Top four epl bana pumzi

Tuesday February 14 2017

STEVEN Gerrard anasema hivi, Arsenal na Manchester United zisahau kuhusu Top Four. Gwiji hilo la Anfield anaamini Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu itakuwa na Manchester City, Tottenham Hotspur, Liverpool na Chelsea na hivyo kwenye orodha ya timu za Top Six zinazochuana kuwamo Top Four, Arsene Wenger na Jose Mourinho hawatakuwa na chao.

“Arsenal itaondoshwa na Man United imejipa kazi ngumu ya kufanya,” alisema Gerrard.

Mwanaspoti linatazama Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu na kutambua kuna vita ngumu sana, si kitu unachoweza kuchukua kalamu na kuanza kuorodhesha tu timu kirahisi. Kuwamo ndani ya Top Four msimu huu unapaswa kugangamala. Mechi 13 zimabaki kabla ya ligi kufika mwisho na Mwanaspoti linatazama ratiba ya kila timu katika mechi zao zijazo kutambua kama itakuwa na uwezo wa kuvuka kizingiti na kuwamo kwenye orodha ya timu nne za juu ambazo ndizo hasa zinazofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Chelsea wao ni kama tayari imeshajiweka ndani ya Top Four na mechi zao 10 zijazo za nyumbani na ugenini itacheza na Swansea City, West Ham, Watford, Stoke City, Crystal Palace, Man City, Bournemouth, Man United, Southampton na Everton.

Spurs itacheza na Stoke City, Everton, Crystal Palace, Southampton, Burnley, Swansea City, Watford, Bournemouth, Leicester City na Arsenal, wakati Arsenal mechi zao 10 zijazo itakipiga na Liverpool, Leicester City, West Brom, Man City, West Ham, Crystal Palace, Middlesbrough, Sunderland, Tottenham na Man City na Liverpool itacheza na Leicester City, Arsenal, Burnley, Man City, Everton, Bournemouth, Stoke City, West Brom, Crystal Palace na Watford.

Man City mechi 10 zijazo za itacheza na Bournemouth, Sunderland, Stoke City, Liverpool, Arsenal, Chelsea, Hull City, Southampton, West Brom na Middlesbrough na Man United itakipiga na Bournemouth, Southampton, Middlesbrough, West Brom, Everton, Sunderland, Chelsea, Burnley, Swansea City na Arsenal.

Kwa kuzingatia ratiba ya kila timu, Mwanaspoti linaamini Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu itafahamika baada ya mechi hizo 10 za kila timu, ambazo kutakuwamo pia za wenyewe kwa wenyewe waliopo kwenye Top Six kwa sasa. Kwa wakati huu timu ya kutoka nafasi ya pili hadi sita pointi zilizowatofautisha hazizidi tatu, hivyo kama kila timu itashinda mechi nyingine zitakapokutana zenyewe vita yake itakuwa si ya kitoto!