DIAMOND: Afanya kufuru, azoa tuzo saba KTMA, sasa asubiri za MTV Africa

Muktasari:

  • Nyota huyo aliyekuwa akiwania tuzo zaidi ya nne sambamba na Lady Jaydee, alimgaragaza mshindani wake baada ya kubeba tuzo zote huku mwanamuziki huyo wa kike akiambulia tuzo mbili za Wimbo Bora wa Zouk Rhumba na Mwimbaji Bora wa Kike Kizazi Kipya ambazo Diamond hakushiriki.

ULIKUWA ni usiku wa Diamond baada ya mwanamuziki huyo anayeng’ara kitaifa na kimataifa kuwapiku wasanii wa muziki wa kizazi kipya kwa kutwaa tuzo saba za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Mlimani City usiku wa kuamkia jana Jumapili.

Nyota huyo aliyekuwa akiwania tuzo zaidi ya nne sambamba na Lady Jaydee, alimgaragaza mshindani wake baada ya kubeba tuzo zote huku mwanamuziki huyo wa kike akiambulia tuzo mbili za Wimbo Bora wa Zouk Rhumba na Mwimbaji Bora wa Kike Kizazi Kipya ambazo Diamond hakushiriki.

Kwa ujumla Diamond alifanikiwa kunyakua tuzo zote saba alizokuwa akiwania; Wimbo Bora wa Mwaka, Wimbo Bora Wa Kushirikiana, Wimbo Bora wa Afro Pop, Video Bora ya Muziki ya Mwaka, Mtumbuizaji Bora wa Kiume, Mtunzi Bora wa Mwaka Kizazi Kipya na Mwimbaji Bora wa Kiume Kizazi Kipya.

Tuzo hizo zimemfanya mwanamuziki huyo kuvunja rekodi ya Bendi ya Mashujaa ambayo mwaka jana ilitwaa tuzo tano. Mara ya mwisho Diamond kutamba katika tuzo hizo ilikuwa mwaka 2012 alipotwaa tuzo tatu za KTMA.

Staa huyo anasema tuzo alizozipata ni chachu kwake na anaamini zitazaa matunda katika tuzo za kimataifa anazowania za MTV Africa maarufu kwa jina la MAMA.

Katika tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa Juni 7, Diamond anawania vipengele viwili, Mwanamuziki Bora wa Kiume na Kolabo Bora kupitia ‘Number One’ (Remix) aliyomshirikisha Davido kutoka Nigeria.

Anasema Watanzania wamethibitisha kwamba yeye anafanya muziki ulio bora hivyo anaamini kwamba ataweza kukubalika pia kimataifa.

“Huu ni utabiri kwangu na kwa Watanzania wote, kitendo cha kunyakua tuzo zote nilizoteuliwa kinanifanya nijiamini zaidi katika tuzo za MAMA ambazo Watanzania wengi walishaanza kukata tamaa kutokana na vigogo niliokaa nao katika vipengele hivyo, ila cha kuamini ni kwamba tunaweza iwapo tutapiga kura za kutosha,” anasema Diamond.

Washindi wa KTMA 2014

Bendi ya muziki wa Taarab ya Jahazi Morden Taarabu iling’ara baada ya kutwaa tuzo nne; Kikundi Bora cha Mwaka cha Taarabu, Mtunzi Bora wa Mwaka Taarabu, Mwimbaji Bora wa Kiume Taarabu (zote zilikwenda kwa Mzee Yusuph) na Wimbo Bora wa Taarabu.

Isha Ramadhani naye kutoka Mashauzi Classic alifanikiwa kupata tuzo mbili ikiwamo ya Mwimbaji Bora wa Kike Taarabu na Mtumbuizaji Bora wa Kike wa Muziki. Fid Q naye aling’ara baada ya kutwaa tuzo mbili ikiwamo ya Mtunzi Bora wa Mwaka Hiphop na Msanii Bora wa Hiphop.

Kundi wa Weusi pia lilipata tuzo mbili ikiwamo ya Wimbo Bora wa Hiphop na Kikundi Bora cha Mwaka cha Kizazi Kipya. Bendi ya Mashujaa ilifanikiwa kupata tuzo ya Wimbo Bora wa Kiswahili Bendi na Bendi ya Mwaka.

Wasanii wengine waliopata tuzo ni pamoja na Wimbo Bora wa R&B (Closer-Vanessa Mdee), Msanii Bora Chipukizi Anayeibukia (Young Killer Msodoki), Mwimbaji Bora wa Kike Bendi (Luiza Mbutu), Mtunzi Bora wa Mwaka Bendi (Christian Bella), Mtayarishaji Bora wa Nyimbo wa Mwaka Bendi (Amarosi), Mtayarishaji Bora wa Muziki wa Mwaka Kizazi Kipya (Man Walter) na Mtayarishaji Bora wa Nyimbo wa Mwaka Taarabu (Enrico).

Washindi wengine ni pamoja na Rapa Bora wa Mwaka wa bendi (Ferguson), Mwimbaji Bora wa Ragga imekwenda (Chibwa), Wimbo Bora wa Afrika Mashariki (Tubonge wa Chameleone), Wimbo Bora wa Reggae (Niwe na Wewe Dabo) na Wimbo Bora Wenye Vionjo vya Asili ya Tanzania (Bora Mchawi wa Dar Bongo Massive).

Tuzo za Nishani zilikwenda kwa Hassan Bitchuka ambaye ni mwanamuziki na Masoud Masoud naye alipewa tuzo ya heshima kwa kazi yake ya utangazaji wa muziki tangu mwaka 1977.

Wasanii waliotangulia mbele za haki walikumbukwa akiwamo Muhidin Gurumo, Langa Kileo, DJ Rankim Ramadhani na mtangazaji, Julius Nyaisanga.

Shoo ilivyokuwa

Shoo ilifunguliwa saa 3:30 usiku na kikundi cha wacheza shoo wa THT. Baadaye jukwaani waliingia Wamasai waliokuwa wameongozana na Mwana FA na kuimba wimbo mmoja wakiisifu nchi ya Tanzania.

Washereheshaji wa shughuli hiyo walikuwa ni Sylivester Mujuni ‘Mpoki’ na Shadee ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wanachekesha watu, huku wakiwaudhi baadhi yao kwa matani ya ukaribu waswahili wanasema (utani ulio karibu na ukweli).

Burudani nyingine iliyotolewa ni pamoja na dansi kutoka katika bendi ya Twanga Pepeta na Extra Bongo, Weusi ambao waliamsha ukumbi na wimbo wao Gere, Vanessa Mdee, Kundi la wanamuziki watano wa kike, Madee aliyeimba Pombe Yangu na kugawa vinywaji kwa wageni waalikwa, Kadja Nito na mpiga tarumbeta maarufu King Maluu, Ommy Dimpoz na Diamond. Shoo ilifungwa saa 8:24 usiku.

Tuzo zilizolalamikiwa

Ingawaje watu wengi walizifurahia tuzo za mwaka huu, katika ukumbi wa Mlimani City wageni waalikwa walikuwa wakiulizana mara kwa mara uhalali wa tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike kwenda kwa mwanamuziki Lady Jaydee.

Hata hivyo bado kulikuwa na sintofahamu kuhusu tuzo nne zilizokwenda kwa Jahazi Modern Taarab ambapo mashabiki wengi walionekana kutofurahia na hata ushangiliaji ulikuwa hafifu, huku wakionekana kuwashangilia Kapteni Temba ambaye hakunyakua tuzo hizo na Mashauzi Classic.