Micho: Sio TFF tu, hata Yanga nimeshateta nao

Muktasari:

Ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika Mashariki na Kati akiwahi kufundisha hapa nchini katika klabu ya Yanga, lakini hata Uganda alipo kwa sasa na The Cranes, alishawahi kufanya kazi kwa mafanikio na SC Villa.

ACHANA na kitendo chake cha kuipeleka timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2017) baada ya kupita miaka 39, lakini ukweli Kocha Milutin ‘Micho’ Sredojevic ni bonge la kocha.

Ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika Mashariki na Kati akiwahi kufundisha hapa nchini katika klabu ya Yanga, lakini hata Uganda alipo kwa sasa na The Cranes, alishawahi kufanya kazi kwa mafanikio na SC Villa.

Rwanda, Ethiopia na hata Afrika Kusini kote amewahi kuacha alama zake kwa kufundisha, hivyo huwezi kumdanganya katika soka na maisha ya soka la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, amelowea muda mrefu.

Mwanaspoti lilimfungia safari kocha huyo hadi Uganda na kufanya mahojiano maalumu na yeye yaliyozaa makala haya ambapo, alifunguka mambo mengi ya kusisimua, ikiwamo miujiza aliyoifanya Uganda. Kivipi? Endelea naye...!

Mwanaspoti: Kuifikisha Uganda fainali za Afcon limekuwa jambo kubwa sana, nini ilikuwa siri ya mafanikio hayo? Pia umepata uzoefu gani kwenye fainali hizo?

Micho: Tulifuzu baada ya kupita miaka 39. Haikuwa kazi rahisi, ni matunda ya umoja na kujituma, hakika tulifanya maandalizi ya kutosha, hasa mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu bora ikiwamo Ivory Coast.

Kule kwenye fainali zenyewe tulipata ushindani mkubwa. Imetusaidia sana kuwa timu imara zaidi. Hata kama hatukufika mbali, lakini kwa Uganda kucheza dhidi ya Ghana na Misri katika mashindano makubwa kama yale, imetuachia faida kubwa kiufundi.

Mwanaspoti: Nini hasa kiliwafanya mshindwe kufikia hatua ya juu zaidi katika fainali zile?

Micho: Si jambo rahisi kutwaa ubingwa wa Afcon. Ushindani ulikuwa mkubwa ndio maana tukaishia hatua ya makundi. Lakini kama nilivyosema, kwa Uganda kucheza fainali zile ilikuwa na faida kubwa kiufundi, ndio maana tulifanya vizuri pia kwenye Kombe la Chalenji kule Ethiopia tulikotangazwa mabingwa.

Mwanaspoti: Uganda sasa ina nafasi gani kufuzu fainali za Kombe la Dunia?

Micho: Ninaamini nafasi ipo, ijapokuwa njia ya kupita ina miiba mingi. Kwanza tuna mechi mbili ngumu dhidi ya Misri na Ghana, kwa ugenini pia dhidi ya Congo Brazzavile, lakini tukipata pointi tatu au nne itatusaidia.

Lengo ni kucheza Kombe la Dunia licha ya changamoto zinazotukabili, fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazoanza Juni, zitakuwa sehemu ya maandalizi yetu pia kuelekea Kombe la Dunia.

Mwanaspoti: Kuna taarifa kuwa unataka kuachana na Uganda, ipoje hii?

Micho: Kwa sasa mimi ni mwajiriwa wa The Cranes. Ninafurahishwa na kazi yangu, hata mashabiki wa hapa wanaipenda sana timu yao, wanaisapoti kwa kiwango kikubwa. Wanaifanya hata kazi yangu kuwa nzuri japo kuna ofa nyingi zinazonifuata.

Mwanaspoti: Je ungependa kurudi kuifundisha Yanga, au Taifa Stars?

Micho: Yanga na TFF (shirikisho la soka Tanzania) wote ni rafiki zangu, hata watu wa Simba pia ninaelewana nao. Nina uhusiano mzuri na viongozi wa timu zote kubwa za Tanzania, hata Rais wa TFF (Jamal Malinzi), huwa tunawasiliana mara kwa mara na kubadilishana mawazo ya soka.

Hivyo siwezi kuzungumzia juu ya kurudi Yanga au kuifundisha Taifa Stars kwa sasa, lakini kumbuka katika soka huwezi kusema huu ndiyo mwisho.

Huwa nalifuatilia soka la Tanzania, Yanga walikuwa na kocha mzuri, Hans Pluijm na sasa wana George Lwandamina, ninaamini watafanya vizuri. Nawatakia ushindi pia katika mechi yao ya marudiano ya kimataifa dhidi ya MC Alger (ya Kombe la Shirikisho).

