Msitafute mchawi, muziki wa injili umeshuka hivi...

Bahati Bukuku na Christina Shusho.

Muktasari:

  • Ilifika hatua sasa, muziki wa injili umekuwa maarufu zaidi kuliko hata Bongo Fleva, ambao unaminika kupendwa na kuwa na mashabiki wengi hasa vijana.

SI jambo la kawaida unapoingia kwenye maduka yanayouza kaseti za muziki bila kusikia nyimbo za injili zikipigwa.

Maduka mengi ya muziki yamekuwa yakipiga nyimbo za injili kwa sauti kubwa kwa lengo la kuvutia wateja.

Kila unapokutana duka la muziki, nje ama ndani utakutana na spika za uhakika na nyimbo za injili ndizo zimekuwa zikitikisa kwa kuchezwa zaidi.

Ilifika hatua sasa, muziki wa injili umekuwa maarufu zaidi kuliko hata Bongo Fleva, ambao unaminika kupendwa na kuwa na mashabiki wengi hasa vijana.

Kwenye kumbi za burudani, harusi na hata shughuli za kisiasa, muziki wa injili ulishika chati kubwa kutokana na kupendwa na wengi. Hata hivyo, kwa sasa mambo yamekuwa tofauti kidogo.

Muziki wa injili umeshuka kwa kasi sokoni tofauti na miaka ya nyuma, ambapo hata wasanii wake walitengeneza fedha ndefu sana kuanzia kwenye mauzo na hata kupata shoo karibu kila wiki kupitia matamasha ya injili.

Ambwene Mwasongwe, mmoja wa wanamuziki wa injili nchini mwenye mashabiki lukuki, anasema kwa sasa mazingira ya soko la muziki huo ni mazuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma kidogo.

“Soko la muziki wa injili kwa sasa haliko vizuri na sababu kubwa ni wasambazaji kutokana na kuchagua kazi ili wafanye biashara. Waimbaji wengi wamekuwa wakikutana na hali ngumu  katika kufanya kazi,” anasema Mwasongwe.

Hata hivyo, anasema kuwa muziki wa injili bado utaendelea kuwa huduma ya kumtumikia Mungu hivyo kamwe haitabadilika.

“Lakini, bado lengo la muziki wa injili lipo pale pale nalo ni kumtumikia na kumtukuza Mungu hivyo, tutaendelea japo mazingira siyo mazuri,” anaongeza.

Naye, mwandaji wa muziki wa injili, Smart Bilionea Baraka anakiri soko la muziki huo limeporomoka kwa kasi.

“Siyo tu kwa waimbaji wanaochipukia, soko ni gumu sana kwa waimbaji wote, muziki wa injili umeporomoka sokoni na hali ni mbaya. Naweza kusema muziki huu umeporomoka kwa asilimia 75,” anasema.

Anaongeza kuwa imefika hatua hata waimbaji wengi wakubwa kazi zao mpya zilizoandaliwa hazisikiki na kwamba, zilizobaki kusikika mtaani ni zile za zamani, ambazo zilipata umaarufu.

“Waimbaji wengi wakubwa wanazo albamu mpya, lakini ukiuliza watu kama wanazifahamu jibu ni hapana, zaidi anakutajia nyimbo za zamani ambazo zilitamba.

Katibu wa Chama cha Muziki wa Injili Tanzania, Stella Joel anakiri hali ya soko la muziki huo umeshuka na hata wasanii wakubwa hawapati dili za matamasha ama kufanya ziara za kimuziki.

Sababu za kuporomoka

Produza Baraka anasema zipo sababu nyingi zilizofanya muziki wa injili kuporomoka kwa kasi ikiwamo kukua kwa matumizi ya teknolojia.

Anasema utandawazi, umewafanya watu wengi kuwa na uwezo wa kupakua nyimbo za Injili za waimbaji tofauti duniani na hivyo, kuwa na uwezo wa kuchuja kiwango cha kazi.

