BITCHUKA: Sina tatizo la moyo dharau zilinikimbiza Msondo Ngoma

Muktasari:

  • Mashairi ya huo wimbo hapo juu yameimbwa na Bendi ya Nuta Jazz. Wimbo unaitwa Nidhamu ya Kazi, ni tungo moja nzuri yenye kuleta ujumbe murua kwa wapenzi wa muziki wa dansi .

NIDHAMU ya kazi ni msingi wa mafanikio mema kaziniiii…. viongozi na wafanyakaziiiiiiiii… lazima wote tuwe na nidhamuuu………..migogoro na migongano ya kazini ni ukosefu wa nidhamuu…….

Mashairi ya huo wimbo hapo juu yameimbwa na Bendi ya Nuta Jazz. Wimbo unaitwa Nidhamu ya Kazi, ni tungo moja nzuri yenye kuleta ujumbe murua kwa wapenzi wa muziki wa dansi .

Kwa kundika tungo hiyo, wapenda burudani na mashabiki wa bendi kongwe hapa nchini ni lazima watakuwa wameshajua namzungumzia nani leo hii.

Si mwingine ni Hassan Rehani Bitchuka, mwanamuziki mwenye sauti kinanda na isiyochuja licha ya kuwa kwenye muziki kwa zaidi ya miaka 33.

Bitchuka ambaye ni shabiki mkubwa wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, pia ndiye mwanamuziki wa dansi unayeweza kuvutiwa naye kumtazama akiwa jukwaani kutokana na jinsi anavyojua kuucheza muziki wa dansi kwa ufasaha.

Bitchuka pia ni mtunzi wa Wimbo wa ‘Fikirini Nisamehe’ na nyingine nyingi akiwa na bendi tofauti. Nyimbo zake zinaonesha ukomavu wa utunzi wa nyimbo za Kitanzania.

Hayo na mengineyo mengi ni baadhi tu ya sifa za msanii huyu zilizolishawishi Mwanaspoti, kufanya mahojiano na mkongwe huyo nyumbani kwake Sinza, White Inn jijini Dar es Salaam hasa baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo mkubwa huku kudaiwa kumua kuachana na muziki.

AKANUSHA UZUSHI

“Jamani nawashangaa watu wanaonizulia magonjwa au kunisemea mambo ya moyoni mwangu, kwani ni vizuri kama hivi wewe umesikia na umekuja kuniuliza, kwa ukweli siumwi huo ugonjwa ambao naambiwa nina moyo mkubwa na wala sijatangaza kuacha muziki, miye naomba watu waelewe tu kuwa, naumwa macho na nimefanyiwa upasuaji kama hivi unavyoniona

“Na siwezi kuacha muziki na sifikirii kwani naielewa vizuri kazi hii ya muziki, hivyo watu waache kuunganisha matukio na kama wanavyotangaza,”alisema Bitchuka.

UKIMYA

Bitchuka anasema ukimya wake kwa sasa umesababishwa na matatizo ya macho ambayo yalianza kumsumbua takribani miaka miwili iliyopita.

Mwanamuziki huyo ambaye ni swala tano anafafanua kwamba mwanzo alikuwa akihisi vumbi la hapa na pale ambalo lilikuwa likimsumbua, lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda ndio tatizo limekuwa kubwa na kuamua kwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kuambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji.

Bitchuka maarufu kwa jina la Stereo, anasema tangu afanyiwe upasuaji katika Hospitali ya Kairuki iliyopo Mikocheni wiki moja iliyopita anaendelea vizuri.

SIRI YA SAUTI YAKE

Bitchuka ni mwanamuziki mwenye sauti yenye kuvutia sana pindi anapoimba na ameacha pengo kila alipohama kwenye bendi kiasi cha kushindwa kupatikana mrithi wake.

“Kwanza nataka utambue kuwa muziki upo kwenye damu na nimerithi kwa baba na mama. Wazazi wangu wote walikuwa wasanii, baba akipiga ngoma na mama akicheza ngoma za Warua maarufu sana mkoani Kigoma.

SAFARI YA MUZIKI

“Ni siku nyingi sana nilianza muziki mwaka 1973, nilikuwa ninasoma Shule ya Msingi Kipapa mjini Kigoma, lakini nikaacha shule nikaenda kucheza mpira kwenye timu ya Breweries, Mjini Arusha, enzi hizo nilikuwa nacheza namba tatu hadi saba, ingawaje sikucheza sana nikaacha, baada ya Said Mabela wa Msondo Ngoma kuja Arusha na kunishawishi nijiunge na bendi ya National iliyokuwa na makazi yake Ngarenaro.”

