Buriani George Otieno Okumu ‘George Tyson’

Marehemu George Otieno Okumu ‘George Tyson’

Muktasari:

  • Tyson aliyabadilisha mapenzi ya Watanzania wote na kuwafanya waanze kupenda kazi zao alipotengeza Filamu ya Girlfriend.
  • George Tyson akiwa na Joyce Kiria wakaanzisha kipindi hicho na mtayarishaji huyo ndiye aliyebuni jina la Bongo Movie ambalo limeshamiri na kushika kasi mpaka leo hii.
  • Tyson alifunga ndoa na Msanii Ivonycherryl Ngatikwa ‘Monalisa’  na kufanikiwa kupata  mtoto mmoja wa kike aitwaye Sonia.

MEI mwaka huu umekuwa ni mwezi mchungu sana kwa familia ya Bongo Movie.

Simanzi imetawala katika mioyo ya wasanii, maprodyuza na wapenda filamu kwa jumla.

Mwezi huo ulianza kuwa mchungu baada ya tasnia hiyo kumpoteza msanii na mwongozaji wa filamu, Adam Kuambiana, aliyefariki Alhamisi ya Mei 17,  baada ya kuugua vidonda vya tumbo.

Jumanne ya Mei 27, Msanii Rachel Haule naye aliaga baada ya kujifungua katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar.

Majonzi ya Rachel yakiwa bado  hayajasahaulika, msiba mkubwa unatokea tena, mwongozaji, mtayarishaji, mwalimu wa wasanii, George Otieno Okumu ‘George Tyson’ kama alivyofahamika na wengi, amefariki dunia Mei 30, kwa ajali ya gari, maeneo ya Gairo Morogoro.

George Tyson ndiye dira ya mafanikio ya tasnia ya filamu Tanzania, baada ya vituo vingi vya runinga nchini kuwamiliki waigizaji waliowahi kutamba katika vipindi vya redio lakini walishindwa kuonyesha upinzani kutoka kwa waigizaji wa Kenya walikuwa wakitamba na Igizo la Tausi ambalo lilipendwa sana na Watanzania.

George Tyson aliibukia  katika Kundi la Nyota Ensemble lililokuwa na wasanii wanne tu, Richie,  Bishanga, Aisha na Waridi.

Mtayarishaji huyo aliibua vipaji vingine vingi vya akina Monalisa, Natasha, Mzee Kamba Ulaya na wengine wengi waliotoa upinzani mkali walipoibuka na Igizo la Nyota.

Makundi mengine yaibuka

Kutokana na changamoto ya kulipanua kundi hilo na kuwa kubwa, makundi mengine yakaibuka na kuzalisha vipaji kadhaa vya wasanii ambao leo hii ndio wanaotamba kwenye filamu za Kitanzania.

Mwaka 2000, George Tyson aliachana na Nyota Ensemble na kuanzisha Kundi la Nyota Academia baada ya kundi la awali kugawanyika.

Hata hivyo, mwamko aliouanzisha ukawa mkubwa na kuendelezwa na makundi ya Kaole Sanaa Group, Kidedea, Splendid na Kamanda Family.

Wanafunzi wengi wa George Tyson wakatawanyika na kutoa msaada kwa makundi mapya na kwa kufuata nyayo zake.

Filamu

Utengenezaji wa filamu kwa watu binafsi hapa nchini ulianza mwaka 1995 pale Filamu ya Shamba kubwa ilipotengenezwa jijini Tanga, lakini Watanzania walikuwa bado hawajaamka na kuendelea kupenda filamu za kutoka nje kama India, Nigeria na Ulaya.

Mwaka 2002/ 03, Tyson aliyabadilisha mapenzi ya Watanzania wote na kuwafanya waanze kupenda kazi zao alipotengeza Filamu ya Girlfriend.

Ni kazi iliyoshirikisha wasanii wa kila fani wakiwemo wale wa Muziki  wa Kizazi Kipya, ‘Bongo Fleva’ waliokuwa juu wakati huo kama vile GK, AY, Jay Mo, TID na wasanii waliotamba katika maigizo.

Mwigizaji mkubwa zaidi katika filamu hiyo alikuwa ni Sauda Simba Kilumanga.

George Tyson alikuwa na kipaji cha kipekee kwani baadaye aliongoza filamu ya Dilema na kuwashirikisha watu mashuhuri wakiwemo wanasiasa na watangazaji.

Msanii Baraza kutoka Kenya alishiriki sambamba na akina Jenerali Ulimwengu, Mheshimiwa Mudhihir Mohammed Mudhihir na wengineo.

Mwasisi wa neno Bongo Movie

Pamoja na filamu kuweza kutoa ajira kushika kasi lakini hakukuwa na vipindi maalumu vilivyokuwa vikiizungumzia tasnia hiyo.

George Tyson akiwa na Joyce Kiria wakaanzisha kipindi hicho na mtayarishaji huyo ndiye aliyebuni jina la Bongo Movie ambalo limeshamiri na kushika kasi mpaka leo hii.

Ni raia wa Kenya

Mbali na hayo, mwongozaji huyo wa filamu wa kimataifa amefanya mambo makubwa sana kwa kuikuza tasnia ya filamu pamoja na kwamba hakuwa  Mtanzania, bali ni  raia wa Kenya aliyekuja nchini kuwafumbua macho Watanzania waliokuwa wamelala.

Familia

Tyson alifunga ndoa na Msanii Ivonycherryl Ngatikwa ‘Monalisa’  na kufanikiwa kupata  mtoto mmoja wa kike aitwaye Sonia.

Hata hivyo ndoa hiyo haikudumu, ilivunjika pamoja na kwamba wawili  hao waliendelea kuwa marafiki wakubwa  kwa kufanya kazi za sanaa pamoja.

Kwenye kazi, Monalisa amepoteza rafiki muhimu sana katika maisha yake lakini kifamilia  msanii huyo amempoteza mwenza wake ambaye ni baba mtoto wake.

Amekufa akiitumikia nchi

Tyson alikuwa mtayarishaji mkuu  wa vipindi vya  Wanawake Live kinachotangazwa na Joyce Kiria na Mboni Show.

Kipindi cha Mboni Show ndicho kilichomfanya aende Dodoma katika Kijiji cha Chilonwa, Chamwino kutoa msaada wa madawati katika Shule ya Msingi ya Chaula, shughuli ambayo siku zote imekuwa ikifanywa na wanasiasa wanapoitumikia nchi.

Baada ya kumaliza shughuli hiyo akiwa kama prodyuza aliyerekodi kipindi hicho kwa ajili ya kukionyesha kwa Watanzania mauti yalimkuta saa 12 jioni saa 4  tangu aanze safari ya kurudi Dar es Salaam.

Katika gari hilo walikuwa watu wanane lakini ni George Tyson  pekee ndiye aliyepoteza maisha na wengine wamepata majeraha.

Kuzikwa Kisumu

Jumamosi Mei 31, mwili wake ulisafirishwa hadi Dar es Salaam na kuifadhiwa katika Hospitali ya Mikocheni.

Kesho Jumatano, mwili wake utaagwa katika Viwanja vya Leaders Kinondoni na jioni utasafirishwa hadi Nairobi na baadaye kuelekea Kisumu nchini Kenya kwa mazishi.

Pengo lake limeiacha tasnia katika wakati mgumu lakini hakuna jinsi, tumwombee.

 Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.