“Siku ukitaka wimbo wa nchi yoyote ile unaupata tena kwa aina na kiwango utakavyo, hii pia imesababisha muziki wetu kuporomoka,” anasema.

Anaitaja sababu nyingine kuwa tabia ya baadhi ya waimbaji kuiga muziki kutoka nje ikiwa ni pamoja na mashairi na hata mapigo.

“Ukiiga muziki wa Afrika Kusini wakati mtu akiutaka muziki huo anaupata mtandaoni, sasa unadhani utabaki sokoni? Ubunifu pia unasababisha soko kupotea,” anasema.

Stella anasema ni lazima kurejea kwenye utamaduni wa Kitanzania, ili badala ya kuiga muziki kutoka nje ni muhimu kwa wale wa nje kuiga wasanii wa Tanzania.

“Tukiimba kwa uhalisia wetu tunaweza kupenya nje kama wenzetu wanavyouza kazi zao hapa kwetu, Nigeria walistuka wameamua kurejea kwenye utamaduni wao,” anaeleza na kuongeza;

“Tukiendelea kuigaiga mara Afrika Kusini, mara Kongo nani atalipa kiingilio kuja kwenye tamasha lako?

“Ninaimani watu watalipa Dola ili waone tamaduni za Kigogo, Kihehe, Kingoni na hapa ni lazima turudi kwenye vionjo vya asili tu.”

Serikali yabebeshwa mzigo

Baraka anaibebesha lawama Serikali kuwa haina sera nzuri ya kuwalinda wanamuziki wa ndani, jambo linalosababisha kukwamisha jitihada zao.

“Nchi yetu haithamini muziki wala wanamuziki, sidhani kama imewahi kufanya tathmini kujua muziki umeingiza kiasi gani na una faida gani, lakini nataka nikuambie kungekuwa na sera nzuri hakuna muziki ambao ungeporomoka,” anasema.

Anasema imefika hatua wasambazaji ndio ambao, wanawaongoza wenye kazi zao na kwa sababu za ugumu wa maisha, wanamuziki inabidi wawafuate.

Anabainisha kuwa kama sera ya muziki wa Tanzania ingeandaa mazingira mazuri ya muziki, waimbaji wa muziki wa injili waliowahi kuvuma sana wangekuwa matajiri wakubwa wakisaidia serikali kuondokana na mzigo wa tatizo la ajira.

Nini kifanyike

Baraka anasema serikali ni lazima ikubali kuwekeza kwenye muziki wa Tanzania ikiwamo injili.

Rais wa Tanzania Music Foundation (Tamufo), Dk. Donald Kisanga, anasema kinachoweza kurejesha hadhi ya muziki wa kitanzania ni sheria itakayowabana wezi wa kazi za muziki, kukamatwa kwa makosa ya jinai.

“Sheria ikiruhusu polisi kumkamata mwizi wa kazi ya muziki wa msanii, akafikishwa kituoni kwa kosa la jinai itapunguza wizi unaowaumiza waimbaji na wasanii,” anasema.

Anashauri kuwa lazima kurejea kwenye msingi halisi wa muziki wa Injili ili kazi ya mungu iendelee kufanyika.

“Wenzetu Afrika Kusini wana msimamo na utamaduni wao, turejee nasi kwenye utamaduni wetu naamini tutafanya kazi nzuri,” anasema.

Mwasongwe anashauri waimbaji wa muziki wa Injili kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa badala ya kufanya kazi wakitaka kutoka haraka wakati hazina kiwango.

Muimbaji wa nyimbo za injili, Elizabeth Ngaiza anasema lazima Serikali iingilie kati kuokoa muziki wa kitanzania.

“Sheria zitumike, muziki ulindwe naamini tusingelia na ugumu wa maisha kama kazi za wasanii zingekuwa zinalipa,” anasema.