NANI MKALI? Vita ya Diamond na Ali Kiba yahamia Unguja

Monday November 14 2016

Ali Kiba (kushoto) na Diamond (kulia).

Ali Kiba (kushoto) na Diamond (kulia). PCHA|MTANDAO 

By MOHAMMED SAID, UNGUJA

HAKUNA ubishi kwamba nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, wanaotamba barani Afrika, Diamond Platinumz na Ali Kiba ndio wenye mashabiki wengi na wanaoungwa mkono kwenye makundi mengi ya mitandao ya kijamii kwa sasa.

Ingawa kiuhalisia wametofautiana kwenye mambo mengi, lakini huwezi kuzungumzia muziki wa kisasa bila kuwataja wakali hao.

Unaambiwa sasa upepo wa upinzani wa mastaa hao unaonekana kuvuka bahari, umehamia upande wa pili wa nchi ambapo ni visiwani Zanzibar kwenye tamasha la kimataifa la kila mwezi maarufu kama Usiku wa Mbalamwezi.

Juzi Jumamosi kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Zanzibar, Diamond alifanya shoo kisiwani hapa kwenye Usiku wa Mbalamwezi ambao hufanyika kwenye fukwe za Hoteli  ya Kendwa Rocks.

Msanii huyo anayetamba na Wimbo wa ‘Salome’ alipiga shoo ya saa tatu ambayo iliwapagawisha mashabiki, huku Diamond mwenyewe akiwa haamini jinsi raia wa kigeni walivyokuwa wamejazana kwenye tamasha hilo.

Jambo ambalo lilimpandisha mzuka huku mashabiki wakishinikiza kukesha naye lakini alilazimika kushuka jukwaani saa 9 usiku.

Tofauti na matamasha ya hivi karibuni lile la juzi lilijaza mashabiki 3,000 kutoka mikoa ya Zanzibar, Dar es Salaam, Arusha na nchi za Kenya na Uganda pamoja na watalii kutoka mataifa mbalimbali waliopo Zanzibar, walijazana katika fukwe hizo kumshuhudia msanii huyo  aliyeitangaza zaidi Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Mashabiki wengi walionekana kutoamini kama kweli msanii huyo angefanya shoo Zanzibar, kwani walisikika wakisema amekuwa hashikiki kwa sasa. Lakini sasa katika kile kinachoonekana kama maboresho kwenye tamasha hilo, mratibu wake, Ali Kilupi alisema kwenye shoo ijayo ambayo ni ya kufunga mwaka, Kiba atakuwa ndani ya nyumba.

Jambo ambalo huenda likachukuliwa na mashabiki kama kutia chumvi ushindani baina ya mastaa hao, kwani huenda Kiba akaja na utamu zaidi kutaka kumfunika mpinzani wake.

Wakipepewa na upepo mwanana wa Bahari ya Hindi, kwenye shoo ya juzi mashabiki walianza kufurika kuanzia saa 12.00 jioni, walionekana kuwa na shauku kubwa ya kumuona Diamond na kusikia vibao vyake vinavyotamba katika studio mbalimbali, ndani na nje ya nchi.

Awali zilianza kutumbuiza bendi mbalimbali za kiutamaduni za Zanzibar pamoja na Kundi la Wasafi, kabla ya Diamond mwenyewe kuonekana jukwaani na kuibua shangwe za kutosha saa 6 usiku.

‘‘Ni mara yangu ya kwanza kufanya shoo mahali hapa, nimefurahi sana, nawapenda sana Wazanzibari, nitawapa kile kitu roho inapenda,” alisema Diamond alipowasalimia mashabiki huku wanawake wakilipuka kwa shangwe.

Bila hiyana alilishambulia vilivyo jukwaa bila kupumzika, akiporomosha vibao mbalimbali, ambavyo siyo tu kuwa viligusa hisia za mashabiki, pia viliibua vifijo, hoi hoi na nderemo kadiri muda ulivyosonga.

Wakati msanii huyo akilishambulia jukwaa kwa hasira, madansa nao walionyesha umahiri mkubwa katika unenguaji, kiasi cha kuwafanya mashabiki kushindwa kuamini kile kinachotokea.

Mbali na mwanamuziki huyo kupiga vibao mbalimbali, lakini Wimbo wake wa Salome, ndiyo ulioonekana kuteka nyoyo zaidi za mashabiki, hali iliyomlazimu kuurudia mara tatu, kila baada ya kumaliza kuimba kutokana na shinikizo la mashabiki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Diamond alisema Zanzibar ni mahali tulivu na panapofaa kwa maonyesho kwa kigezo kuwa, kuna mashabiki wengi, hususan wa muziki wa Bongofleva.

Alisema kupitia Tamasha la Usiku wa Mbalamwezi,  serikali inaweza kuongeza makusanyo ya fedha kutoka kwenye hoteli, kwani tamasha hilo huvuta wageni wengi, akiamini kuwa watalii wengi ni wapenzi wa muziki wa Kiafrika.

Alitoa wito kwa bodi zinazosimamia utalii nchini, kuwa na bajeti itakayowapa fursa  wasanii wa Tanzania kuwashajihisha wageni kutoka nje kuja nchini, badala ya kutumia fedha nyingi kwa ajili kushiriki maonyesho nje ya nchi.

‘‘Matamasha kama haya yakiendelezwa, kuratibiwa na kupangwa vyema, wageni wengi kutoka nje watakuja, hivi ni vitu vinavyovutia wageni, wanapenda sana muziki wa Kiafrika,” alisema.

Wakati msanii Diamond na vikundi vingine vya sanaa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar vikinogesha tamasha hilo katika fukwe za Kendwa Rocks zilizopo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, imebainika kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la wageni kwenye fukwe za Zanzibar katika wiki za hivi karibuni.

Huku ikielezwa tamasha hilo pamoja na mapumziko ya mwishoni mwa mwaka yakitajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kunoga huko kwa mji wa Zanzibar.

Tamasha hilo linaheshimika visiwani hapa kutokana na kukidhi viwango vyote vya ubora na kufikia malengo ya kuukuza muziki, utamaduni na kuwakutanisha wasanii kutoka mataifa mbalimbali ambao hupata nafasi ya kuonyesha kazi zao na kubadilisha ujuzi na uzoefu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli ya Kendwa Rocks ambao ndio waandaji wa ‘Full Moon Party’, Ali Kilupi alithibitisha kwamba tamasha lijalo msanii Ali Kiba atatua visiwani hapa kwa ajili ya kuwaburudisha wageni mbalimbali. Pia ikiwa ni sehemu ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.

Alisisitiza kwamba shoo hiyo lengo lake kubwa ni kuutangaza utamaduni wa Tanzania kwa jumla, lakini vilevile kuonyesha uwezo wa wasanii wazawa kwa wageni.