ROMA- (2): Ana jeuri, kiburi

Roma anasema changamoto ya vitisho imewafanya baadhi ya wasanii kushindwa kuendelea na muziki wa aina yake kwa hofu ya kufanyiwa lolote ama baada ya kupokea vitisho

Muktasari:

Roma anasema vitisho vimekuwa sehemu ya maisha yake na ndiyo sababu amekuwa akiweka jumbe mbalimbali katika nyimbo zake kuashiria kuwa lolote linaweza kutokea muda wowote.

“....NIKAMATENI si mlishindwa Tibaijuka, leta difenda, leta Wajeda, leta Wagambo, Roma nimejitoa sadaka...”

Ni mistari inayopatikana kwenye wimbo wa Viva Roma, imebeba ujumbe mzito na unaoonyesha ujasiri. Mwanzoni mwa wimbo huo pia Roma amezungumzia kuhusu kupewa vitisho mbalimbali.

Roma anasema vitisho vimekuwa sehemu ya maisha yake na ndiyo sababu amekuwa akiweka jumbe mbalimbali katika nyimbo zake kuashiria kuwa lolote linaweza kutokea muda wowote.

“Kuna wakati nalazimika kuamka usiku wa manane na kuhama nyumbani, nakuwa na hofu ya kufanyiwa chochote maana siyo kila mtu anapenda kuambiwa ukweli,” anasema.

“Siwezi kusema napokea vitisho kutoka kwa nani, lakini vitisho vipo, hiyo ndiyo sababu hata kwenye wimbo wa Viva Roma nimeimba juu ya hilo.

“Natetea haki ya kila mmoja, lakini siyo wote wanapenda, mfano unaweza kutetea maslahi ya polisi, ila wakachukulia vinginevyo, wengine wanaona kama umewadhalilisha,” anaeleza

“Mfano kuna wakati nilikamatwa jijini Mwanza na kuwekwa mahabusu, nilipowatazama polisi niliona kabisa baadhi yao wakinitamani, walikuwa wakiniangalia kwa uchu.”

Roma anasema changamoto hiyo ya vitisho imewafanya baadhi ya wasanii kushindwa kuendelea na muziki wa aina yake kwa hofu ya kufanyiwa lolote ama baada ya kupokea vitisho.

“Kuna wakati Izzo B alitoa wimbo wa ‘Ongea na Mshua’, baada ya hapo alikumbana na changamoto nyingi na ndiyo sababu akaamua kubadilika na sasa anatamba na wimbo wa Kidawa,” anasema.

Mtiti ulianzia mwanzo

“...Najua msema kweli hufa mapema sijali, kama mlimuua Amina hapa chuma cha reli, kwanza kwetu nimeaga wakanichinjia mbuzi na kunibless nije mjini kutetea wanyonge...”

Ni mistari iliyopo kwenye wimbo wake wa kwanza uliobeba jina la Tanzania ambao ndiyo uliomtambulisha nchini kutokana na kuwa na mistari mikali na yenye kuonyesha ushujaa.

Roma anasema baada ya kutoa wimbo huo alikutana na changamoto nyingi hasa woga kutoka katika baadhi ya vituo vya redio ambavyo viliogopa kuucheza wimbo huo.

“Ilikuwa ni changamoto kwangu, ndiyo kwanza nilikuwa nimeenda Dar es Salaam ili kuutambulisha wimbo huo, sehemu nyingi nilikoupeleka ilikuwa ni tatizo, waliogopa kwa madai kuwa ulikuwa na mistari mikali,” anasema

Ubunge

Roma anasema baada ya kutoa nyimbo zake kadhaa kuna baadhi ya viongozi wa serikali walimfuata na kumuomba akagombee ubunge lakini akagoma kwa kuwa kitendo hicho kingeharibu muziki wake.

“Kuna wakati baadhi ya viongozi walinifuata, ni viongozi wakubwa tu na kuniomba nigombee ubunge, walisema wamevutiwa na kazi ninazofanya,” anasema.

“Tatizo ni kwamba ukishajiunga na chama cha siasa unakuwa umechagua upande mmoja wa kufanya nao kazi wakati ukiamua kuwa mwanaharakati unakuwa huru kukosoa upande wowote.

“Nakuwa huru pia kutamba kama msanii, nakuwa huru kupanda jukwaa lolote la siasa iwe jukwaa la CCM ama la Chadema,” anaeleza.

