Cheza mbali na Vanesa Mdee

Vanesa Mdee

Muktasari:

Huyo alikuwa ni Vanessa Mdee maarufu kama Vee Money. Hakuna aliyewaza kwa wakati ule kuwa sauti hiyo ya kilio iliashiria kuwa miaka 28 baadaye angekuwa msanii mkubwa nchini. Pengine kwa wakati huo wazazi wake walipenda aje kuwa rubani ama daktari, lakini tayari maisha yamempeleka anapostahili.

JIONI ya Juni 7, 1988, pembezoni mwa Jiji la Arusha ilisikika sauti ya kichanga cha kike ikilia. Ndiyo kwanza kilikuwa kimezaliwa. Hakuna aliyejua kama angekuja kuwa Malkia wa muziki laini wa R &B nchini Tanzania na kutamba Afrika Mashariki na Kati na kutikisa Afrika nzima. Hakuna. Ni ngumu kutabiria fani ya mtu akiwa angali bado ‘ng’aa’.

Huyo alikuwa ni Vanessa Mdee maarufu kama Vee Money. Hakuna aliyewaza kwa wakati ule kuwa sauti hiyo ya kilio iliashiria kuwa miaka 28 baadaye angekuwa msanii mkubwa nchini. Pengine kwa wakati huo wazazi wake walipenda aje kuwa rubani ama daktari, lakini tayari maisha yamempeleka anapostahili.

Bila shaka kwa sasa hapa nchini Vee Money yuko mmoja tu. Karibu kila chipukizi sasa anatamani kuwa kama Vee Money kwa namna alivyoibuka na kuwa matawi ya juu, tena ndani ya muda mfupi tu.

Kama zali tu

Vee Money hakuanza maisha katika muziki kama wasanii wengine walivyofanya. Staa huyo alianza kama mtangazaji tena katika vituo vikubwa vya televisheni nje ya nchi na baadaye hapa nchini. Vee Money alifanikiwa kupata nafasi ya kuendesha shoo kadhaa katika kituo cha MTV baada ya kushinda katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo mwaka 2007 wakati huo akiwa na miaka 19 tu.

Aliendesha shoo kadhaa na MTV kama ‘MTV Staying Alive’, redi kapeti katika Sauti za Busara kwa miaka mitatu mfululizo kupitia tuzo za ‘MTV African Music Awards’ pamoja na ‘Epic Bongo Star Search’ kupitia kituo cha ITV. Hakika alifana katika tuzo hizi.

Video zake sasa

Katika vitu ambavyo vinamweka Vee Money katika daraja tofauti na la wasanii wenzake ni ubora wa video zake. Mpaka sasa ndiye msanii pekee wa kike wa Tanzania ambaye video zake zinachezwa katika vituo vya nje vya Trace na MTV.

Vee Money alikiri kupokea fungu la maana kutoka katika vituo hivyo kutokana na kucheza kazi zake. Video bora zaidi ni ile ya ‘Nobody But Me’, ‘Never Ever’ na video yake mpya ya ‘Niroge’ ambayo inaonekana kutikisa kwa sasa. Ukitazama kituo cha Trace ndani ya DSTV huwezi kumaliza masaa mawili bila kuona kibao hicho kikipigwa.

Kolabo zake

Hapa ndipo Vee Money anapozidi kuwaacha wasanii wenzake wa kike. Anamshinda hadi Lady Jay Dee ‘Ndi ndi ndi’ ambaye ndiye msanii bora wa kike wa nyakati zote nchini. Vee Money bhana anafanya kolabo za maana. Wakati wasanii wa kike nchini wakizunguka kufanya kolabo na Chidi Benz ama Baraka Da Prince, Mdee anakwenda mbali.

Katika nyimbo zake tatu alizofanya kolabo, mbili kafanya na wasanii wa nje moja kaimba na Barnaba Boy. Katika nyimbo zake nyingine Vanessa ameshirikiana na Burna Boy pamoja na KO wote wa Afrika Kusini.

