HATARI TUPU: Wanaigeria wanalitibua soko la muziki Bongo

TIWA

Muktasari:

  • Mdj wanajua ili watu wasiondoke katika “dancefloor’’ ni lazima wapige nyimbo za Nigeria. Bila kupiga Testmoney, Ayee, Skelewi, Away Dance, GingerMama Africa, Adama na nyingine usiku wa mpenda burudani hauwezi kuwa umekamilika.

Kuna kilio kinasikika kwa mbaaali. Wanamuziki na wadau wanalalamika kuwa muziki wa Nigeria unapandishwa na Bongo Fleva inapotezewa.

Cha kujiuliza ni iwapo muziki huu unabebwa au ni ubora wa kazi hizo ndio unaowavutia mashabiki.

Mdj wanajua ili watu wasiondoke katika “dancefloor’’ ni lazima wapige nyimbo za Nigeria. Bila kupiga Testmoney, Ayee, Skelewi, Away Dance, Ginger,  Mama Africa, Adama na nyingine usiku wa mpenda burudani hauwezi kuwa umekamilika.

Ukweli ni kwamba hawa jamaa wameshaharibu fomesheni ndiyo maana sasa hivi wasanii wanabuni mbinu mbalimbali ili angalau waweze kupata kitu kidogo.

Kuwakwepa na kutafuta njia nyingine siyo dawa, kinachotakiwa ni kuhakikisha Bongo Fleva inasimama na huu ugonjwa wa ‘Naija Muziki’  unatokomea katika mlango ulioingilia.

Kuna tukio la hivi karibuni limetokea kwenye burudani ya Muziki. Mwanamuziki Davido alipotembelea nchini mwaka jana huenda alituibia kitu na sasa ndicho kinamfanya akombe mamilioni ya pesa.

Inawezekana Davido alipokuja alikusanya CD nyingi za kundi la Offside Trick kama siyo za AT na kwenda kutoka na wimbo mkali ambao sasa unafanya vizuri.

Ukisikiliza wimbo wake, “Aye” una kila sababu ya kuamini kuwa Davido ameiba mahadhi ya mduara wetu na kwenda kufanya mambo mbele ya safari.

Huu ndio ukweli

Bongo Fleva haipo dukani halikadhalika muziki wa Nigeria. Maana yake ni kwamba hakuna duka lolote sasa hivi linalouza cd za muziki. Nyimbo zote unazozisikia mitaani ni za kunyonya kutoka mtandaoni.

Kuwezeshwa kwa mitandao kumeifanya dunia iwe kijiji. Leo hii huwezi kumdanganya mpenda burudani kuhusu wimbo mpya au sinema mpya iliyotoka. Ukifumba na kufumbua utakuta tayari anayo; iwe kwenye simu, kompyuta au cd.

Kwa maana hii kumlaumu mtu fulani kuwa ndiye chanzo cha muziki huu kushika nchini hoja hii haitakuwa na ukweli wowote.

Watanzania huwa wanapata faraja na fahari wanapoziona  nyimbo za wasanii wetu zikionyeshwa katika vituo vya kimataifa kama vile; Mtv Base, Channel O na Trace. Hutamani kuziona mara kwa mara kwa kuwa wakiamini hiyo ndiyo njia pekee ya kujitangaza kimataifa.

Lakini kwa asilimia 80, nyimbo za Nigeria ndizo zinazoonekana kwa wingi zikifuatiwa na Afrika Kusini, Ghana, Zimbabwe na nchi nyingine zinazochuana na Tanzania. Ukweli ni kwamba, nyimbo nyingi za Nigeria zinazopigwa katika vituo hivyo zina ubora wa hali ya juu na ndiyo sababu pia wimbo wa Diamond, Number One na ile ya Remix zimekuwa zikipigwa zaidi.

Nyimbo za Ay, Shaa, Ben Pol na wengine waliorekodi katika ubora zikipigwa. Kwa maana hiyo kinachoangaliwa huko ni ubora wa kazi na siyo propaganda.

Hapa nyumbani, kusema eti vyombo vya habari vinawabeba Wanigeria itakuwa uonevu. Vyombo vya habari vinajihusisha na biashara, hivyo ni haki kuwapa wateja kile wanachokipenda kwa wakati ule.

Kama kumbukumbu zipo sahihi ni kuwa, katikati ya miaka ya 90 muziki wa Bolingo ndiyo uliokuwa ukipendwa zaidi nchini, lakini haukuzifanya bendi zetu ziache kufanya kazi na kwa kipindi chote hicho bado tunazizungumzia.

Mpaka sasa ushabiki wa bendi kongwe kama Msondo na Sikinde upo juu kwa kuwa pamoja na changamoto hawakuacha kufanyakazi kwa bidii.

Kati ya mwaka 2006 na kuendelea muziki wa Afrika Kusini maarufu kama Kwaito nao ukashika chati hapa nchini. Kwenye redio, televisheni na magazeti habari za wanamuziki wa huko zilibamba.

