Huyu Wema atalia au atacheka pale Chadema?

Msanii wa filamu, Wema Sepetu akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni mama yake mzazi Mariam. Picha na Omary Fungo

Muktasari:

Asema anakwenda upinzani kupigania demokrasia huku akiituhumu CCM kutomlipa fedha zake za kampeni

JANA  Ijumaa mrembo Wema Sepetu alitangaza kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia Chadema.

Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006 alitangaza maamuzi hayo baada ya juzi  kuonekana akimsindikiza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mahakamani katika kesi inayomkabili.

Wengi hawakuamini kama waliyekuwa wakimuona katika benchi pembeni ya mwanasiasa huyo ni Wema.

KItendo chake cha kuonyesha  alama ya  vidole viwili  inayotumiwa kama utambulisho wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, ilionyesha kina kitu.  Na ilishangaza watu kwa kuwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Taifa wa mwaka juzi 2015, Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006 alikuwa bega kwa bega na CCM na kumnadi mgombea wa chama hicho, ambaye kwa sasa ni Rais wa Tanzania, John Magufuli. Wema alikuwa na jopo lake lililofahamika zaidi kama Mama Ongea na Mwanao ikihamasisha vijana kuichagua CCM.  Ushindi wa kishindo cha CCM kwa wagombea wake ulikuwa na  mchango  mkubwa wa kisura huyo kupitia kampeni zake, kwani nyuma yake alikuwa na kundi la wapiga kura kibao walimwaga kura chama tawala.

Lakini Jumatano wiki hii wakati Mwanasheria Mkuu wa Chadema alipojitokeza kumtetea msanii huyo, ilionekana ni jukumu lake la kawaida la kiwakili, kumbe haikuwa hivyo tu,  suala hilo lilikwenda mbali zaidi.

Wema alijitokeza mahakamani kumsindikiza Mbowe katika kesi ambayo mbunge huyo wa Hai amefungua dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro na sasa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika tukio hilo Wema alikuwa Mahakama Kuu huku akionekana mwenye furaha ambapo alikaa katikati ya Freeman Mbowe na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na wakati mwingi alikuwa akionyesha ishara ya vidole viwili, ambayo hufanywa na wafuasi wa chama hicho kila kamera za wanahabari zilivyommulika. Picha za Wema zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na muda mfupi baadaye ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene alituma ujumbe unaosema; “Chama kupitia Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe, baada ya kesi ya kikatiba kitawakaribisha wanachama wapya akiwemo Wema Sepetu.”

Ndipo jana mwanadada huyo akatangaza kujiunga rasmi chama hicho akisema ni kwa hiari yake tena bila kupewa hata senti tano, lakini Mwanaspoti leo linakuletea faida na hasara za Wema kujiunga Chadema na madhara ya kuihama CCM katika kipindi hiki ambacho anakabiliwa na tuhuma mbalimbali mahakamani.

Ni fimbo kwa Chadema

Kumkaribisha Wema kundini huenda ikawa na faida kwa Chadema na Ukawa kwani watavuna wanachama wengi vijana kwa ushawishi wa mrembo huyo ambaye ana mashabiki wengi. Kama alivyowahi kufanya Zitto Kabwe kipindi cha nyuma akiwa Chadema kwa kuwahamasisha vijana wengi wa vyuo vikuu kujiunga kwenye siasa, Chadema huenda ikanufaika na mtaji huo wa Wema. Ingawa bado ukweli unabaki palepale kwamba Chadema ni kubwa kuliko Wema na binti huyo anaihitaji zaidi taasisi hiyo kufikia malengo yake.

Wema amekuwa kada wa CCM kwa kipindi kirefu licha ya kwamba makali yake yalionekana mwaka 2015 alipokwenda kugombea Viti Maalumu Singida na baadaye kushindwa. Taarifa zinaeleza kuwa baada ya kukosa nafasi hiyo, Wema alikuwa radhi kukihama chama na kwenda Chadema ili kugombea viti maalumu huko, lakini akapata mradi wa Mama Ongea na Mwanao uliomfanya aendelee kubaki chama tawala.

Kuonekana msaliti

Yeyote anayeondoka katikati ya kundi ambalo hukaa pamoja na kupanga mipango ya namna ya kumwangamiza adui, huonekana msaliti. Hivyo ndivyo Wema anavyochukuliwa kwa sasa na kutokana na kuhama katika kipindi anachokabiliwa na tuhuma mbalimbali, moja kwa moja kundi lake la mwanzo litasimamia tuhuma hizo kuzidi kumkandamiza.

Amechagua panapomfaa

Kuwa na tuhuma hakumfanyi yeye kupoteza haki zake za kikatiba kama raia wa Tanzania, hii ni katika mambo mengi ikiwemo kujiunga na chama chochote cha siasa na vilevile Chadema kama chama cha siasa kina haki ya kupokea mwanachama yeyote ili mradi afuate taratibu  za chama.

