Bifu hizi zimesumbua 2016

Thursday December 15 2016

 

By Thomas Matiko

TARATIBU mwaka 2016 unazidi kuyoyoma huku zikiwa zimesalia takriban siku 16 tuukaribishe Mwaka Mpya wa 2017. Kumekuwepo na matukio mengi katika ulingo wa burudani nchini na kimataifa. Moja kati ya mambo yaliyotikisa mwaka huu ni bifu za wasanii mbalimbali hapa nchini, Afrika Mashariki na duniani kwa jumla. Cheki bifu zilizotikisa kinoma noma.

OMMY DIMPOZ Vs DIAMOND

Kwa zaidi ya miaka mitatu hivi, bifu kubwa ya Diamond ambayo wengi wamekuwa wakiifahamu ni ile iliyopo kati yake na Ali Kiba. Lakini juzi kati, imebainika kuwa Diamond ameingia katika bifu na Ommy, ambaye alikuwa mshkaji wake wa karibu. Chanzo cha bifu hilo ni mambo ya kimasilahi zaidi na kutotendeana haki kipindi cha nyuma. Hata hivyo, mzizi ulijikita zaidi baada ya Ommy kuanzisha uhusiano wa ukaribu na Wema Sepetu baada ya kubwagana na Diamond.

Ommy alionekana kuwa karibu na Wema na hata akaishia kumtumia katika wimbo wake wa ‘Wanjera’, jambo ambalo linatajwa halikumfurahisha baba Tiffah.

Hata hivyo, Ommy amezidi kumtia kichefu chefu Baba Tiffah baada ya hivi majuzi kuungana na hasimu wake Ali Kiba na kuachia kolabo ya ‘Kajiandae’. Siku kadhaa baadaye, Diamond alichia kolabo yake na Rich Mavoko ‘Kokoro’ na baadhi ya mashairi yanadaiwa kuwa ni ya kumlenga Ommy.

Mara tu baada ya kutoka kwa ngoma hiyo, Ommy na Diamonds walianza kurushiana cheche za maneno kila mmoja akimkashifu mwenzake kwa ishu mbalimbali. Ommy alidai muziki wa Diamond ni wa kijanja janja na kwamba, hununua ‘views’ kwenye Youtube ili kumwezesha kutengeneza mkwanja.

Malumbano hayo yameendelea na hivi majuzi kwenye mahojiano ya redioni, Diamond kafunguka kuhusu jitihada zilizowahi kufanywa na Ommy ili kumaliza bifu lao ikiwemo kumpigia simu na kumtuma meneja wake Sallam azungumze na Diamond, kitu ambacho mzee wa ‘Wanjera’ kakanusha.

“Kashatuma watu wengi sana, kashamtuma Sallam na alishanipigia simu nikashindwa kupokea, nitaongea naye nini? Mipaka ilishavuka halafu mimi ni Mwislamu. Sina matatizo na watu ndiyo maana wakijaribu kushindana na mimi huwa wanashindwa,” alisema Diamond.

Hata hivyo, kupitia Twitter, Ommy alikana: “Aisee kumbe Sallam kila siku unavyonibembeleza tuyamalize na mwana (Diamond) kumbe nakutuma, kweli nyie profeshenooo,” alitwiti Ommy.

VISITA Vs GRAND PA RECORDS

Ni bifu nyingine ambayo ilionekana kumlenga moja kwa moja mmiliki wa Grand Pa Records, Reffigah huko nchi jirani ya Kenya ambaye katika busara zake aliamua kusalia kimya.

Hii ni baada ya produsa wake matata aliyekuwa amemtunuku cheo cha Naibu Rais wa Grand Pa, Vista kuikacha lebo hiyo akidai kuwa jamaa alikuwa akinufaika kwa huduma zake huku yeye akibakia kapa. Kuondoka ghafla kwa Vista mmoja wa watetezi sugu wa lebo hiyo, kuliwashtua mashabiki wengi kwani alionekana kuwa karibu sana na Reffigah.

Licha ya Reffigah kuupiga uzi mdomo wake kuhusu hili, vyanzo vimearifu kuwa tatizo lilitokana na Visita kuuza beats za ngoma ya msanii chipukizi ndani ya lebo hiyo pasi na idhini ya Reffigah.

