KWELI MZIKI: Ubingwa wa England sasa hauna mwenyewe, mambo yanaanza upya

PRESHA sasa imeshuka. Makocha wa timu zinazoshika Top Six kwenye Ligi Kuu England, ukimweka kando Antonio Conte wanakenua chinichini wakiamini kwamba mbio za kusaka ubingwa huo sasa zipo wazi, mambo yanaanza upya.

Msimamo unavyosomeka kwa sasa, timu inayoongoza ligi, Chelsea imetofautiana na timu inayoshika nafasi ya sita, Manchester United kwa pointi 10. Lakini, imeizidi timu inayoshika nafasi ya pili, Liverpool kwa pointi tano. Utamu zaidi, timu namba sita hadi namba mbili zimepishana pointi tano. Timu ya sita na timu inayoshika nafasi ya tatu, Tottenham Hotspur na nafasi ya nne, Manchester City zimetofautiana pointi tatu tu. Kwa tofauti hiyo, vita ya ubingwa ndiyo kwanza inaanza upya.

Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger amesema baada ya Chelsea kukubali kichapo kutoka kwa Spurs juzi Jumatano usiku, jambo hilo limeziweka mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kuwa wazi na sasa timu yoyote kati ya sita za juu zina uwezo wa kunyakua taji.

Wenger alisema mwanzoni Chelsea ilikuwa inakatisha tamaa kutokana na kushinda mfululizo mechi 13, lakini kwa kichapo hicho kimefanya pengo la pointi lisiongezeke na sasa timu nyingine zimepata matumaini ya kurudi kwenye mbio za ubingwa.

Alipoulizwa anaonaje mbio za ubingwa wa England msimu huu kama unahusisha timu sita, Wenger alisema kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia mechi yake ijayo ya Kombe la FA dhidi ya Preston, Mfaransa huyo alisema: “Inaonekana kuwa hivyo, Chelsea kwa sasa wanaweza kuona kama wapo salama, lakini matumaini mapya yameibuka kwa wengine. Mambo yanaanza upya.”

Wenger alisema ndani ya miezi miwili ijayo kila kitu kitafahamika wazi kuhusu bingwa wa ligi hiyo kwa sababu ni kipindi muhimu kwa timu zote zinazoshika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Ushindi huo wa Spurs kwa Chelsea, umeifanya Arsenal kuporomoka hadi kwenye nafasi ya tano katika msimu, pointi mbili tu zaidi ya Man United inayoshika namba tisa. Wenger na kikosi chake cha Arsenal amejikuta akiporomoka kwa kasi sana kwa siku za karibuni kutoka kwenye nafasi ya pili hadi ya tano na kilichotibua zaidi ni ile sare yake ya mabao 3-3 dhidi ya Bournemouth.

Baada ya kushinda kwa mechi sita mfululizo kwenye Ligi Kuu England na kushindwa kuonyesha tofauti yoyote kwenye msimamo wa ligi hiyo ikibaki kwenye nafasi ya sita, Man United sasa inaweza kupata mabadiliko kama itashinda mchezo wake ujao dhidi ya Liverpool uwanjani Old Trafford na kisha waliopo juu yao, Arsenal wakaendelea kusuasua. Utamu wa msimu huo ni kwamba, timu hizo sita zilizopo kileleni zitaanza kuchujana zenyewe kwa zenyewe kwa kukumbana kwenye ligi hiyo iliyoshuhudia mechi 20 kwa kila timu hadi sasa

Wenger kwa mara ya kwanza aliwapongeza mahasimu wake Spurs, hasa kwa viungo Dele Alli mfungaji wa mabao yote yaliyoizamisha Chelsea na Christian Eriksen, mpishi wa mabao yote hayo kwamba wamefanya kitu kizuri kuziweka hai mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.