyesha kiwango cha kuvutia ambacho kinaweza kumshawishi Kocha Mkwasa kumwongeza tena. Yondani amekuwa na kiwango bora msimu huu ambapo, amekua akianza mara kwa mara hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kuitwa kwenye kikosi cha Stars.

 

MKUDE/MAO

Kuna wakati Mkwasa huwa anaamua kukwepa lawama katika eneo hili na kuwaanzisha viungo Jonas Mkude wa Simba na Himid Mao wa Azam kwa pamoja. Mkude na Mao hawakosekani katika vikosi vya kwanza vya timu zao na wote wamekuwa katika viwango bora, jambo ambalo linampa wakati mgumu Mkwasa kuona ni nani aanze katika kikosi chake. Viungo hao wawili wamekuwa na uwezo mkubwa wa kukaba na kupandisha timu jambo ambalo limewafanya kuwa viungo wa daraja la juu nchini.

 

MZAMIRU/MUDATHIR

Nafasi nyingine ambayo ina ushindani mkubwa katika kikosi cha Stars ni ya kiungo mshambuliaji ambapo, sasa Mzamiru Yassin wa Simba ametia maguu na kuwapa changamoto Frank Domayo na Mudathir Yahya wa Azam. Mzamiru amekuwa katika kiwango bora msimu huu ambapo, mbali na kutengeneza nafasi za kufunga tayari ameifungia timu hiyo mabao manne na kuwa kiungo aliyefunga mabao mengi zaidi nchini. Katika kikosi cha Stars itakuwa ni vita kubwa juu ya nani aanze na nani akae benchi katika nafasi hii.

 

MAGULI/MANDAWA

Katika eneo la ushambuliaji la Taifa Stars kwa sasa kuna ushindani mkubwa nani acheze na Samatta kati ya Elius Maguli anayekipiga nchini Oman na Rashid Mandawa anayetusua hapo Mtibwa Sugar. Maguli yupo kwenye kiwango bora hadi kupata nafasi nchini Oman wakati Mandawa amekuwa moto msimu huu akifunga mabao sita mpaka sasa.

Nafasi hii inakabiliwa na ushindani mkubwa pia kutoka kwa Mussa Abdulrahman wa Ruvu Shooting aliyefunga mabao matano mpaka sasa na John Bocco wa Azam mwenye mabao manne. Bocco amekuwa akipewa nafasi kutokana na uzoefu wake mkubwa.

 

KASEKE/KICHUYA

Winga moja ya Stars ni ya Thomas Ulimwengu hivyo ushindani mkubwa umebaki katika winga ya kushoto ambapo, ni baina ya Deus Kaseke wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba. Nyota hao wote wamekuwa katika viwango bora msimu huu ambapo, Kichuya tayari ameifungia Simba mabao saba huku Kaseke akiwa ameifungia Yanga mabao matatu na kupika mengine mengi. Katika kikosi cha Stars yeyote atakayecheza ni poa tu kwani, ushindi ndio mpango mzima.