Ikumbukwe kuwa chama chochote ili kiwe na nguvu  yahitaji iwe na wanachama wa kutosha hivyo ni wajibu wao kuendelea kuwapokea wanachama bila kujali kabila, dini, rangi na jinsia. Huenda staa huyu ameona kuna haja kwake kwa sasa kujiunga na chama hicho ili kutimiza lile lengo lake la muda mrefu kuwa mwanasiasa hai.

Itamjenga kisiasa

Kwa kuwa kwa muda mrefu amekuwa ni mwanachama wa kuingia katika harakati kipindi cha kampeni pekee, kuwa kwake katika chama hicho cha siasa kutamfanya apate nafasi ya kushiriki mambo mengi katika siasa tofauti na hapo awali. Lakini pia kufika kwake Chadema kutamfanya aanze upya kuzisoma kanuni za chama na ilani zake, hivyo kumjenga zaidi kiakili na kisiasa kiasi cha kumwezesha kujua mengi kuhusu nchi yake na kujipangia maamuzi nini cha kufanya kwa sasa.

Itamtengeneza kimaadili

Mrembo huyu ambaye ni binti wa Balozi, Isaack Sepetu amekulia katika familia ya masuala ya siasa na maadili, kutoka kwake nje ya mstari kulimfanya azungumziwe na wengi, lakini kuanza kujihusisha tena na siasa ni mwanga mzuri kwake kumfanya atulie kimaadili.

Wengi wanafahamu Wema ni mtu wa aina gani, uwepo wake kwenye siasa huenda ukamtengeneza kuwa mtu wa tofauti kulinganisha na ilipokuwa hapo mwanzo.

Huenda akabadilika sana kwani lazima kiitikadi Chadema watampa elimu ya nini anapaswa kufanya na kipi hastahili ili kuwepo katika nafasi nzuri kisiasa na kujenga imani kwa maadui zake na wale wanamnyooshea vidole, vilevile kuishawishi Chadema kwamba hawakufanya uamuzi dhaifu.

Kuachana na makundi yasiyofaa

Wakati akiwa ameachana na aliyekuwa meneja wake kutokana na makundi mabaya, Wema alionekana kama kukosa mwelekeo.

Alikuwa hana shughuli maalumu ambayo alionekana kuifanya kwa kipindi fulani, na hiyo imeelezwa kwamba huenda ndiyo sababu ya kuonekana na watu ambao hawakuwa wakimwongoza vizuri. Uwepo wake kwa mara nyingine katika masuala ya kisiasa iwapo atapewa shughuli ya kufanya na chama, itamwezesha kuwa katika mikono salama kwa kuwa muda mwingi atakuwa na kazi ya kufanya kiasi cha kuachana na masuala yasiyo na tija.

Kwanini amekuwa maarufu?

Alipotawazwa kuwa Miss Tanzania 2006, Wema alipendwa na wengi. Tofauti na warembo wengine yeye alikwenda mbali zaidi kiasi cha kuingia katika fani ya uigizaji pale alipoigiza katika filamu ya Point Of No Return na Steven Kanumba mwaka 2007.

Tangu hapo Wema alianza kuwapa umaarufu wale wote aliojihusisha nao kwa namna moja ama nyingine katika kazi kiasi cha kumfanya Kanumba kuwa maarufu zaidi hasa walipoingia katika masuala ya uhusiano wa kimapenzi. Baada ya hapo aliigiza katika filamu za Red Valentine, White Maria, Tafrani, Sakata, Crayz Tenant, Diary, Lerato, Dj Benny, Madam, Basilisa na nyinginezo. Akiwa na shoga yake Snura aliwahi kujaribu kuingia katika muziki kwa kutoa wimbo wa “Shoga Yake Mama” ambao haukufanya vizuri katika tasnia hiyo. Baadaye aliingia katika uhusiano wa kimapenzi na mwimbaji Diamond Platnumz enzi hizo nyota huyo wa muziki Afrika kwa sasa hakuwa na umaarufu na wala hakuwa amekua kimuziki.

Mwaka 2012 wawili hao walichumbiana na uhusiano ukaanza kupaa kwa kasi kiasi cha kumfanya Diamond apendwe zaidi kama ilivyokuwa kwa Wema na baadaye wawili hao waliachana na Diamond kuwa na Penny.

Miaka miwili baadaye uhusiano wao ulirudi kwa kasi na safari hii Diamond alitangaza kumuoa lakini uhusiano huo ukavunjika kwa mara nyingine na Zari akaingia kati. Licha ya kuwa katika uhusiano na mshindi wa Big Brother The Chase, Idriss Sultan baadaye, Wema alishafanya vipindi vingi vya televisheni, kuuza bidhaa mbalimbali kupitia kampuni yake ya Endless Fame.

Mtoto huyo wa mwisho katika familia ya Balozi Sepetu yenye watoto wanne wa kike, alizaliwa Septemba 28,  1988. Je atafanikiwa kisiasa ndani ya Chadema?