Kuna Diamond halafu Harmonize

Muktasari:

Tunakumbuka ilikuwa muda mfupi baada ya kumaliza kufanya mahojiano ya kina na kinara wa kundi hilo, Diamond Platinumz, tulianza kujiandaa kutimka baada ya kuridhika na kazi nzuri tuliyofanya na staa huyo wa kiimataifa.


SAFARI ya kutembelea makao makuu na studio za Wasafi Classic, inabakia kuwa yenye kumbukumbu ya kipekee kwa timu ya waandishi wa Mwanaspoti iliyotembelea ofisi hizo hivi karibuni.

Tunakumbuka ilikuwa muda mfupi baada ya kumaliza kufanya mahojiano ya kina na kinara wa kundi hilo, Diamond Platinumz, tulianza kujiandaa kutimka baada ya kuridhika na kazi nzuri tuliyofanya na staa huyo wa kiimataifa.

Lakini wakati tukianza kujizoazoa tulipokuwa tumekaa, Meneja wa kundi hilo, Babu Tale, alituzuia kuondoka na kutuahidi kuwa tumpe muda mfupi ili aweze kutuletea zawadi. Kila mmoja alipigwa na butwaa ni zawadi gani ambayo Babu Tale alikuwa akitaka kutupatia, ingawa hakuna aliyemhoji mwenzake. Tulitulia tuli.

Wakati tukiendelea kuitafakari zawadi gani ambayo Tale amepanga kutupatia, mlango unafunguliwa na kumuona meneja huyo akiwa ameambatana na kichwa kingine kutoka ndani ya kundi hilo la Wasafi ambaye ni msanii Harmonize.

Huku akitabasamu, Tale anafichua kuwa zawadi ambayo alipanga kutupatia ni kumleta msanii huyo, ili tufanye naye mahojiano kama ilivyokuwa kwa Diamond ambaye muda huo tayari alikuwa ameshaondoka kwenye chumba cha mikutano na kuelekea kwenye ofisi yake.

Kama ilivyokuwa awali kwa Diamond, Harmonize anatukaribisha kwa ucheshi na kujitambulisha huku akitusisitiza tuwe huru kumuuliza chochote kinachohusu maisha yake na muziki kiujumla.

 

Kalala standi ya mabasi

Nyuma ya mafanikio ya yeyote huwa kuna nyakati ngumu ambazo kwa namna moja zilichangia kumhamasisha kupambana zaidi na changamoto za kimaisha hadi akaweza kufikia mahala alipo.

Harmonize ni miongoni mwa watu waliopita kwenye milima na mabonde kabla ya kufanikiwa kuikaribia nchi ya ahadi hivi sasa na kuwa mmoja wa mastaa wanaotamba kwenye muziki nchini.

Pamoja na kumiliki vitu vingi vya thamani hivi sasa, Harmonize anafichua safari ya kimuziki kwake ilikuwa ngumu kiasi cha kufikia kulala kituo cha mabasi yaendayo mikoani huku akikutana na misukosuko ambayo hata haikumzuia kufika alipo sasa.

“Nilivyotoka Mtwara kuja Dar es Salaam, nilifikia kwa dada’angu mwaka 2009 na ilipofika mwaka 2011 nikaanza mambo ya muziki. Kwa hiyo nilipoanza muziki, kama unavyofahamu kuwa mambo ya muziki yanataka muda sana,” anasema.

“Kwa hiyo kuna wakati asubuhi nikawa natoka nakwenda kuzunguka kwenye studio narudi usiku namgongea dada, halafu sasa dada alikuwa akiishi na mume, yaani nilikuwa naishi kwa shemeji. Hivyo wakawa wanaona kama nawazingua. Hata mi’ mwenyewe nikawa najishtukia maana unakwenda kuzurura halafu unarudi usiku upikiwe chakula ule, haufanyi kazi yoyote halafu ukiangalia maisha yenyewe magumu.”

 

Shemeji ampa makavu

“Lile suala shemeji alishindwa kukubaliana nalo, ikabidi amwambie dada yangu. Kama dada sawa damu nzito kuliko maji, lakini wakati mwingine naye pia alikuwa anaumia kwa sababu haiwezekani huishi tu kama mzigo, hata ningekuwa mimi nisingeweza.” anasema Harmonize.

Msanii huyo anasema kuwa hiyo ilikuwa sababu tosha ya yeye kuondoka kwa dada yake na kuingia mtaani ambako alikutana na changamoto ya kulala vituoni.

“Kwa hiyo wakaniambia bwana kama umeamua kufanya muziki anza kujitegemea kwa sababu sisi hatuwezi kukaa na wewe kwa sababu haiwezekani kukaa na mtu ambaye hatusaidii, hafanyi chochote. Unakula tu, unavaa na unalala bure,” alisema akiwakariri.

Baada ya kujishtukia, aliamua kuanza kujitegema. Anakiri kuna wakati maisha ni kama yalielekea kumshinda, lakini akaamua kukomaa kwa sababu siku zote katika maisha yake huwa hakubali kukata tamaa kirahisi.

“Ndipo nikaanza kujichanganya na vijana wanaolala kwenye vituo vya mabasi na kupiga mbonji kama chokoraa, yaani ilikuwa kawaida kwangu kulala nje, katika mazingira kama hayo unadhani utalala wapi, gesti?” Anahoji.

 

Muziki wampeleka Mbezi Beach

Waliosema kuwa baada ya dhiki faraja, hawakukosea. Huwezi amini kwa sasa staa huyo wa Aiyola, anaishi kwa wanene, mitaa ya Mbezi Beach, jambo ambalo hata yeye mwenyewe anajishangaa kuishi huko.

Harmonize anasema kilichompeleka Mbezi ni muziki ambapo kwa sasa anaishi katika nyumba nzuri tofauti na siku za nyuma wakati anaanza kupambana.

“Kwa sasa naishi Mbezi Beach, nipo na mama yangu. Maisha ya zamani na sasa hivi ni tofauti kwa sababu zamani nilikuwa najitegemea, ila sasa hivi nategemewa kwa sababu nakaa na mama yangu pamoja na dada yangu,” anasema.

“Hivyo naishi kama baba mwenye nyumba kwani nategemewa na maisha lazima yawe tofauti. Hiyo nyumba nimepanga.

Mama yangu alikuwa anaishi Mtwara, ila wakati mwingine ukipata hata kidogo ni vizuri ukila na mama yako unapata faraja kwa sababu unaweza kula chipsi na kuku halafu unaanza kujiuliza mama hivi kala nini. Lakini ukikaa naye hata mkila wali au ugali na maharage unakuwa una amani ile ya moyo kwamba nimekula na mama yangu, yupo vizuri na tumeshiba.”

Hapo Mbezi Beach Harmonize amepanga, ila anajenga mjengo wa hatari, unadhani mjengo wake huo una thamani ya kiasi gani na unafahamu anamiliki gari la watu wenye noti? Gari gani hilo na unajua ilikuwaje hata akafika WCB? Ungana naye keshokutwa Jumatatu.