Shoo zake

Umewahi kusikia shoo yake hapa bongo? Ni nadra sana. Vee Money mara nyingi amekuwa akifanya shoo zake nje, hasa katika nchi za Nigeria na Afrika Kusini. Shoo kubwa ambayo amewahi kufanya hapa bongo ni ile ya Kill Music Tour.

Majuzi tu alifanya shoo jukwaa moja na Shilole Ukumbi wa Billicanz. Ni chache sana. Hata hivyo, katika shoo anazofanya ni lazima upagawe. Wakati akiwa na nyimbo mbili tu za ‘Closer’ na Come Over’, Vanessa aliweza kulikosha jukwaa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza.

Katika shoo zake huwa na madansa wake wawili wa kike ambao husafiri nao maeneo mbalimbai duniani. Watatu hao hucheza kwa pamoja tena kwa madoido kama Yamoto Band. Wakati Vee Money anaimba madansa hao hucheza na akimaliza kuimba hujiunga na madansa hao na kuvunja kinoma.

Tuzo kibao

Miaka mitatu mituzo kibao. Vee Money ana tuzo nyingi usiambiwe na mtu. Alianza kushinda tuzo zake mbili za kwanza kabla hata ya kuachia wimbo binafsi. Tuzo hizo za mwanzo zilikuwa za Kilimanjaro Tanzania Music (KTMA) katika vipengele vya kolabo bora pamoja na wimbo bora wa Afro Pop kupitia wimbo wa Me and You alioshirikishwa na Ommy Dimpoz.

Baada ya hapo Vanessa alishinda tuzo ya wimbo bora wa RnB wa mwaka kupitia singo yake ya ‘Closer’ mwaka 2014. Mwaka huo huo alishinda tena tuzo ya msanii bora wa kike Afrika Mashariki kupitia tuzo za All Africa Music huko Nigeria.

Mwaka 2015 Vee Money alishinda tuzo za Mtumbuizaji Bora wa kike na msanii bora wa kike nchini katika tuzo za Kili Music kupitia wimbo wake wa ‘Hawajui’. Mwaka huo ulikuwa wa bahati kwa Vanessa ambapo, alishinda tuzo ya msanii bora wa kike wa Afrika Mashariki katika tuzo za African Music Magazine huko Marekani kabla ya kushinda tena tuzo ya wimbo bora wa Pop Afrika katika tuzo za All Africa.

Vanessa amelishinda pia tuzo ya msanii bora wa kike Afrika Mashariki katika fasheni na mwaka huu ameteuliwa kuwania tuzo za Kora pamoja na za ‘Nigeria Interta inment Award’ kama mwimbaji bora wa kike Afrika, tuzo hizo zitafanyika Septemba mwaka huu nchini Marekani.

Matangazo

Vee Money ana nyota usiambiwe na mtu. Hapa nchini ndiye balozi wa kampuni ya Samsung na bila shaka utakuwa umemuona mara kadhaa katika matangazo ya simu za kampuni hiyo.

Vee alikuwa pia katika matangazo ya ‘Switch On’ ya Airtel ambapo, alipiga mkwanja wa maana. Vee ni balozi pia wa Crown Paints hapa nchini.

Nyota huyo amekuwa akihusika pia katika kampeni kadhaa za Umoja wa Mataifa (UN) nchini. Alishiriki katika shoo za Coke Studio Afrika msimu wa pili kwa kufanya kolabo na wasanii wakubwa Afrika kama 2face na wengineo.

Mahusiano yake

Kila mtu anapenda kuwa karibu na waridi. Hiki ndicho kilichotokea kwa mwimbaji Jux, ambaye aliwahi mapema kujiweka kwa Vee Money na sasa mahusiano yao yamedumu kwa zaidi ya miaka miwili. Vee Money na Jux wamekuwa miongoni mwa wasanii wachache kuweka mahusiano yao hadharani, huku wakikwepa skendo za mitaani ambazo zitawavuruga. Mpaka sasa wawili hao yanatajwa kuwa miongoni mwa wapenzi bora zaidi.