Msimbazi mjipange, shughuli ni pevu

Muktasari:

HAUKWEPEKI. Ndivyo unavyoweza kusema juu ya Mkutano Mkuu wa Simba. Awali mkutano huu ulitangazwa kufanyika Julai 10, lakini uongozi wa klabu hiyo ukaahirisha na kutangaza utafanyika upya mwishoni mwa mwezi huu.

HAUKWEPEKI. Ndivyo unavyoweza kusema juu ya Mkutano Mkuu wa Simba. Awali mkutano huu ulitangazwa kufanyika Julai 10, lakini uongozi wa klabu hiyo ukaahirisha na kutangaza utafanyika upya mwishoni mwa mwezi huu.

Uongozi umesema sasa utafanyika Julai 31, japo hakuna anayejua nini kitatokea tena, ila ni kwamba mkutano huo haukwepeki hata iweje na watoto wa uswahilini wana msemo wao kuwa kurukaruka wa kwa maharage chunguni ndio kuiva kwake.

Mkutano huo wa wanachama unafanyika katika kipindi ambacho mashabiki wa klabu hiyo hawapo vema kwa vile hawana furaha kutokana na timu hiyo kushindwa kutoa ubingwa kwa misimu 4 iliyopita.

Pamoja na kwamba timu hiyo haifanyi vibaya katika Ligi Kuu Bara, lakini hata kuipata nafasi ya kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa nako ni mitihani na hivyo wadau wa klabu hiyo hawaridhiki.

Kukosa nafasi hiyo ya michuano ya kimataifa kwa miaka minne kumeifanya Simba kubezwa na watani wao wa jadi, Yanga ya Dar es Salaam na kupewa majina ya kebehi kama vile wa Mchangani na wa Matopeni.

Mwanaspoti inakuletea mambo 10 ambayo uongozi wa Simba unatakiwa ujipange kweli kuweza kuwajibu wanachama wake, ambao nao wanawajibu wa kuhoji siku ya mkutano huo, panapo majaliwa ya Mungu kwa mustakabali wa klabu yao.

 

1. Mapato na matumizi

Moja ya mambo ambayo wanachama wa Simba wanapaswa kuhoji uongozi ni suala la mapato na matumizi ya klabu hiyo angalau kwa msimu uliopita.

Uongozi wa klabu nyingi hukwepa kutoa mapato na matumizi ya klabu zao na hutafuta njia ya mkato za kukwepa hilo na kumaliza mkutano bila kutoa maelezo yoyote juu ya mapato na matumizi ya fedha.

Hilo ndio jambo la msingi kwa uongozi madhubuti kuwaeleza wanachama wake kwani ndio itakayowaonesha weledi wao uongozi na uadilifu wao.

Hivyo wanachama wa Simba wanawajibu wa kujua mapato yaliyoingia katika klabu yao na kujua jinsi yalivyotumika kwa uwazi na kwa usahihi.

 

2. Njia za kujipatia mapato

Mbali na uongozi wa kutoa ripoti ya mapato na matumizi, pia unapaswa kuwaeleza wanachama wao ni njia zipi watatumia kuingiza mapato ili waweze kuendesha klabu hiyo kwa mafanikio.

Wanachama wa klabu ya Simba wanapaswa kujua jinsi ambavyo klabu yao itapata fedha za kujiendesha, ili isiwe kwenye mkwamo wowote wakati ligi itakapoanza.

Lakini pia ni muhimu kwa wanachama wa klabu hiyo kujipanga na kuwa tayari kusaidia kwa kutoa michango ambayo itaongeza kipato cha klabu hiyo.

Simba ina wadhamini, lakini bado kipato inachokipata kuendesha klabu hiyo hakitoshelezi kwani ina gharama kubwa kubwa za kuihudumia timu zikiwemo mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi, kambi ya timu na kukodi viwanja vya mazoezi kwa kutaja kwa uchache.

 

3. Mipango ya maendeleo

Wanachama hawana budi kuutaka uongozi wao uwaeleze mipango yao ya maendeleo kwa klabu hiyo angalau kwa msimu ujao.

Klabu inayoendeshwa bila ya kuwa na mipango itakuwa inafanya mambo yake shaghalabaghala na itakuwa vigumu kupata maendeleo ya uhakika.

Rais Evans Aveva na wenzake wanalazimika kuwaeleza wanachama wao juu ya mipango yao ya maendeleo ili kuitoa hapo ilipo na kuipeleka katika mazingira ya hali ya juu zaidi.

