Kathy Ireland : Mrembo wa miaka 50 anayetakatishwa na fedha

Muktasari:

  • Matangazo ya kibiashara ambayo yanatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa utajiri wa Kathy ni pamoja na yale ya sabuni, nguo, marashi, majarida na mengineyo.

CALIFORNIA, MAREKANI

ANA umri wa miaka 50, lakini bado yuko bomba na anatamba katika fani ya mitindo huku hivi karibuni tu akitajwa na mtandao wa businessinsider kuwa ni mwanamitindo namba moja duniani kwa utajiri.

Jina lake ni Kathleen Marie Ireland, lakini katika fani na hata nje ya fani anafahamika zaidi kwa jina la Kathy Ireland.

Kathy alizaliwa Machi 20, 1963, California, Marekani na kwa mujibu wa mtandao huo, toleo la Agosti mwaka jana, utajiri wa mwanamama huyo unafikia Dola 350 milioni.

Ni utajiri ambao unachangiwa na mambo mbalimbali ambayo amekuwa akiyafanya mrembo huyo mkongwe ambaye kipaji chake kiligundulika alipokuwa na umri wa miaka 17.

Amekuwa akitokea katika vipindi zaidi ya 30 kwenye televisheni, ameshiriki filamu mbalimbali pamoja na matangazo ya kibiashara.

Matangazo ya kibiashara ambayo yanatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa utajiri wa Kathy ni pamoja na yale ya sabuni, nguo, marashi, majarida na mengineyo.

Katika majarida ambayo yamechangia kumpa Kathy utajiri ni yale majarida maarufu ambayo ameyapamba kama Vogue na Cosmopolitan.

Cathy pia anajihusisha na ubunifu wa mavazi ya maharusi pamoja na vito mbalimbali vya thamani.

Nje ya hayo, Kathy tayari ametunga vitabu sita kikiwamo kile cha Powerful Inspiration: Eight Lessons That Will Change Your Life, ambacho kilitamba katika mauzo.

Vitabu vingine ni pamoja na Real Solutions For Busy Moms, 52 God Inspired Messages From My Heart, Mona’s Favorite Words, What Do Mommies Do? na An Angel Called Hope.

Kathy pia ametengeneza na kuuza mkanda wa video ambao unahusu mazoezi ya viungo unaoitwa Kathy Ireland’s Total Fitness Workout.

Biashara za Kathy kupitia Kathy Ireland Worldwide zinakwenda vizuri na anajivunia ikielezwa kuwa amefanya mauzo ya Dola 2 bilioni yaliyotokana na bidhaa mbalimbali katika nchi 50.

Kwa utajiri huo haishangazi kwa Kathy kumiliki jumba la kifahari lililopo Montecito, California lililopo katika eneo la ekari 2.5.

Kathy amelibatiza jumba hilo jina la Santa Barbara Oasis, ni jumba ambalo pia linatoa huduma mbalimbali ikiwamo sherehe za harusi na matukio mengine makubwa.

Mbali na jumba hilo, Kathy pia anamiliki jumba jingine katika Kisiwa cha Hawaii, jumba ambalo awali lilikuwa mali ya mwanamuziki John Travolta na mkewe Kelly Preston kabla ya Kathy kulinunua mwaka 2004.

Unaweza kushangaa ni kwa nini Kathy ambaye ana miaka 50 sasa lakini bado ameshika namba moja mbele ya wanamitindo wengine kama kina Natalia Vodianova, Kate Moss, Heidi Klum, Cindy Crawford, Tyra Banks.

Hao ni wanamitindo maarufu ambao wako katika 20 bora kwa utajiri duniani, lakini amewaacha mbali kiumri kwa tofauti ya kati ya miaka 10 hadi 20.

Mambo ambayo yanatajwa kuwa yamesaidia kumbeba Kathy hadi kufikia hatua aliyofikia sasa na hata kuendelea kutamba licha ya umri wake mkubwa ni ujasiri katika kazi yake pamoja na uadilifu.

Pamoja na kuitambua dini ya kikristo na kuzaliwa katika mazingira ambayo dini hiyo imeshamiri, Kathy alianza kusoma Biblia akiwa na miaka 18 na hapo akajifunza mambo mengi likiwamo suala la ujasiri na umakini.

Mwenyewe anasema kwamba Biblia pia ilimfanya abadili msimamo wake kuhusu suala la utoaji mimba, awali aliliona jambo hilo kuwa ni sahihi lakini sasa anaamini utoaji mimba ni kudhulumu kiumbe ambacho kimepewa uhai.

Kathy pia amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii kama afya za wajawazito na watoto, Ukimwi na mikakati ya kuwawezesha wanawake.

Tofauti na wanamitindo wengine, Kathy si mwenye kupenda matanuzi na kupigwa picha za mara kwa mara akiwa katika mazingira ya starehe pengine ni kutokana na umri wake mkubwa au kutofurahia tabia hiyo.

Kathy ambaye ana Shahada ya Sanaa ya heshima aliyopewa na Chuo Kikuu cha Intercontinental cha Marekani ni mama wa watoto watatu, Chloe, Erik na Lily.