Nyumbani kwa Rose Muhando, ulinzi si wa kitoto

Muktasari:

Nikiwa huko nakutana na mwanamama ambaye siku za karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikilitaja jina lake kwa stori zake akituhumiwa kwa mambo mbalimbali.

NI jioni, saa moja kasoro giza likiwa limeanza kushika hatamu ndani ya Mji wa Dodoma, Makao Makuu ya Tanzania ambako Rais John Pombe Magufuli ameagiza vigogo wote Serikalini waanze kuhamia huko.

Nikiwa huko nakutana na mwanamama ambaye siku za karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikilitaja jina lake kwa stori zake akituhumiwa kwa mambo mbalimbali.

Ni msanii nguli wa nyimbo za injili, Rose Muhando ambaye mbali na kuwavutia watu kwa sauti yake nyororo, utunzi wa mashairi, midundo na uwezo wa kumiliki jukwaa vimekuwa vikiwavutia wadau mbalimbali bila kujali utofauti wa imani za dini.

Rose alikuwa ameongozana na vijana wake watano wa shoo ambao amekuwa akiwatumia kucheza katika nyimbo anazorekodi na kwenye majukwaa anapoalikwa kuimba na hapo ilikuwa ni nje ya geti la nyumba yake iliyopo Ipagala nje kidogo ya mji huo.

Hamu kubwa ni kutaka kuufahamu ukweli juu ya mambo hayo anayohusishwa nayo ikiwamo kutumia madawa ya kulevya yanayodaiwa kumfilisi mali zake pamoja na utapeli wa pesa kwa wachungaji.

Alipomkaribia mwandishi ambaye alikuwa ameweka kambi Dodoma kwa siku kadhaa ili tu kuupata ukweli wa mambo, alishtuka lakini baada ya kufahamu anachokihitaji mwandishi aliahidi kutoa ushirikiano siku ya pili kwani alikuwa amechoka kwani alikuwa ametoka kufanya huduma ya Mungu (kuimba) kijiji cha jirani.

Siku hiyo ya pili asubuhi na mapema ndipo mwandishi alipoonana kwa karibu na mwanamama huyo mcheshi ambaye pia ni mama wa watoto watatu, Gift, Nicolas na Maximilian. Kimwonekano ana mwili unaoashiria mzima wa afya, lakini anashindwa kujiachia katika miondoko kutokana na maumivu ya miguu ambayo imevimba kidogo.

 

KUINGIA NDANI KWAKE UJIPANGE

Rose ana nyumba kubwa ya kifahari na kwa mahesabu ya haraka haraka thamani yake si chini ya Sh. 200 milioni. Nje ina uzio mkubwa na geti ambalo linaimarisha ulinzi kwani huwa linafungwa wakati wote.

Ukifika bila mawasiliano naye utapokewa na wenyeji ukiwa nje ya geti na kama huna maelezo yanayojitosheleza utaondokea hukohuko bila mafanikio na hapo, Rose anafafanua sababu ya kufanya hivyo.

“Nafanya hivyo kwa sababu katika kipindi hiki, nimepitia mambo magumu, nachukua tahadhari kutokana na maadui niliokuwa nao, wapo wanaofika na kunitishia maisha na wengine wanakuja na mbinu zao nyingine ilimradi kukuharibia maisha,”anasema Rose na kuongeza: “Jana ulipoondoka tu usiku saa mbili, alikuja mtu akazungumza maneno mengi ya vitisho mimi naogopa hali hiyo.

 

NYUMBANI KWAKE

Mbali na mjengo huo wa kifahari ambao anaishi na watoto wake na baadhi ya wafanyakazi, ndani ya uzio kuna sehemu kubwa ya wazi ambayo anaitumia kwa ajili ya mazoezi anapokuwa na shoo au anapojiandaa kurekodi video.

Kwa nyuma ipo nyumba nyingine ambayo wanaishi vijana wake wa shoo na wafanyakazi wengine na upande wa pili wa jengo hilo dogo ametenga jiko la nje na stoo.

Ukiingia ndani ya nyumba hiyo kubwa inajitosheleza kwa kila kitu kuanzia vyumba vya kulala, sebule iliyopambwa kwa seti mbili za sofa, televisheni ya kisasa na urembo mwingine.

Ukutani kuna picha za watoto wake, sehemu ya kulia chakula kuna friji kubwa, kabati la vyombo na meza kubwa ya familia na jikoni kuna mambo yote yanayohitajika.

 

KWA NINI AMEKUWA KIMYA

Rose anasema, amekuwa kimya kwa sababu mbalimbali lakini anawaambia mashabiki wake yupo na anafanya maandalizi mengine: “Nipo hata hivyo kuna kazi nyingine nimeandaa ipo kwa Alex Msama bado haijatoka kutokana na mambo mbalimbali, ingawa naandaa kazi nyingine ninayotegemea kuikamilisha mwezi wa tatu mwakani tutakapojaaliwa. Nimeshaanza kuandaa baadhi ya nyimbo na nyingine naendelea kutunga, unajua kazi hizi huwa nasikiliza sauti ya Mungu aniambie niimbe nini.”

“Pia, nimekuwa nafanya huduma ya kuimba katika mikutano tofauti ndani na nje ya nchi kama hivi jana umenikuta natoka kijiji cha jirani kuimba na wiki iliyopita, nilikuwa Kenya ambako nilifanya huduma, Kisumu na Mombasa, nimeamua kufanya hivyo kwa sababu zangu,”anasema Rose.

 

KWELI ANATUMIA DAWA ZA KULEVYA

Baada ya kutajiwa tuhuma ya madawa ya kulenya, Rose anashtuka na kusema: “Situmii madawa na sitatumia, kama waliona ndiyo skendo itakayonimaliza wameshindwa, wanaofanya hivyo ni watu wanaotaka kunimaliza walitaka nifanye kazi zao, nikakataa.”

“Sijajiingiza na mambo hayo na wanavyozungumza nasikitika kwa sababu wanaiumiza familia yangu kisaikolojia, mimi ni mama wa watoto watatu na nina ndugu zangu, naambiwa mambo yote hayo kwa sababu sina mtu wa kunitetea,”anasema Rose.

Rose anaeleza sababu zinazomfanya watu waamini anatumia madawa ya kulevya, je ni sababu gani hizo, usikose kusoma gazeti la Mwanaspoti toleo la keshokutwa Alhamisi.