 

4.Ujenzi wa uwanja

Wanachama wanapaswa kuwauliza viongozi wao juu ya ujenzi wa uwanja wa mazoezi ulianza kujengwa na klabu hiyo maeneo ya Bunju, jijini Dar es Salaam.

Ujenzi wa uwanja huo umechukua muda mrefu na ni wakati muafaka kwa viongozi wa Simba kuwaeleza wanachama wao juu ya hatma ya uwanja huo.

Kwa miaka mingi Simba imekuwa inakodi viwanja kwa ajili ya mazoezi ya timu yao jambo ambalo linagharama kubwa na haliendani na hadhi ya klabu hiyo.

Hata kama Simba haina uwezo wa kujenga uwanja wa kuchezea mechi kwenye majukwaa, lakini haina budi angalau kuwa na uwanja wa mazoezi na ni bora zaidi ikajenga na hosteli kwa ajili ya kuweka kambi timu yao.

 

5. Kwanini haifanyi vizuri?

Huu ni muda muafaka katika mkutano huo wa wanachama wa Simba kujiuliza na uongozi wao kwanini timu hiyo haifanyi vizuri kwa kuchukua ubingwa katika msimu minne iliyopita.

Mkutano huu ni jukwaa zuri kwa wanachama kutoa dukuduku lao badala ya kuwa na mijadala pembeni kutaka kuusikia kwa viongozi wao sababu za timu yao kuyumba.

Wakijua sababu wanachama hao watoe ushauri wa jinsi ya kuziiondoa ili klabu yao ionje ubingwa wa bara ambao haujanusa Msimbazi tangu ilipotwaa kwa mara ya mwisho msimu wa 2011/2012.

 

6.Usajili mpya ukoje?

Katika kipindi hicho cha misukosuko ya kutofanya vizuri, Simba imesajili wachezaji 85 lakini hayo yamepita na wanachama sasa wanachotaka kujua usajili wa wachezaji kwa msimu ujao ukoje.

Ni dhahiri kwamba klabu inavyofanya usajili mzuri inajiweka katika mazingira mazuri ya kuweza kufanya vizuri katika Ligi Kuu.

Kwa hiyo wanachama wana haki ya kupata maelezo yakinifu juu ya usajili wa nyota wa kikosi chao na pia benchi lao la ufundi.

 

7. Kina Singano wameondokaje?

Weka pembeni beki Hassan Kessy aliyetua Yanga baada ya mkataba wake kumalizika Simba, lakini wanachama wana haki ya kuhoji juu ya utitiri ya wachezaji wao wa vijana ambao wamehama klabu hiyo.

Wachezaji kama Ramadhani Singano, Abdallah Seseme, Christopher Edward, Miraji Juma na wengineo baada ya kukuzwa na kuinukia vizuri ndani ya Simba hawapo tena klabuni hapo.

Wakati kulikuwa na matumaini kwamba Simba ndio klabu ya mfano inayozalisha wachezaji wake lakini wote hao wamepotea.

 

8. Kwanini makocha hawadumu?

Wanachama wa Simba wanapaswa kuwahoji viongozi wao ni kwanini katika miaka ya karibuni makocha wanaoifundisha timu hiyo wanatimuliwa mara kwa mara na kuifanya Simba wakati mwingine ifundishwe na makocha wawili kwa msimu mmoja?

Wanachama hao wanapaswa kujua hilo kwani huenda ni moja ya madudu yanayoitafuna timu yao na kushindwa kupata maendeleo.

 

9. Ahadi gani msimu mpya?

Wanachama wanapaswa wapewe ahadi kutoka kwa Rais Aveva na wenzake ya kwamba timu itafanya vizuri katika msimu ujao na kubeba ubingwa.

Lakini ahadi hiyo isiwe kama ya msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara aliahidi aulizwe ifikapo Mei kama Simba sio bingwa, lakini hadi leo hajatoa jibu.

 

10. Hatma ya wanachama waliofukuzwa

Suala jingine ambalo wanachama wa Simba wanapaswa kuwauliza viongozi wao ni juu ya wanachama wenzao ambao walifukuzwa ndani ya klabu hiyo na uongozi wa Rais Aveva.

Wanachama hao hawana budi kuuliza juu ya wanachama wenzao kwani hakuna sababu ya msingi ya kuwatenga ikieleweka kwamba siku zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Mambo hayo ni baadhi ya masuala ambayo wanachama wa Simba wanapaswa kuyapa kipaumbele katika mkutano huo wa wanachma na viongozi waingie ukumbini wakiwa na majibu yake.

 

Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Business Times (Mhariri Mwanzilishi wa Spoti Starehe) na Mwananchi. Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF). Anapatikana email [email protected] simu 0712-020020