ACHA KABISA: Wakala wa Ozil achachamaa vibaya

Muktasari:

Dr Erkut Sogut, wakala wa kiungo mchezeshaji wa Arsenal, Mesut Ozil ameibuka na kuwabwatukia watu wote wanaomlaumu staa huyo kwa vipigo vya Arsenal akidai kwamba mteja wake amegeuzwa kuwa mbuzi wa kafara kutoka na matokeo hayo.

PALE Arsenal kwa sasa kila mtu na lake. Hakuna amani tena. Kila mtu anaongea. Kila mtu anamwaga sumu. Na sasa imekuwa zamu ya mawakala wa wachezaji. Mmoja wao amejitokeza kumtetea mteja wake akidai hahusiki na vipigo vyao.

Dr Erkut Sogut, wakala wa kiungo mchezeshaji wa Arsenal, Mesut Ozil ameibuka na kuwabwatukia watu wote wanaomlaumu staa huyo kwa vipigo vya Arsenal akidai kwamba mteja wake amegeuzwa kuwa mbuzi wa kafara kutoka na matokeo hayo.

Ozil alianza tena katika pambano dhidi ya Bayern Munich ambalo Arsenal walichapwa 5-1 Allianz Arena Jumatano usiku licha ya wachambuzi na baadhi ya mashabiki kutaka nyota huyo asipangwe kutokana na kushindwa kung’ara katika mechi kubwa.

Ozil alichemsha tena katika pambano hilo na msimu huu amekuwa akishindwa kuonyesha makali yake katika mechi kubwa huku wiki mbili zilizopita akipwaya katika pambano dhidi ya Chelsea ambalo Arsenal alichapwa mabao 3-0 Stamford Bridge.

“Kukosolewa ni kitu cha kawaida kama mchezaji akicheza vibaya. Lakini Mesut anaamini kwamba watu hawaangalii kiwango chake, wanamtumia kama kisingizio cha timu baada ya matokeo mabaya. Inawezekana vipi kwa mtu anayecheza namba 10 kutengeneza nafasi kama hana mpira?” alihoji Sogut.

“Soka ni mchezo wa timu na Arsenal haichezi vizuri kama timu. Wachezaji 11 walikuwa uwanjani lakini Mesut ndiye aliyekosolewa zaidi. Yeye ndiye aliyekuwa sababu ya Arsenal kufungwa mabao matano?” alihoji wakala huyo.

Wakala huyo aliendelea kumtetea staa huyo wa zamani wa Werder Bremen na Real Madrid kutokana na hoja kwamba amekuwa hafanyi lolote katika mechi kubwa.

“Sikubaliani na hoja kwamba Mesut amekuwa hana mchango katika mechi kubwa. Vipi kuhusu ushindi dhidi ya Chelsea Emirates au dhidi ya Manchester United mwaka mmoja kabla? Vipi kuhusu mechi za Ujerumani dhidi ya Italia na Ufaransa katika michuano ya Euro 2016?”

“Siku zote watu wanasema Mesut huwa hapigani uwanjani au kufanya tackling, kwamba huwa anaonekana hana ari, lakini hivyo ndivyo alivyo. Niamini mimi ana tamaa kubwa ya kupata mafanikio. Kama mambo hayaendi sawa huwa anachukia na anaonyesha. Mbona anakuwa hivi hivi Arsenal ikicheza vizuri?”

Msimu huu Ozil amepiga pasi nne tu za mabao, ikiwa ni tofauti kubwa na msimu uliopita ambapo alipiga pasi 19. Kuna wasiwasi kwamba huenda akaondoka mwishoni mwa msimu wakati huu akiwa bado hajasaini mkataba mpya huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao.

Licha ya kukwama kwa mazungumzo ya mkataba mpya, Sogut amesisitiza kwamba Ozil ana furaha na maisha ya klabuni hapo na ataendelea kujikita na kupambana katika siku zote za mkataba wake. “Mesut amejifunga katika klabu hii. Hakuna shaka kwamba atacheza kwa asilimia 100 akiwa kama mchezaji wa kulipwa na kujikita katika timu kadri anavyochezea Arsenal. Hakuna kitakachobadilika. Anaomba samahani kwa mashabiki, anaomba samahani kwa sababu yeye na wachezaji wenzake hawakuwapa mashabiki matokeo mazuri Munich,” alimaliza Sogurt.

Ozil alitua klabuni hapo katika dirisha la majira ya joto mwaka 2013 akitokea Real Madrid kwa dau la uhamisho la Pauni 42 milioni ambalo lilimfanya awe mchezaji ghali wa muda wote katika kikosi cha Arsenal.

Kiwango chake kimekuwa kikisua mara kwa mara huku akikosa mwendelezo wa ubora.

Yeye na staa mwingine wa Arsenal, Alexis Sanchez wameripotiwa kudai dau kubwa la mshahara katika ofa za mikataba mipya na mpaka sasa bado hakuna makubaliano na Arsenal huku ikitabiriwa kuwa wanaweza kuuzwa mwishoni mwa msimu huu kwa ajili ya kuepuka kuondoka bure mwishoni mwa msimu ujao.