‘Guardiola’ wa Azam alistahili

Friday December 30 2016Zebenzui Hernandez

Zebenzui Hernandez 

KWA wanaokumbuka Alasiri ya Mei 19 kulikuwa na picha zilizopamba mtandao wa Azam na mingine za kijamii zikimwonyesha Mhispania Zebenzui Hernandez akitia saini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.

Huyo ndiye aliyekuwa Kocha Mkuu mpya wa Azam aliyetua nchini kutokea Hispania akiwa sambamba na Kocha viungo Jonas Garcia.

Baadaye lilifuata jopo lingine la makocha wengine wasaidizi akiwamo Yeray Romero, Pablo Borges na Jose Garcia na kulifanya benchi la Azam kusheheni makocha watano wa Hispania, huku ikitabiriwa kucheza soka tamu la kuvutia.

Wengi waliamini kama ilivyo kwa Man City ya Pep Guardiola ndivyo ambavyo Azam ingetandaza soka na pengine kulingana kidogo na lile la Barcelona.

Hata walipohojiwa makocha hao walidokeza mipango yao ni kuifanya Azam kucheza soka la kampa...kampa tena...yaani tik..tak.. Walionekana ni watu wenye mambo mengi mapya, aina mpya ya soka la pasi fupi fupi, staili mpya ya usajili ya kuita wachezaji kutoka nchi mbalimbali kufanya majaribio.

Wakamiminika wachezaji kutoka Ghana, Ivory Coast, Zimbabwe na kwingineko ili kunusa shekeli za matajiri wa Chamazi. Kali kuliko zote makocha hawa wakaruhusu wachezaji muhimu kuondoka kama Kipre Tchetche, Kipre Balou na hivi karibuni Mnyarwanda Jean Baptiste Mugiraneza, Ya Thomas Gonabo, Fransisco Zekumbawira nao wakaonyeshwa mlango wa kutokea. Mapya yakawa mapya kila siku. Azam ikawa Azam kweli. Ile Azam ya Stewart Hall iliyokuwa na uwezo wa kuchukua pointi pale Sokoine, Nagwanda Sijaona, Majimaji na Stand United taratibu ikaanza kusanda kwa kupata matokeo yasiyoridhisha uwanjani.

Miezi saba ya ndoa ya Azam na Hernandez na wenzake ilikamilika juzi kwa Wahispania hao kupigwa chini kutokana na matokeo mabovu inayovuna timu hiyo. Meneja Mkuu wa Azam, Abdul Mohammed aliishia tu kusema Hernandez amefukuzwa kutokana na matokeo mabovu.

Jana, uongozi ulimtangaza Kally Ongalla aliyekuwa Majimaji, kuwa kocha wake. Hata hivyo, Mwanaspoti linaangazia mambo kadhaa ambayo ilikuwa ni lazima kwa makocha hao kutimuliwa pale Chamazi.

Mabadiliko ya kikosi

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Azam ilitengeneza kizazi cha wachezaji waliokaa pamoja na kuelewana kama Kipre Tchetche, Kipre Balou, Jean Mugiraneza, Pascal Wawa na wengineo waliondoka. Mhispania huyo na jopo lake hawakufanya juhudi zozote kuhakikisha nyota hao wanabaki badala yake waliridhia kuondoka kwao.

Matokeo yake timu ikaanza kuhangaika kwa kuwa alishindwa kupata wachezaji sahihi wa kuziba mapengo badala yake alisajili wachezaji ambao, hivi karibuni walivunjiwa mikataba yao. Unabaki vipi kwa mfano.

Usajili wa gharama

Ndani ya kipindi cha Kocha Hernandez, Azam imejikuta ikitumia fedha nyingi kusajili. Katika kipindi cha miezi saba alichokuwepo Azam, Hernandez na jopo lake amesajili mchezaji aliyemtaka na viongozi walimuunga mkono. Nyota kama Enock Atta Agyei, Daniel Amoah, Yahya Mohammed, Yakubu Mohammed, Fransisco Zekumbawira, Ya Thomas Gonabo, Bruce Kangwa, Samuel Afful na Joseph Mahundi.

Usajili huu umeshindwa kuilipa Azam kwa kuwa kiwango cha timu kimebaki kile kile. Unaposajili nyota wazoefu watu wanahitaji mabadiliko, kama hamna inakuwaje? Lazima utaondoka tu.

Azam ipi ya kibarcelona?

Alipokuja tu nchini Hernandez alitangaza Azam itacheza kama Barcelona. Akasahau kuwa huku kuna viwanja vya ‘mabonde poromoka’ kama Nangwanda Sijaona, Majimaji.

Inawezekana Hernandez alikuja akijua miundombinu iliyopo Barcelona ndio iliyopo hapa  Bongo. Katika mahojiano niliyofanya naye alisisitiza anataka timu yake icheze soka la kupasiana. Mtapasiana vipi pale Kambarage au Majimaji? Matokeo yake Azam ya Stewart Hall tuliyoizoea ghafla ikaanza kutoweka machoni petu. Hapa Hernandez amelipa gharama za mbinu alizokuwa akizitumia.

Matokeo mabovu

Ni kweli kwamba kila kocha anakuja na mifumo na mbinu zake ambazo anaamini zitamsaidia kuleta mafanikio. Hayo ni tisa, kumi kinachoangaliwa ni matokeo na mafanikio husika. Hernandez alianza kwa matumaini kwa kutwaa taji la ngao ya hisani kwa kuichapa Yanga, lakini kilichofuata ni majanga.

Hadi jana mchana (kabla haijacheza na Prisons usiku pale Chamazi), Azam ilikuwa imecheza mechi 17 na kushinda mechi saba, kutoa sare sita na kuchapwa mechi nne. Unavumiliwaje hapa kwa mfano?

Hall, Hernandez ni watu tofauti

Ni dhahiri shahiri Stewart Hall aliijenga Azam ikajengeka. Wachezaji walikaa pamoja kwa muda mrefu na kuelewana. Alichokifanya Hernandez ni kufuta legacy (urithi) aliouacha Hall na kuanzisha yake ambayo amefeli kabla hata ya kufikia matarajio. Hakuna kilichobadilika katika staili ya uchezaji. Unaponaje hapa kwa mfano? Hata hivyo, imethibitika kuwa Hall na Hernandez ni watu wawili tofauti wenye mipango mkakati na soka la Azam.

Matarajio ya viongozi

Tangu awali viongozi wa Azam walionyesha shauku baada ya kukiri mabadiliko ya benchi la ufundi yanalenga kupata mafanikio zaidi ya yaliyopatikana. Kiongozi mmoja mwandamizi wa Azam alisema hawatakuwa na simile ya kumfukuza kazi Hernandez ikiwa matokeo ya timu hayataridhisha.

Hernandez alikiri wazi matokeo yasiyoridhisha yalikuwa yakimpa presha ya kufutwa kazi. Bila shaka tiketi kaipata sasa na amevuna alichopanda.

Ni dhahiri Hernandez aliyetoka klabu ya daraja la tatu alikuja kufundisha soka Afrika akidhani kila kitu kinaendeshwa kama Ulaya, bahati mbaya hakuwahi kufundisha kabisa Afrika na ilikuwa mara yake ya kwanza.

Licha ya Azam FC kushindwa kumthamini kwa jumla katika kipindi cha miezi saba aliyokaa Chamazi na huenda hakujua mabosi wake wanahitaji nini, kilichompata ndiyo hicho ulichosikia na imebaki stori tu.