Visita anaamini alistahili kwa sababu yeye ndiye amekuwa akitengeneza beast pale na baada ya kuondoka aliungana na mwenzake Kenrazy, aliyeikacha lebo hiyo pia na kuunda yao Hela Records. Vita hiyo ilitikisa nchi jirani, pia moshi wake kufuka huku nchini hasa kwa wasanii waliojihusisha na lebo hiyo.

KANYE WEST Vs JAY Z/SNOOP DOGG

Rapa Kanye kwa sasa yupo katika hali mbaya ya kiakili kwa kile kinachodaiwa kusababishwa na msongo wa mawazo. Matatizo katika ndoa na kutengwa na rafiki yake wa siku nyingi, rapa mkongwe Jay Z imeonekana kumwathiri sana Kanye.

Siku kadhaa zimepita Kanye alilazimika kusitisha ziara ya shoo zake ya Siant Pablo na kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ya kiakili na kisaikolojia.

Katika kumbi nyingi ambazo alipanda kutumbuiza kwenye ziara yake hiyo kabla ya kukatiza, Kanye amekuwa akimtupia madongo Jay Z kwa kumtelekeza na hata kuacha kabisa kwenda kumtembelea kama ilivyokuwa hapo zamani.

Hata hivyo, kambi ya Jay Z imesema tangu Kanye afunge ndoa, alibadilika na hasomeki kabisa na ndiyo chanzo cha yeye kujiweka mbali naye.

Ukimweka pembeni Jay Z, Kanye pia amekuwa akiwakashifu wakongwe wengine wa hiphop akiwemo Snoop ambaye naye juzi alimtemea shombo;

“Mimi huvuta bangi ila haiwezi ikakufanya utamke maneno kama yale, sijui Kanye anavuta nini kiasi cha kumfanya apande jukwani na kuanza kutukana watu wasiojihusisha na mambo yake bila mpango,” Snoop alicharuka kwenye kipande cha video alichorekodi na kutupia Instagramu.

FEMI ONE Vs NJERI/SOSOUN

Mwishoni mwa Oktoba rapa wa kike Femi One ambaye muziki wake umeanza kutamaba Afrika Mashariki aliingia studio na kuachia distraki ‘Pilau Njeri’ akiwachana marapa wenzake wa kike. Licha ya yeye kudai aliwalenga marapa wenzake kwa kuzembea kazini na wachache kuendelea kushika chati kwenye ‘game’ akiwemo Wangechi, wanaoendelea kufanya muziki huku akionekana kumlenga zaidi rapa Njeri, ambaye kazi zake nyingi anazifanya kwa lugha ya Kikuyu.

Kwenye mahojiano, Femi One alikanusha kuwa traki hiyo ilimlenga msanii huyo na kusisitiza kwamba, ilikuwa ni ya kuwazindua wenzake wanaosinzia ili wainuke na kukaza.

“Wamelala, hiyo ngoma ilikuwa ni ya kuwachangamshe warudi studio kwa sababu kumenyamaza sana,” Femi One alidai.

Hata hivyo, baada ya wiki mbili tu, Njeri alijibu distraki hiyo ya ‘Pilau Njeri’ na ‘Conoka’ ambapo katika mashairi yake alimchana Femi kuanzia fasheni, maumbile na usanii wake.

Ila ilibainika kuwa wawili hao walianza kuwa na chuki ya kimya kimya baada ya menejimenti ya Njeri kumtokea Femi One kwa ajili ya kufanya kolabo, lakini hasimu wake huyo akamyeyusha.

Kwa upande wa Sosoun, alisema hana uhakika ikiwa kweli Femi One alikuwa akimlenga ila kama ndivyo ilivyo basi kama akiamua kumjibu basi itakuwa ndio mwisho wa taaluma ya mwenzake huyo.

Sosoun aliongeza kwamba huwa ana heshima sana kwa wanawake na kabla ya kujibu lazima awe na uhakika kuwa Femi One alimlenga yeye.

Hata hivyo, pamoja na yote kazi hiyo iliwapa fursa wasanii wengine wa kike chipukizi kutoka.