Diamond, Masanja wajanja wa mjini

Muktasari:

Bodi hiyo iliendesha warsha hiyo ya siku mbili katika Jiji la Mwanza na waliohudhuria walipata darasa la kutosha kutoka kwa wawezeshaji mahiri wa mambo ya filamu kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) na Dodoma (UDOM).

WIKI iliyopita Bodi ya Ukaguzi na Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania (TFBC) iliendesha warsha kwa wasanii wa filamu jijini Mwanza ambapo, mambo makubwa yaliyofichuka.

Bodi hiyo iliendesha warsha hiyo ya siku mbili katika Jiji la Mwanza na waliohudhuria walipata darasa la kutosha kutoka kwa wawezeshaji mahiri wa mambo ya filamu kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) na Dodoma (UDOM).

Katibu Mtendaji wa Bodi, Joyce Fissoo amesema serikali imejipanga kujenga weledi kwa wadau wa filamu kwani, wamekuwa wakikutana na sinema zenye matatizo mengi na baada utafiti wameamua kuanzisha programu ya mafunzo.

Katika warsha hiyo wasanii wa filamu walifunuliwa mengi, ikiwa kuonyesha namna gani wanavyoshindwa kutumia ukubwa wa majina yao kupiga fedha za matangazo, huku Diamond na Masanja Mkandamizaji wakitajwa kama wasanii pekee wajanja nchini wakitengeneza fedha ndefu.

Mada ya namna wasanii wanavyopishana na fedha kwa kushindwa kutumia vipaji vyao, iliwasilishwa na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungy.

 

MATUMIZI MABAYA

Mungy alisema wasanii wengi wameshindwa kutumia mitandao vema na kujikuta wakipoteza nafasi za biashara, akawataja walioshituka kuwa na kutumia mitandao ya kijamii kuingiza fedha kuwa ni Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ na Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’.

“Wasanii wameshindwa kutumia mitandao ya kijamii katika kujipatia fedha na badala yake wanaitumia kujidhalilisha kwa kuposti picha zisizo na maadili, wangekuwa makini wangetengeneza fedha ndefu sana,” alisema Mungy.

Mungy alisema wasanii wana nafasi kubwa ya kujitengenezea fedha kupitia mitandao ya kijamii badala ya kuitumia kulishana vitu visivyo vya maana, kwani hata dunia iliyoendelea wasanii wamekuwa wakipiga fedha kwa njia hiyo.

“Diamond na Masanja ni kati ya wanaojua kutumia mitandao ya kijamii kupiga fedha, wasanii wengine wanapaswa kufuata mkondo huo kwani, njia hii ni rahisi hasa kwa kusambaza kazi kimataifa,” alisema.

 

KISWAHILI MTAJI

Katika warsha hiyo ilielezwa kuwa, Lugha ya Kiswahili ni mtaji mkubwa ambao pengine watengenezaji wa filamu wameshindwa kuitumia kutokana na matumizi ya kuchanganya lugha za kigeni japo si kwa umahiri mkubwa zaidi ya kubabaisha babaisha tu.

Ilielezwa kuwa wasanii wanaotumia Kiswahili vizuri ni; Abdalah Mkumbila ‘Muhogo Mchungu’, Bi. Hindu, King Majuto na Riyama Ally ambao wamekuwa wakikomalia kiswahili na kujitengenezea jina zuri.

Mkurugenzi wa Lugha kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni , Michezo na Sanaa, Hajat Shani Kitogo, ndiye aliyebainisha hilo wakati akiwakilisha mada iliyosema Filamu katika Ukuzaji wa Lugha ya Kiswahili kimataifa ambapo, alisema akiwa Zanzibar katika kongamano la CHAWAKAMA, wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda walidai wamekuwa wakifaulu mitihani yao ya Lugha ya Kiswahili kwa kujibu maswali kwa kutumia sinema zinazoigizwa na King Majuto, Riyama, Bi. Hindu Muhogo Mchungu.

 

KIWANJA CHA STUDIO

Kufuatia mafunzo hayo kufanikiwa mmoja ya wasanii na walimu wakongwe wa ufundishaji tasnia ya filamu, Fumbuki Lubasa alitoa zawadi ya kiwanja cha kujenga studio kubwa ya uzalishaji wa filamu na vipindi.

Kiwanja hicho kipo maeneo ya Nyegezi chenye ukubwa wa mita 50 kwa 40, Mwalimu Lubasa alitoa kiwanja hicho kwa ajili ya hali halisi inayowakumba wasanii wengi nchini kukosa mitaji na sifa za kukopesheka, hivyo kuwataka walitumie eneo hilo ambapo mfuko wa Jamii wa PPF umeahidi kulifanyia kazi kwa ajili ya kuangalia kama inaweza kuwekeza hapo.

 

RAI KWA WASANII

Warsha hiyo iliyofunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Mwalimu Hamis Maulid na kufungwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Marry Tesha Onesmo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella haikuishia patupu tu. Wasanii walipewa rai kupitia mkuu huyo wa wilaya ambaye alifurahishwa na mafanikio ya semina hiyo kwa kusema:

“Niipongeze Bodi ya Filamu kwa kutuletea warsha hii iliyozaa mafanikio makubwa kwa wana Mwanza, ujanja kuwahi sasa watu wa Dar es Salaam wajipange tutafanya makubwa katika filamu, lazima Mwanza iwe nambari moja katika filamu,” alisema Tesha.

Aliwataka wasanii waliopigwa msasa kuwa mfano kwa wengine, lakini kubwa kwa Mwanza kutolala tena bali kuwa mfano wa kuigwa.