Kutumika kisiasa

Roma anasema yupo huru kufanya shoo kwenye jukwaa la chama chochote lakini anayemwalika ni lazima akubaliane na masharti yake ikiwemo kumpa uhuru wa kuimba nyimbo zake.

“Kuna kipindi Idd Azan (Mbunge wa Kinondoni) alinialika kwenye mkutano wake, alikuwa anaenda kuzungumza na vijana hivyo akaona njia pekee ya kuwaleta karibu ni kunialika, nilikwenda na vijana walifurahi.

“Hivyo ndivyo ninavyofanya kwa sasa, niko huru kwenye chama chochote, wakifika dau nitakwenda kuimba kwenye kampeni zao lakini si kufanya kampeni,” anasema.

Roma anasema kwa sasa ameshindwa kufanya kazi na baadhi ya wagombea kutokana na wengi wao kushindwa kufika dau, huku akiwashangaa pia baadhi ya wagombea kuwatumia wasanii wanaoimba nyimbo nyepesi katika kampeni zao.

“Leo unashangaa kuona msanii fulani anaimba katika mkutano wa chama cha upinzani, msanii anayetamba na nyimbo za mapenzi wakati hiyo ilitakiwa iwe nafasi ya Roma kutokana na aina ya nyimbo ninazoimba.

“Kwa sasa pia nimekuwa na hofu ya kupanda jukwaani, baadhi ya wagombea wanafikiri kwa kuwa Roma anaimba nyimbo za kuikosoa serikali basi atapanda jukwaani bure, hiyo imekuwa changamoto,” anaeleza Roma baba wa mtoto mmoja.

“Mimi ni msanii na ninategemea kula katika kazi yangu hivyo lazima waje niwape bajeti yangu, wakifika dau basi nitakwenda kufanya kazi zao.”

Ampania JK, amkosa

Roma anasema wakati anatamba na kibao chake cha ‘Mr President’ alipata mwaliko katika maadhimisho ya Malaria ambapo pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alikuwa mwalikwa.

“Kipindi natoka chuo wakati huo natamba na kibao cha ‘Mr President’ nilialikwa kwenye maadhimisho ya Malaria, nilipata pia taarifa kuwa rais atakuwepo.

“Nilipania kwenda kuimba mbele ya rais tena wimbo ambao unamchana rais, kwa bahati mbaya sikufanikiwa,” anasema.

“Wakati napewa nafasi ya kuimba rais alikuwa ameshaondoka, mpango wangu ukawa umefeli.”

Wasanii hawana njaa

Roma anasema kitendo cha wasanii kutumika katika siasa kwa sasa siyo njaa kama watu wanavyodai bali ni kwamba wanafanya biashara ya kazi zao.

“Ukisema wasanii wana njaa utakuwa unakosea, basi hata shoo za kawaida ambazo huwa tunafanya ni njaa, siyo kweli, hii ni kazi na mtu akifika bei huwezi kukataa,” anasema.

“Msanii anapewa fedha ambazo hajawahi kuzipata tangu ameanza sanaa, unafikiri atakataa vipi? Unapokuwa na jina kubwa ni lazima uone faida yake na ndivyo ilivyo kwa sasa.

“Tatizo ambalo lipo kwa sasa ni kwamba siasa imekuwa ngumu, mtu anatamani msanii aimbe na baada ya kuimba afanye na kampeni pia, wengine wanawanunua tu wasanii ili kuweka vitu katika mitandao,” anasema.

Kumbe kamsema mama

Roma anasema mama yake amekuwa mzito kumkubali katika kazi anayoifanya kutokana na muziki anaoimba lakini kuna baadhi ya muda ananyoosha mikono juu.

“Mama amekuwa mgumu kidogo kukubali muziki wangu, kuna wakati anakubali kama tukienda sokoni pamoja akaona namna vijana wanavyonishangilia, anafarijika.

“Yeye ni daktari, na kama unakumbuka niliwahi kuimba na kusema wagonjwa wanakufa wakati daktari anakunywa pombe, madaktari wenzake wamekuwa wakimtania pia juu ya hilo,” anaeleza.

Roma ni nani

Roma alianza kutamba katika muziki miaka minane iliyopita alipoachia wimbo uliobeba jina la Tanzania. Baada ya hapo alitoa nyimbo nyingine kali kama Pastor, Mechi za Ugenini, Mr President, Mathematics, 2030, KKK, Mwanakondoo na wimbo wa Viva Roma Viva unaotamba kwa sasa.