KWA NINI ALIACHA MPIRA?

“Unajua mpira nilienda kucheza kwa ajili ya ujana na wala sikuwa naupenda mpira kama muziki, mara nyingi nyumbani kwetu ilikuwa ni kuimbaimba tu na kwa kuwa Mabela alikuwa ananijua ilikuwa rahisi kwangu kuingia kwenye muziki kupitia yeye.”

KUJIUNGA NA SIKINDE

“Mwaka 1980, nilijiunga na Bendi ya Mlimani Park Ochestra baada ya kuachana na Nuta Jazz iliyokuwa ikiniliipa mshahara mdogo sana wa Shilingi 300, hazikunitosha licha ya kwamba nilikuwa bado kijana sikuwa na familia na Mlimani Park iliahidi kunilipa Sh 2,500 pamoja na marupurupu kibao, nilijiunga Mlimani niliyokaa nayo kwa miaka minne, nikahamia OSS mwaka 1985.”

KWA NINI ALIONDOKA MLIMANI?

Sikuondoka kwa kupenda na sikuwa peke yangu, tulikuwa wanamuziki sita, mimi, marehemu Abel Bartazali marehemu, marehemu Muhidin Maalim Gurumo, marehemu Kassimu Rashidi, marehemu John Ngosha na Ally Makunguru.

“Sababu kubwa ilitokana na meneja wa Mlimani Park wakati huo, marehemu Funda, alisema kwenye moja ya vikao vya bendi kwamba mtu akiumia kazini atajua mwenyewe, bendi haitatambua, hicho kitu kilitukera sana ndio tukaamua kuondoka.

“OSS nilikuwa na mkataba wa miaka miwili mwaka, na nilikuwa nalipwa Sh12,000 ilikuwa nyingi na angalau iliweza kupunguza baadhi ya matatizo yangu.”

BAADA YA MKATABA KUISHA

“Ikiwa imebaki miezi mitatu au minne mwaka 1990 meneja mpya wa Mlimani Park, Herizon Mwampulo, alinihitaji, hivyo nilivyomaliza mkataba wangu nikarudi na hapo nilikuwa nalipwa Sh190,000.

“Japo sikukaa sana mwaka huohuo nikarudi Nuta wakati huo ikiitwa Ottu ‘Msongo Ngoma’, ambapo nilikaa kwa muda wa miaka 12 kabla ya kurudi tena Mlimani Park mwaka 2012.

SABABU YA KUONDOKA MSONDO

“Niliondoka Msondo kwa sababu kulikuwa na dharau sana, binafsi huwa simdharau mtu na sitaki kudharauliwa. Wakati huo kiongozi wa bendi alikuwa, Said Mabela.

SABABU ZAIDI YA KWENDA OSS

“Kweli nilikuwa nazunguka zaidi kwenye hizi bendi mbili lakini nilivyoenda OSS, mbali ya matatizo ya meneja pia nilikuwa nataka kupima uwezo wangu wa kufanya kazi umefika wapi na kwa kiasi gani mashabiki wa muziki wanaikubali kazi yangu.

“Nilijua nini nilikuwa nafanya, lakini vilevile nilitaka kujifunza kutoka kwa wengine nini wanafanya hapo pia nilifanikiwa na nilijifunza zaidi na zaidi.”

UPINZANI ZAMANI

“Kipindi hicho upinzani ulikuwa kwenye steji zaidi, lakini kwa baadhi ya wasanii walikuwa na chuki hadi nje ya steji, wanaaamua kukukasirikia hata ukiwasalimia hawaitikii vizuri,” anafunguka.

FAMILIA

Bitchuka ambaye anaweka wazi kuwa hakubahatika kupata elimu kwa kiasi kikubwa, anajivunia ujuzi katika muziki, kutembea hadi Marekani na kujulikana na wengi.

Mkongwe huyo alizaliwa mwaka 1955, Ujiji, Kigoma, ameoa na mkewe anaitwa Zainabu Salumu na amebahatika kupata watoto wanne, Salimu, Salma, Mwanaidi na Masoud na pia ana wajukuu wanne.