Lakini Simba wanapambana kutwaa ubingwa wa ligi, najua Azam nao wapo vitani kwani hawajafanya vizuri sana msimu huu. Kiujumla naikubali Tanzania katika soka. Ni nchi inayojali watu muda wote.

Mwanaspoti: Umesema unalifuatilia soka la Tanzania, unaizungumziaje Ligi Kuu Bara hasa jinsi bingwa anavyopatikana?

Micho: Mpira unachezwa, nakumbuka kuna msimu Simba ilianza vizuri kwenye ligi, lakini ikapoteza mwishoni. Unajua ubingwa unategemea jinsi gani umejipanga kuuchukua, hata kwa mbinu za nje ya uwanja maana mambo hayo kwenye soka yapo.

Kwa msimu huu Yanga wana changamoto kubwa, wapo kwenye michuano ya kimataifa, wachezaji wamechoka kimwili na kiakili, hivyo wajitahidi kupambana, nawaombea waitoe MC Alger.

Mwanaspoti: Unamzungumziaje Juuko Murshid (beki Mganda anayekipiga Simba) ni mchezaji wa aina gani? Mipango yake ikoje katika soka?

Micho: Nafikiri Simba haijajua ni wachezaji wa aina gani inawahitaji, ama jinsi gani ya kuwatumia waliopo. Juuko ni mchezaji mzuri, ana dhamira ya kwenda Ulaya na katika kikosi changu, anafanya vizuri sana.

Kiujumla Tanzania ina mchango mkubwa kwa wachezaji wa Uganda. Tanzania na Uganda sasa ni kama ndugu. Ninawashukuru sana Watanzania, viongozi wa klabu na waandishi kwa ujumla katika hili wameweza kuwasaidia wachezaji katika soka, tumekuwa tukishirikiana vizuri kwenye mambo ya michezo.

Mwanaspoti: Umemwita Okwi na kumpa unahodha, wakati wa fainali za Afcon ulimwacha, ana nini jipya?

Micho: Kwenye klabu yake (SC Villa) kwa sasa anafanya vizuri. Katika mechi saba amefunga mabao sita. Nimefuatilia na kiwango chake kimepanda, hivyo nimemwangalia kiufundi zaidi.

Nasikia anajiandaa kurudi Tanzania, kama atarejea atakuwa changamoto mpya, hata kama atakwenda sehemu nyingine naamini atalifurahia soka lake.

Anajua maana ya soka. Ndio maana alipokuwa Denmark pamoja na kupata pesa nyingi, lakini alithamini soka. Alipoona hapati nafasi ndio akaamua kurejea Villa ili acheze na sasa anafanya vizuri.

Ninazungumza naye mara kwa mara kuhusiana na maisha ya soka, maana ni kama mdogo wangu.

Hata nilipomwita, amefanya vizuri kwenye mechi tulizocheza, dhidi ya Kenya ambayo tulitoka sare ya 1-1 na dhidi ya timu ya jeshi la Ufaransa tuliyoifunga 3-1.

Naamini bado Okwi atanifaa hata kwenye CHAN na kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia. Unajua binadamu huwa anaendelea kukua siku hadi siku kabla ya kufikia uzee.

Hicho ndicho kilichopo kwa Okwi, hivi sasa anaonekana kukuwa zaidi kisoka, namtakia kila la kheri, ajiamini na aweze kufunga mabao mengi zaidi.

Mwanaspoti: Umefundisha soka kwa miaka mingi Afrika Mashariki, unadhani nini kifanyike kukuza soka kwa nchi hizo?

Micho: Katika ukocha nina miaka 25. Nimekuwa Afrika Mashariki kwa muda wa kutosha tu. Naamini kwa muunganiko wenu wa Rwanda, Uganda, Kenya na Tanzania na Burundi, kinaweza kufanyika kitu kikubwa.

Tena kwa uwepo wa Ahmed Ahmed (Rais mpya wa CAF, shirikisho la soka la Afrika) tunaweza kufanya kitu kikubwa kama serikali za nchi hizi zitaamua kuleta mabadiliko katika soka.

Angalia, kuna wachezaji kama Mbwana Samatta, ana mafanikio makubwa baada ya kujitambua haraka. Alipata nafasi TP Mazembe akaitumia vizuri na sasa yupo Ulaya (KRC Genk ya Ubelgiji) ambako anafanya vizuri pia, hata Taifa Stars anaisaidia.

Pia alikuwepo Mrisho Ngassa, alikwenda Free State (ya Afrika Kusini), nasikia amerudi Tanzania anacheza Mbeya City, ni mchezaji ambaye ana kipaji kikubwa, atakuwa amerudi ili kupandisha tena kiwango kama alivyofanya Okwi kurudi Villa, wote hao nawatakia mafanikio mema, bado wana nafasi.