Filamu zinavyowatesa wasanii uraiani

Muktasari:

Kwa upande wa fani ya filamu mara nyingi hilo linatokana na kuuvaa vyema uhusika wa nafasi anayoigiza katika kazi japokuwa kushindwa kuuvaa uhusika inavyotakiwa pia inaweza kumshusha msanii husika.

KATIKA tasnia ya uigizaji kuna mambo mbalimbali unaweza kukutana nayo kwenye jamii, iwe kwa uzuri au kwa ubaya. Japokuwa vinaweza kumpatia mtu umaarufu ingawa mara nyingi hutegemea na jinsi msanii anavyojiweka ama anavyojihusisha na sanaa yake.

Kwa upande wa fani ya filamu mara nyingi hilo linatokana na kuuvaa vyema uhusika wa nafasi anayoigiza katika kazi japokuwa kushindwa kuuvaa uhusika inavyotakiwa pia inaweza kumshusha msanii husika.

Yote hayo, inategemea na mashabiki wanakupokeaje katika sanaa na ili upate kuwateka itakulazimu kuwa mbunifu na kujua nini wanahitaji ili kuburudika na hawataki mambo ambayo kuchukizwa japo si rahisi kuwaridhisha wote.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha wasanii wamekuwa wakipata adha mbalimbali kutokana na uhusika wanaouvaa katika baadhi ya filamu zao hasa zile zinazokuwa za matukio ya ajabu katika jamii kama uchawi, uhuni, utapeli, dawa za kulevya, ukabaji au unyanyasaji wa watoto.

Kiuhalisia hufanya hivyo ili kufikisha ujumbe kwa jamii, lakini matokeo yake jamii hiyo hiyo huwachukulia kama ni tabia za maisha yao halisi hivyo, wakati mwingine huwahukumu.

MWANASPOTI ilifanya mahojiano na baadhi ya wasanii waliopata adha za aina hiyo na kuweka wazi jinsi filamu zinavyowapa maisha ya shida uraiani.

DUDE

Kulwa Kikumba .k.a Dude, ni mmoja wa wasanii anayekumbana na adha hiyo kiasi cha kufikia hatua ya kuadhibiwa na jamii inayomzunguka kutokana na kuigiza filamu za kitapeli hivyo, kuambulia kipigo kutoka kwa wananchi.

Alishakutana na adha hiyo kwa nashabiki kwenye mikoa ya Iringa na baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam.

BI MWENDA

Bi Mwenda ambaye jina lake halisi ni Fatuma Makongoro, hupenda kuigiza kama mchawi au mtu katili. Mwana mama huyu alisema kuna wakati wananchi walitaka kumchoma moto wakiamini kweli ni mshirikina.

Mbali na hilo, aliwahi kuzomewa katika mikoa kadhaa huku baadhi ya watu wakijitokeza na kumkanya kuachana na tabia hiyo, hali ambayo ilienea hadi kwa baadhi ya wasanii wenzake wakiamini ni mchawi.

Licha ya kufanikiwa kuuvaa uhusika na kujipatia umaarufu alichoambulia ni kutengwa na jamii wakati katika maisha yake halisi hayuko hivyo.

CHARLES MAGARI

Maarufu kama Mzee Magari, yeye anapenda kuigiza kama mtu mwenye roho mbaya sambamba na msanii mwenzake Ally Fungafunga maarufu Jengua, ambaye pia hupenda kuigiza kama mtu mwenye sifa za Mzee Magari.

Mzee Magari alisema alitengenezewa njama nusura atekwe kwa lengo la kwenda kumlipizia, lakini kwa bahati nzuri aliokolewa na msanii mwenzake.

RIYAMA, SHAMSA FORD

Kwa upande wa Riyama na Shamsa wameonja adha hiyo baada ya kutafasiriwa na jamii kama wanawake wa uswahilini wanaopenda ugomvi, vijembe na kusutana na wenzao kila wakati ingawa kwenye maisha yao ya kawaida tabia zao ni tofauti na wanavyoigiza.

AUNTY, LULU, JOHARI

Ni wasanii wanaoweza kuigiza uhusika ipasavyo na wao waliwahi kupatwa na adha hiyo kwa kitendo cha kuigiza uhuni na uchangudoa.

Wamecheza uhusika wa aina hiyo katika filamu nyingi na wamekuwa wakitafsiriwa tofauti kiasi cha kuwakosesha raha. Kinachowakera hasa ni pale wanapokuwa kwenye mikusanyiko ya watu wanaume wakware wanaanza kuwataka kimapenzi kwa makubaliano ya pesa.

IRENE UWOYA

Naye amekuwa akipata shida kwenye jamii hasa wanawake ambao, wanaamini kuwa Irene ni mwizi wa wanaume za watu kwani, mara kadhaa amekuwa akiigiza hivyo.

RAY NA HEMED “PHD”

Wasanii hawa wanapenda kuigiza kama wanaume wenye lugha nzuri za kuwavutia wanawake wawakubali kimapenzi. Wamekuwa wakifanikiwa kwa hilo lakini wamekuwa wakiwaingiza kwenye matatizo mara tu wanapokuwa kwenye mahusiano hayo.

Hilo limekuwa tatizo kwao kwani wanapowahitaji wanawake wamekuwa wakiambulia matusi na kukataliwa.

Wenyewe wanasema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa filamu nyingi walizocheza walivaa uhusika wa aina hiyo na kufanikiwa kuwasilisha ujumbe sahihi hivyo, jamii kuamini kuwa tabia hizo ndiyo sehemu ya maisha yao hivyo, kuogopwa mara kwa mara wanapojitokeza hadharani katika maisha yao halisi.