Van Persie afichua siri ya kichapo cha Arsenal

Muktasari:

  • Staa huyo wa Manchester United, alisema ilikuwa ni lazima Arsenal ife kwenye mchezo huo kwa sababu walifahamu kila kitu cha timu hiyo inayonolewa na Mfaransa Arsene Wenger.

MANCHESTER, ENGLAND

STRAIKA aliyeiua Arsenal juzi Jumapili, Robin van Persie, amefichua siri kwamba Manchester United inatambua udhaifu wa wapinzani wao na ikaufanyia kazi mazoezini kabla ya kuwachapa bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu England.

Staa huyo wa Manchester United, alisema ilikuwa ni lazima Arsenal ife kwenye mchezo huo kwa sababu walifahamu kila kitu cha timu hiyo inayonolewa na Mfaransa Arsene Wenger.

Alipoulizwa kuhusu mechi hiyo dhidi ya waajiri wake wa zamani, Van Persie, 30, ambaye alifunga bao hilo pekee alisema waliingia na mbinu maalumu ambayo ni sumu ya Washika Bunduki hao wa London.

Van Persie alisema: “Tulikuwa na mfumo tofauti kidogo kwa sababu Arsenal wanakariri. Wana uchezaji wao huohuo wa kila siku, ambao mimi naufahamu vizuri sana.

“Hivyo kuwafunga, unapaswa kuwabadilishia mchezo kidogo tu, hawana ujanja. Nadhani tulilifanya hilo kwa ufasaha karibu kila mtu.

“Ukimtazama Patrice Evra alikuwa akienda mbele kila wakati hata kama kulikuwa na mshambuliaji, hilo linakuonyesha tofauti fulani.

“Nadhani tulianza vizuri pia kwenye kipindi cha pili, licha ya kwamba wakati fulani tulikuwa na hofu japo hatukuwapa nafasi. Tulipata nafasi mbili nyingine kubwa tu, moja ya Wayne Rooney na nyingine ya Chris Smalling. Haikuwa mechi yenye nafasi nyingi, bali ni ya kimbinu zaidi, tulikuwa sawa.”