Tamasha la Band Lilikuwa bab’ kubwa

FM Academia

Muktasari:

  • Tamasha hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam lilifanya na kupokewa kwa msisimko wa aina yake na mashabiki waliohudhuria kwani walipata kile walichokikosa kwa muda mrefu.

ACHANA na mapungufu kadhaa yaliyojitokeza ikiwemo kuhudhuriwa na watu wachache, ukweli ni kwamba Tamasha la Bendi, ‘Tanzania Band Festival’ lilikuwa bab’ kubwa.

Tamasha hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam lilifanya na kupokewa kwa msisimko wa aina yake na mashabiki waliohudhuria kwani walipata kile walichokikosa kwa muda mrefu.

Bendi 13 kutumbuiza kwa pamoja sio jambo lililowahi kutokea katika siku za karibuni, lakini sasa imefanyika na kunonga vilivyo.

Bendi za Msondo Ngoma, Mlimani Park ‘Sikinde’, B Band, Akudo Impact, FM Academia, Skylight, Twanga Pepeta, Yamoto, TOT Plus, Mapacha Watatu, King Kiki, Top Band na na SQ International Band walinogesha burudani kiasi cha watu kudhani lilikuwa shindano la kuwania mkwanja mrefu sana kumbe ni raha tu.

Jinsi hali ilivyokuwa

Tamasha hilo lilifunguliwa saa 12 jioni kwa bendi ya TOT Plus kutoa burudani kabla ya kuipisha Akudo Impact, Sikinde, QS Internationa, King Kikii, Family Team, Msondo, Yamoto, B Band, Top Band, Skylight Band, Mapacha Watatu, Twanga Pepeta kisha FM Academia wakamaliza kazi saa 10 alfajiri.

Kila bendi ilivyopanda kutumbuiza ndivyo mashabiki walivyokuwa wakilipuka kwa shangwe za furaha kuonyesha walivyokunwa na burudani iliyokuwapo uwanjani hapo.

Baadhi yao walishindwa kuvumilia na kulazimika kuviacha viti vyao ili kujimwaya uwanjani kusindikiza nyimbo zilizokuwa zikitumbuizwa.

Bendi zilizoonekana kugusa mitima ya wengi ni FM Academia, Yamoto Band, Mapacha Watatu, Skylight, Msondo, Akudo Impact, TOT Plus, Sikinde, Twanga Pepeta na King Kiki, ila sio kama zingine hazikufanya vema ila mzuka ulikuwa huko.

Pamba kali

Wanamuziki wanajua kupigilia pamba asikuambie mtu, Wazee wa Ngwasuma, Akudo Impact, Msondo, Sikinde, Mapacha Watatu na Twanga Pepeta walifunika kwa pamba kali jukwaani. Jamaa walivutia kwa mavazi kuanzia wanamuziki wao wakiwemo waimbaji na wapiga ala hadi madansa. Ilikuwa tamu sana.

Mbali na mavazi, lakini kulikuwa na burudani nyingine katika tamasha hilo kwani, marapa wa bendi hizo ni kama walikuwa kwenye mchuano fulani hivi.

Marapa hao Sauti ya Radi, Joto, Katalogi, G Seven, Chekidaa, walifunika mbaya kwa jinsi walivyokuwa wakigani na kuwapeleka harijojo mashabiki hadi walipagawa.

Madansa matata

Kama unadhani marapa hao walikuwa wamefunika mbaya kuliko wengine, umekosea hata kwa wanenguaji nako kulikuwa hakujambo.

Chiba yule wa Yamoto Band, alifunika mbaya. Jamaa alikuwa kivutio kwa staili yake ya kuingia kama kafungwa pingu, hivyo anatafuta mtu amfungue huku akiwa hana magongo na kukata maono. Wengine waliobamba tamashani ni wanenguaji wa kike wa Mapacha Watatu kwa staili yao ya kuganda wakifuatiwa na FM Academia kwa staili yao ya kuingia na kuimba wimbo wa taifa na baada ya hapo wanenguaji kucheza kama askari na kuzunguka kwa kujichanganya tofauti na bendi zingine na staili zao zile zile za zamani ndizo walizoonyesha siku hiyo.

Utata mwanangu

Tamasha hili halikuwa shindano, lakini ili kuongeza mvuto aliyekuwa mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliahidi bendi itkayoshangiliwa sana itazawadiwa Sh 1 milioni.

Sasa utata unakuja hivi, kila bendi ilikuwa na mashabiki wake, hivyo bendi ikipanda jukwaani ikishuka inaondoka au zingine zinabaki na kwa mashabiki hivyo hivyo. Kadri muda ulivyozidi kwenda na usiku mnene kuzidi kuingia baadhi ya mashabiki walianza kuondoka na bendi zilizoimba zikaanza kuondoka hadi inafika saa 9 usiku ilibakia bendi mbili za FM Academia na Twanga Pepeta.

Huku mashabiki hao wakiwa wachache mno tofauti na tamasha lilivyoanza muongoza shughuli hiyo, Khamis Dakota alipanda na kutangaza kuwa ameachiwa fedha zilizoahidiwa na RC Makonda.

Akauliza ni bendi ipi inastahili kuzichukua fedha hizo, kelele zikaenda kwa FM Academia kwamba ndio wazibebe wakati huo ilikuwa bado haijapanda kumalizia ngwe.

Kiongozi wa bendi hiyo, Nyoshi El Saadat aliposikia bendi yao ikipigiwa upatu aliomba nafasi ya kuzungumza na kutaka fedha hizo zigawanywe kwa bendi zote kwani, lile halikuwa shindano na isingevutia wao waondoke na ‘jiwe’ kilaini tu. MC Dakota aliwauliza mashabiki kama wanakubaliana na ushauri wa Nyoshi, wote wakaafiki na kumpongeza Nyoshi kwa uungwana na ubinadamu alioonyesha.

Twanga wadinda kinoma

Hata hivyo, katika hali ya ajabu wanamuziki wa Twanga Pepeta walikuwa karibu na gari yao walianza kuimba ‘Tunataka… hela zetu…Tunataka… hela zetu… na wengine wakaanza kuhoji Nyoshi ni nani hadi aamue.

Wanamuziki hao walishinikiza wapewe wao fedha hizo kwa madai ilishangiliwa zaidi kuliko bendi yoyote tamashani, lakini hawakutoa jibu wakati wanaulizwa juu ya ushauri wa Nyoshi kwamba, fedha hizo zigawanywe kwa bendi zote.

Mapungufu

Licha ya tamasha hilo kufana, lakini kuna mambo yaliyochanganya watu, mashabiki walidhani tamasha hilo ambalo linapaswa kufanyika kila mwaka lingehusisha zaidi bendi za dansi kuliko mseto uliofanywa pale Leaders. B Band, Top Band na nyingine za muziki wa kizazi kipya ni kama ziliingizwa chaka mbele ya Twanga Pepeta, Msondo Ngoma. Japo tamasha lilikuwa tamu kwelikweli.

Pia halikwenda na muda kwani, muda uliotangazwa haukuzingatiwa. Matangazo yalionyesha tamasha lingeanza saa 5 asubuhi, lakini ukweli lilianza saa 12 jioni.

Aidha, hata muda wa bendi moja kutumbuiza jukwaani nao haukuwepo na kuleta mkanganyiko kuna bendi zilizotumia dakika 45 nyingine 20, dakika 30 na bendi nyingine hadi saa moja, hii haikuwa haki katika tamasha lililoratibiwa kisomi.