Mastaa wa Bongo Movie wakacha tamasha la Ziff

Muktasari:

  • Hii ni aibu kubwa! Kwani waigizaji, watayarishaji filamu, waongozaji na waandishi wa miswada ya filamu kutoka nchi tofauti duniani wametawala jukwaa la Ziff kwa mwaka huu, lakini wazawa hawajaonekana.

WAKATI Tamasha la Filamu la Kitamataifa (Ziff) likiingia siku ya sita, hakuna mwigizaji yeyote wa filamu za Kibongo maarufu Bongo Movie, ambaye ameonekana katika viunga vya Mji Mkongwe kisiwani Zanzibar.

Hii ni aibu kubwa! Kwani waigizaji, watayarishaji filamu, waongozaji na waandishi wa miswada ya filamu kutoka nchi tofauti duniani wametawala jukwaa la Ziff kwa mwaka huu, lakini wazawa hawajaonekana.

Inatia shaka kidogo kuhusu uelewa na umuhimu wa tamasha hili kwa wasanii wetu, ambao walistahili kuwepo kwa wingi ili kubadilishana ujuzi n ahata kupata mawazo mapya na kufahamiana na waigizaji wa nje.

Hekaheka za tamasha hili ni kubwa na kila kona kwa mastaa kutoka kila kona ya dunia, ambapo baadhi walihoji walipo waigizaji wazawa bila mafanikio.

Waigizaji wengi wa kimataifa walijipanga kukutana na wasanii wa Tanzania kwa lengo la kufahamiana na wanafamilia wa filamu na kujenga uhusiano wa kikazi.

Hata hivyo, waandaji wamekuwa kwenye wakati mgumu pale walipotakiwa kueleza walipo ama kuwakutanisha wasanii wa nje na wa hapa nyumbani.

Mkurugenzi wa Tamasha la Ziff, Profesa Martin Mhando, akizungumzia maendeleo ya tamasha hilo alisema ni aibu kubwa kwa wasanii wazawa kuingia mitini huku wageni wakihaha kuwatafuta kwa lengo la kubadilishana mawazo na kutafuta namna ya kufanya kazi pamoja.

“Kwa sasa filamu nyingi zinaonyeshwa hapa na waongozaji wengi wanakuja, filamu zetu za Bongo Movie pia zinaonyeshwa kwa kasi sana na hilo pekee linatosha kuwafanya kujisogeza karibu.

“Filamu za Kibongo zimeanza kufikia kiwango cha kimataifa na Ziff ni shule ya uhakika ya kuendelea kuwainua,” alisema.

Alisema umefika wakati kwa waigizaji wa Bongo kuwazia zaidi soka la kimataifa na kuacha kufikiria kutegemea Sh20 milioni za wasambazaji waliopo nchini na kwamba, kwa kushiriki tamasha hilo kutawasaidia kufungua milango na kufahamiana na wasambazaji wakubwa wa kimataida.

“Hili tamasha lina umuhimu mkubwa, kwa hawa waliopo nje wanajitahidi sana kupata nafasi ya kukutana na wenzao, lakini Watanzania wameshindwa kutambua hilo. Hapa kuna fursa ya kujifunza na kupanua masoko kimataifa. Waache kutegemea Sh 20 milioni za Wahindi hizo haziwezi kuwainua na kuwafikisha kimataifa,” alisema.

Hata hivyo, mmoja wa waigizaji ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kuwa uwezo umekuwa moja ya kikwazo kwa wasanii wa Kitanzania kushiriki kwenye tamasha hilo.

Alisema hali ya maisha na biashara ya filamu nchini imekuwa ngumu hivyo, ni wachache sana ndio wenye uwezo wa kumudu gharama za maisha ya visiwani humo.

“Unajua tunasubiri tupate muda mwafaka kwa sisi kuhudhuria, ndio maana tunasubiri kuwezeshwa kutoka kwao, tukisema tutumie gharama zetu wengi. Fikiria gharama za hoteli, chakula, usafiri inakuwaje hapo na Zenji kila kitu kipo juu na ule ni mji wa kitalii,” alisema mwigizaji huyo.Hata hivyo, imeelezwa kuwa wasanii wengine wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuhudhuria siku ya ufungaji wa tamasha hilo, ambapo utoaji wa tuzo hufanyika na hapo waandaji hubeba gharama za kuwaalika washindi.

Wasanii wa muziki watamba

Wasanii wa muziki wameonekana kivutio kikubwa kwenye tamasha hilo kutokana na kuhudhuria kwa wingi ikilinganishwa na wenzao wa filamu.

Baadhi ya wasanii wamekuwa wakionekana visiwani Zanzibar ilimradi kuona namna tamasha hilo linavyokwenda, huku baadhi wakitoa burudani jukwaani na kulifanya kunoga zaidi.

Msanii mwenyeji Baby J ameonekana kivutio kwa kushiriki kikamilifu kwenye tamasha hilo, licha ya kufanya onyesho pia siku ya uzinduzi wa tamasha akimuenzi Bi Kidude.

Vikundi kadhaa vya muziki vimekuwa vikitoa burudani katika tamasha hilo kutoka Bara na visiwani.

Usiku wa kuamkia jana ulikuwa ni usiku wa Muziki wa Reggae katika Ukumbi wa Mambo Club, ambapo mastaa wa muziki huo Afrika akiwemo Ras Katongo, Mash Marley/Ras Koko, Dabo kutoka Dar es Salaam, Black Lion kutoka Marekani na The Island Band walitumbuiza.

Usiku wa kuamkia leo Ziff imemkumbuka mkongwe wa Taarab visiwani ya Zanzibar, Bi Kidude, burudani iliongozwa na DJ mwanamke na wasanii ambao walicheza na visu (Samira Bin Sharifu) kutoka London, Uingereza ambaye alifanya onyesho la kimataifa akiambatana na Yasiin Bey (Mos Def).

Leo ndani ya Ukumbi wa Mambo Club utapambwa na burudani ya Usiku wa Sauti Tamu ikiwa na staa kama Galatone, Bayo, TID na Kassim Mganga, na kesho ni usiku wa tuzo ambao utaambatana na burudani ya muziki wa Hip Hop itakayotolewa na Galatone, Bayo, Tid, na Kassim Mganga.