Rapa mkongwe  Profesa Jay aliwahi kukiri kuwa Wanaigeria wamefikia viwango vya juu ingawa naye alilaumu kuwa muziki wa nyumbani haupewi nafasi ya kutosha katika vyombo vvya habari.

 “Bado muziki wetu hatujafikia ‘level’  kama za P Square, ambao wanaweza kufanya shoo kubwa Ulaya,” anasema Jay na kuongeza:

“Sababu kubwa inayokwamisha ni pamoja na wasanii wengi kukosa ubunifu. Unaweza kuwachukua wasanii 10 kwa sasa, wakafanana kila kitu wanachoimba, yaani wanafanya ‘kucopy’  tu. Kwa jinsi hiyo, muziki hauwezi kufika mbali.”

Jay anasema kuwa pamoja na udhaifu huo jambo la pili ni vyombo vya habari kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuutangaza muziki wa Bongo Fleva kama inavyofanyika kwa wasanii wengine wa Nigeria.

Kilio hiki sio kwa wasanii wa Tanzania pekee, kimeenea Afrika Mashariki kwani hata msanii wa Uganda, Bebe Cool aliwahi kulalamika kuwa vyombo vya habari vya nchi hiyo vinaubeba muziki huo.

Nchini Kenya nako halikadhalika, Dj maarufu wa kundi la Codered, DJ Styles aliwahi kusema kuwa muziki huo unapigwa sana nchini humo lakini alisema hiyo ni changamoto kwa wasanii nchini humo.

“Wanaigeria wanakuja kuwaamsha wanamuziki wa Kenya, sioni ubaya muziki huo kupigwa sana kwani utawafanya wanamuziki waamke na kuona wanachofanya sicho kinachohitajika kwenye tasnia,” anasema Dj Styles.

Muziki umesambaaje nchini

Wasanii wenyewe wanachangia kuutangaza muziki wa Nigeria. Kuna baadhi ya nyimbo ukisikiliza unasikia zile swaga za Kinaigeria kama ‘Dey say’, Me Lovu U na nyingine. Watayarishaji wa muziki nao wanatengeneza midundo ambayo kama sio Lugha ya Kiswahili iliyotumika huwezi kuzitofautisha na nyimbo kama za Orezi, M.I, Waje, Nneka na wengine.

Wasanii wakilalamikia hili bila kufanya kazi  ni njia moja ya kutafuta huruma ya Watanzania.  Wakifanya kazi nzuri wataendelea kuthaminiwa kwa juhudi zao.

Wakati mwingine ni vizuri kukubali ushindani unapotokea na kuutumia kama msukumo wa kujituma zaidi na hushinda.

Kukaa na kulalamika, maana yake unakubali kuwa Wanaigeria wamekuzidi. Watanzania wanajua kuwa Wanaigeria wako juu, lakini Mtanzania anapofanya vizuri wanajua na humuunga mkono.

Ay, Ommy Dimpoz na  Diamond wamefungua milango kwa kufanya kazi na wasanii wa Nigeria. Wasanii wengine wanaweza kufuata nyayo zao na kujifunza mbinu mbalimbali za kuliteka soko la Afrika.

Wimbo mmoja tu aliofanya Diamond na msani wa Nigeria, Davido umemfanya aanze kumpumulia kisogoni mwanamuziki huyo.

Hivi majuzi mitandao Kenya iliripoti ikishangaa kwanini Davido atake kulipwa kiasi cha Sh4 milioni za Kenya wakati Diamond wanaeamini ni msanii mkali analipwa Sh2 milioni za Kenya.

Diamond kulipwa nusu ya pesa ambayo msanii mkubwa kama Davido analipwa ni mafanikio ya hali ya juu. Hii maana yake Diamond sasa anakaribia levo za Davido.

Hadithi hii ya Diamond na Davido inatukumbusha ule usemi : “Kama huwezi kushindana naye, ungana naye”. Wakati kampeni za kuupiga vita muziki wa Nigeria zikiendelea yeye ameona njia sahihi ni kuungana nao.

Lakini, kabla ya kufikia huko ni lazima ukubali kuwa Wanaigeria wameliteka soko, siyo kitu kilichotokea ndani ya usiku mmoja. Hivyo ni bora kujifunza kuliko kulalamika.

Mkumbuke kuwa wakati Wanaigeria wakikalia usukani, hawajalala. Kutwa wapo Ulaya na Marekani wakiingia mikataba na kampuni za kimataifa kama Convikt Music, Universal Records na nyingine.

Mbona filamu wameweza!

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 habari ya mjini ilikuwa ni filamu za Kinigeria. Hakuna Mtanzania ambaye aliacha kuangalia filamu ya ‘ Pastor Kenny’. Genevieve , Omotola, Ramsey Nouah, Chika Ike, Muna, Majid na wengine ndio majina yaliyokuwa akilini mwa wapenda filamu.

Lakini taratibu pamoja na vikwazo vya hapa na pale angalau sasa tunaweza kusema tasnia ya filamu nchini imewashika Watanzania.

Watu wanafuatilia zaidi filamu za Mzee Majuto, Jb, Dk Cheni, Irene Uwoya, Wema Sepetu, Kapturado na wengine kuliko za Nigeria.